Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Nyamizi Simon Mhoja (4 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema siku hii ya leo. Kingine nitoe pole kwa Chama Cha Mapinduzi hasa Wanatabora kwa kuondokewa na aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Mzee Nassoro Hamdani na mpendwa wetu Dada Munde Tambwe, Mbunge Mstaafu, Viti Maalum, Mkoa wa Tabora, wapumzike kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wenye ulemavu kwenye Dira ya Taifa ambayo iko mezani inajadiliwa tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuweza kutujumuisha katika dira hii. Dira inaelekeza kuwa na Taifa jumuishi lenye ustawi haki na linalojitegemea. Nitajikita katika mambo mawili; uchumi imara jumuishi na shindani, lakini pia maisha bora na ustawi kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutujali sana sisi watu wenye ulemavu, si tu kutujali yaani anaonyesha utu na sisi wote ni mashahidi. Nikianza kwenye masuala ya afya, watoto chini ya miaka mitano. Ukienda kwenye field ya kawaida watoto wanatibiwa bure chini ya miaka mitano. Hata hivyo, ninaiomba Wizara, kuna watoto wa usonji na watoto wenye vichwa vikubwa, hawa watoto wasiishie tu miaka mitano waendelee kupata huduma mpaka pale watakapokaa sawa, nina imani hili liko ndani ya uwezo wa Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna ulemavu wa afya ya akili, hawa watu wanahitaji dawa maisha yao yote, ninaomba zitolewe bure ili kujenga jamii jumuishi kama dira inavyotuelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sisi watu wenye ulemavu kuendelea kuwa chini ya Waziri Mkuu, inamaanisha mambo yetu wenye ulemavu ni mambo mtambuka yana-cut across kwenye kila Wizara. Kwa hiyo, Waziri Mkuu ana uwezo wa kutoa maelekezo katika Wizara tofauti tofauti ili kuleta maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii Awamu ya Sita tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kitendo cha kuboresha vyuo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu na hii ni namna ya kupambana na ajira kwa vijana wenye ulemavu. Ninaomba nivitaje hivi vyuo viko 10 vingine vimekarabatiwa na kutengenezwa, vingine vimejengwa upya chini ya Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu ambao uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo hivyo ninaomba nivitaje wananchi wavielewe ili waweze kuwapeleka vijana wao kwa ajili ya maendeleo ya vijana, kuzalisha ajira na vijana pia watajiajiri. Vyuo hivyo kuna Chuo cha Rwanzari, mkoani Tabora; Chuo kiko Milongo, Mwanza; Chuo cha Masiwani, Tanga na Mtapika, Masasi, Mtwara. Chuo cha Ufundi, hivi vya watu wenye ulemavu Sabasaba, Singida; Yombo, Dar es Salaam; Ruvuma; Mbozi, Songwe; Kasulu, Kigoma; na Kisesa, Mwanza. Hivi vyuo ni vya watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara ya Elimu hili suala lichukuliwe kama emergence, kuna Chuo mfano kile cha Rwanzari havina mkalimani wa lugha ya alama ambapo wanafunzi wenye uziwi wanakosa mawasiliano kati ya mwalimu na mwanafunzi. Kwa hiyo, ninaomba tuangalie namna ya kupeleka wakalimani, hiyo Rwanzali nimetolea tu mfano kwa sababu nimekitembelea, lakini sijajua hivi vyuo vingine pia Wizara wanaweza wakachukua muda kuvitembelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye Wizara ya Uchukuzi sisi watu wenye ulemavu ninaomba tuondoe mentality kwamba tunapenda kusaidiwa, hapana. Sisi tuondolewe vikwazo ili tuweze kupambana katika maendeleo, kwa sababu kuwa mwenye ulemavu hakuniondolei kwamba nitakuwa na nchi yangu peke yangu, hapana. Huduma wanazozipata watu wengine na sisi tunaenda huko huko. Kama kwenye mabasi tunapanda na sisi tunapanda huko huko, hakuna jamii nyingine. Mfano, kuna usumbufu unaojitokeza kwa sisi watu wenye ulemavu kwenye Wizara ya Uchukuzi hasa SGR, vituo vya mwendo kasi, uwanja wa ndege na stendi za mabasi mfano pale kwa Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka kusema kwamba na sisi ni wapambanaji tunachangia pato la Taifa, lakini kuna usumbufu ambao hauna hata, yaani usumbufu siyo wa lazima. Tumewekewa viti mwendo vile tumewekewa mazingira mazuri sawa mfano, pale kwenye SGR, lakini vile vitimwendo mimi mwenyewe ni shahidi unakaa pale nusu saa nzima saa nyingine unaletewa kitimwendo na vitimwendo vingi vimeharibika inamaanisha havifanyiwi service. Tunapotezewa muda katika hivi vituo. Huu ni usumbufu usio wa lazima. Ninaomba tusaidiwe kwa sababu tunapoteza muda mwingi na tunashindwa kuchangia maendeleo kama watu wengine. Tunapenda tufike kwa wakati twende katika maeneo yetu kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wenye ulemavu tunahudumiwa na ustawi wa jamii kwa ngazi ya halmashauri na hiki kitengo cha ustawi wa jamii kinahudumia si watu wenye ulemavu tu, wanahudumia wazee, watoto wa mitaani, kutatua migogoro ya ndoa, yaani mambo mengi hii Wizara imeyabeba; inapitia changamoto nyingi. Sisi wenye ulemavu changamoto zetu wao ndiyo wanazifahamu. Hawa ndiyo wanaofahamu idadi ya wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kata mpaka kwenye wilaya mpaka mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba na kuishauri Wizara kama itapendeza iongeze idadi ya Maafisa Ustawi wa Jamii. Wawepo angalau kila kata, kwa sababu sasa hivi kazi ya ustawi wa jamii kwenye kata wanafanya pia Maafisa Maendeleo ya Jamii. Pia, ianzishwe Idara ya Ustawi wa Jamii kwenye kila Halmashauri. Kwa sasa muundo wa halmashauri hii ustawi wa jamii ni kitengo kiko chini ya Mganga Mkuu Wizara ya Afya kwenye ngazi ya halmashauri. Ndiyo maana tunakutana na changamoto utakuta vifaa saidizi hatuna, mafuta ya wenye ualbino hayatoshi kwa sababu hawana bajeti maalum ambayo inayowawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba iwe idara katika ngazi ya halmashauri na ngazi ya mkoa. Itasaidia sana kutatua changamoto zetu wenye ulemavu na hii kama ikishindikana basi wazo la pili ni kwamba bajeti ya ustawi wa jamii kwa upande wa watu wenye ulemavu basi ipelekwe kwenye Wizara inayohusu watu wenye ulemavu ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Wenye Ulemavu ili mambo yetu yaweze kutatulika kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninahitimisha kwa kusema kwamba ukimpa mtu chakula kila siku. Leo umempa chakula na kesho unampa chakula, huyu unamtengeneza awe tegemezi maisha yake yote. Tukumbuke sisi watu wenye ulemavu kwenye sensa ya hivi karibuni tuko zaidi ya milioni tano ni sawa na 11.2% ya Watanzania wote. Kwa hiyo, tuangalie tusipoweka mikakati madhubuti ya kuondoa vikwazo kwa hili kundi la watu wenye ulemavu tunatengeneza Taifa kubwa ambalo ni tegemezi na tunavyoangalia kwamba dira yetu inasema tutengeneze jamii jumuishi na yenye kujitegemea. Kwa hiyo, ndugu zangu, Wizara hizi ziwasiliane juu ya namna ya kuondoa vikwazo ili tusitengeneze Taifa tegemezi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninaomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote ninapenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutufikisha kuwa wazima mpaka dakika hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia shukrani za pekee zimwendee Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutujumuisha katika kila sekta watu wenye ulemavu Nchini Tanzania. Pia shukrani zingine zimwendee Waziri Mkuu ambaye kwa sisi wenye ulemavu kuwa chini yake na kuendelea kuratibu mambo yetu ya wenye ulemavu. Kwa kuthibitisha hili hata kwenye hotuba yake amezungumza kuwa yeye ni mdau mkubwa wa watu wenye ulemavu, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja kwa kuokoa muda mchango wangu utajikita katika ukurasa wa 71 na 72 ambao ni uratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu. Hotuba ya Waziri Mkuu ilieleza kwamba Serikali imewezesha bohari ya dawa kuzalisha na kusambaza vifaa saidizi na mafuta kinga kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ninaweza nikatolea mfano, ni sawasawa na samaki na maji huwezi kuvitenganisha. Ukimweka samaki nchi kavu atatapatapa mwisho wa siku mambo yataharibika, hivyo hivyo hata sisi watu wenye ulemavu. Nimefika hapa kwa sababu tu nina vifaa saidizi vimeniwezesha kuingia humu na kutekeleza majukumu yangu ya kiubunge kama Wabunge wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kuwa vifaa hivi vimekuwa ni gharama na wote tunafahamu watu wenye ulemavu hali zetu wanazifahamu, ni duni. Nitolee mfano, mguu bandia kwa aliyekatikia juu ya goti miwili nitolee mfano moja kwa moja kwenye hospitali yetu ya Muhimbili pale Moi, wanauza unapata invoice ya milioni saba miguu miwili. Sasa niambie mtu mwenye ulemavu wa kawaida hiyo gharama anaipata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, vifaa saidizi tukimaanisha hata magongo na crutches kama hizi ninazotembelea mimi nazo ni gharama kwa mtu mwenye ulemavu. Ninamzungumzia mwenye ulemavu wa hali ya kawaida kule kijijini, kwenye kata na kwenye Wilaya kule ambapo anapatikana, hizi gharama anazipata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Waziri Mkuu, Serikali imewezesha KCMC kuzalisha mafuta kinga kwa watu wenye Ualbino, wako wadau mbalimbali ambao wanazalisha vifaa saidizi maana vimekuwa adimu ndiyo maana hata gharama zinakuwa kubwa, wawezeshe hizi hospitali kila Mkoa pawepo basi hata hospitali ambayo inatoa vifaa saidizi na ili kurahisisha maisha kwa watu wenye ulemavu, vinginevyo hali zetu zinakuwa ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ninazungumzia suala la mikopo ya 10%, kwa wenye ulemavu tunapata asilimia mbili. Imezungumzwa sana na wenzangu wazungumzaji waliotangulia. Sisi watu wenye ulemavu nchini Tanzania; kuna aina 13 za watu wenye ulemavu. Kuna aina moja ya ulemavu ambayo ni ya ulemavu wa akili, hawana sifa ya kupata huu mkopo, lakini ikumbukwe kwamba kuwa na ulemavu maisha yanaendelea kama kawaida. Atahitaji kula, atafanya biashara; na tukumbuke kwamba kuna dawa ambazo wanatumia, akitumia anakuwa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali imewatoa kabisa kwamba hawa watu hawapati hii mikopo. Ikumbukwe kwamba sisi wenye ulemavu hatuishi peke yetu, tunaishi na ndugu zetu, either ni mama, ni baba, ni mume, mke, tunaishi nao. Serikali inaweza ikaja na mpango mwingine wa kuwafikiria hawa walemavu wa akili ili nao waingie kwenye kuwapatia mikopo hii ya asilimia mbili ili nao waweze kufaidika na keki hii ya Taifa, ambayo wenye ulemavu wengine wanaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikishindikana hilo, ushauri mwingine basi wafikiriwe wapewe ruzuku, ilimradi tu kurahisisha maisha yao, waendelee kuishi kama watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba pia ya Mheshimiwa Waziri amezungumza kabisa kwamba Serikali imewezesha kituo atamizi kilichopo Singida pale Sabasaba. Chuo hiki ni miongoni mwa vyuo vingi ambavyo Serikali imeviboresha. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ataona inafaa aweze kuvitembelea vyuo hivi, vina changamoto, ikiwemo wakalimani wa lugha ya alama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri Chuo cha Luanzali Mkoani Tabora, hakina mkalimani. Hata juzi likizo nimetoka huko nimeona bado mkalimani hayupo. Hawa wanafunzi wanasomaje bila mkalimani? Ninaomba hili lichukuliwe kwa uzito ili kusaidia; na tutashukuru kama watatembelea na kutatua changamoto nyingi ambazo zinahusiana na hivyo vyuo vyuo vya watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nizungumzie watumishi wenye wa umma ulemavu. Kuna mwongozo upo, mwongozo wa watu wenye ulemavu mahali pa kazi. Mwongozo huu hautambuliki kwa waajiriwa. Ninaomba Serikali, Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora waweze kuwatambulisha waajiri wote huu mwongozo ili wafanyakazi wenye ulemavu waweze kupata haki zao kutokana na mwongozo, ambao Serikali ilikaa na kufikiria na kuona kutengeneza huu mwongozo na si kuuweka tu kapuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, kupitia Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tunaomba waajiri wasiwanyime wafanyakazi wenye ulemavu fursa za safari za kazi kwa sababu ya mitazamo chanya ambayo wanayo kichwani mwao. Sisi watu wenye ulemavu tunafanya kazi na sisi tunatamani tupate hiyo fursa ya kusafiri ili tuweze kupata hicho kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna waraka wa per diem kwa mwanamke ambaye ananyonyesha, akisafiri kikazi analipwa nusu per diem kwa ajili ya kumsaidia mtoto anayesafiri naye kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, sisi watu wenye ulemavu, mimi mwenyewe siwezi kutembea peke yangu, ninahitaji msaidizi. Wafanyakazi wengi wa watu wenye ulemavu wanapokwenda safari za kikazi wanapewa fedha iliyo sawa na mtu mwingine. Kwa hiyo, yeye atamchukua mtu wa nyumbani amsaidie kwenda naye. Atamkatia ile ile per diem ambayo ndiyo anayopata; of which inakuwa sasa hela anayoipata ni kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ofisi ifikirie kutengeneza basi na waraka mwingine kwa watu wenye ulemavu, watambulike kuwa na msaidizi mahali pa kazi na hasa wakisafiri kwenye kuelekea kwenye safari za kikazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Ofisi ya Waziri Mkuu inaandaa maazimisho ya siku ya Kimataifa na pia sisi watu wenye ulemavu tuna siku yetu maarufu kama D Day (Disability Day) ambayo ni tarehe 3 mwezi Desemba. Siku hii imekuwa ikidorora siku hadi siku. Mfano mzuri, mwaka jana tulifanyia Morogoro, ikawa kama ni kikao tu cha walemavu kutoka kata fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Ofisi ya Waziri Mkuu waendelee kuratibu hii Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani kama siku nyingine za kimataifa za UKIMWI na maadhimisho mengine. Waichukulie kwa uzito na sisi tutafurahi; maana siku hiyo ndiyo siku ambayo wadau wanaweza kutoa mambo yao na pia tunaweza tukawajua wadau wanaojishughulisha na mambo yetu. Sisi wenyewe pia tutajulishana mambo mengi ambayo yanatuhusu sisi watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo ninaunga mkono hoja, ninashukuru kwa kunipa fursa. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa. Kwa kuokoa muda ninaomba nijielekeze mchango wangu katika mambo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nitagusia Tume ya Utumishi wa Umma na Watu Wenye Ulemavu; mwaka wa fedha 2025/2026, Tume ilipangiwa fedha takribani milioni 500 na fedha hizi mpaka kufikia Februari mwaka huu 2026, Tume hii haikupokea hizi pesa. Hizi pesa ziliwekwa kwa ajili ya ujenzi wa mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia rufaa za watumishi wa umma na malalamiko yanayotolewa na watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yameongelewa mengi kwa watangulizi waliotangulia, watumishi wa umma wako kila sehemu na endapo mfumo huu utaanzishwa na kufungwa utawezesha watumishi kufikia rufaa na malalamiko yao moja kwa moja kwenye Tume na siyo kupitia kwa mwajiri ambavyo ilivyo sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba hizi ofisi ziko kikanda na hazipatikani moja kwa moja kwenye kila halmashauri. Kwa hiyo, huyu mtumishi anapotaka kukata rufaa kwa malalamiko yake kupitia huu mfumo endapo ungefungwa, basi huyu mtumishi kwanza tutampa uhakika wa suala lake la malalamiko la kiutumishi, kwamba limefika sehemu sahihi kwa sababu atajaza kwenye mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi ambaye yuko kijijini kule au yuko mbali, kumfikishia mwajiri lalamiko lake kwa kweli wakati huo tukumbuke kwamba hawaelewani, kuna sintofahamu kati yao, kwa hiyo kila mtu anajiona kwake ni bora kuliko mwenzake. Kwa hiyo, ukiwepo huu mfumo ninashauri Serikali hii pesa itolewe ili huu mfumo uweze kuwekwa kwa ajili ya manufaa ya watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze pia kwa watu wenye ulemavu. Kwa mujibu wa sheria ya watu wenye ulemavu Na.9 ya 2010, Kifungu cha 27, kinamtaka mwajiri aliyeajiri watu kuanzia 20 ahakikishe kuwa asilimia tatu ya wafanyakazi wake ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili kiukweli, kwanza tunaipongeza Wizara kwa kuendelea kupambania watu wenye ulemavu kuingia katika ajira, lakini tunaomba iweze kuboresha kidogo. Kwa sababu ukiangalia hii sheria na idadi ya watu wenye ulemavu ambao wanamaliza chuo ni wachache sana, ilitakiwa hata mtaani kusiwepo na watu wenye ulemavu ambao wanahangaikia ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwona mtu mwenye ulemavu amemaliza degree yake anatafuta kazi, kwanza tu kufikia ile elimu ni kwamba amepambana vya kutosha mpaka kufikia pale, tukumbuke kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa watu wenye ulemavu kwa kweli anapenda kutupa kipaumbele. Si tu hivyo tu ni kwa sababu ya mazingira mbalimbali ambayo tunayapitia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kuwa Sekretarieti na Wizara husika, tunaamini Waziri Ridhiwani na Naibu Waziri wake wanafanya kazi nzuri sana na hicho kitu hakikwepeki, wanamsaidia vizuri Rais, lakini katika hili tunaomba mwendelee kutupa kipaumbele, watu wenye ulemavu wako mtaani, kwa hiyo watafaidika nao angalau wapate elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru pia hii Wizara kwa sisi watu wenye ulemavu kwenye mfumo wa HCMS pale kwenye dashboard kwa kweli Wizara hii imetutambua. Kwamba Afisa Utumishi anaposhughulikia file labda la mtumishi Nyamizi anajua kabisa Nyamizi pale imeonyesha ni mwenye ulemavu. Kwa hiyo, tunashukuru kwa kututambua hivyo, pia ninaomba mambo yetu, masuala yetu, utawala bora uende pia kwa ajili ya kurahisisha na mambo yetu, kurahisisha angalau kupunguza makali ya maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka pia kwenye suala la Pay as You Earn kwa watu wenye ulemavu nilikuwa ninaomba Wizara kwa huko nyuma, ninakumbuka kuna Rais ninadhani alipunguza Pay as You Earn, ninaomba kwa nini tunataka tupunguziwe Pay as You Earn au saa nyingine kuweka zero kabisa, kwa sababu kuna gharama ambazo ukiwa tu mwenye ulemavu unaingia utake usitake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka tunatumia vifaa saidizi vinahitaji ukarabati wa mara kwa mara, umetumia mguu bandia mara nyayo imegeuka unarudi hospitali, kwa hiyo kuna zile hela ambazo zinaingia tu kwa sababu tu ya ulemavu, hii inazungumzia kwa mtumishi mwenye ulemavu. Kwa hiyo, Serikali tufikirie kwamba hawa watu tuwapunguzie hii Pay as You Earn au kuiondoa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili litakuwa si la kwanza kwa Tanzania hata kwenye nchi za jirani ambazo sisi ni wanachama pia kwenye SADC na East African Community, mfano mzuri Kenya. Kenya katika hili suala la watumishi kwenye kodi hii Pay as You Earn wameondoa wameweka zero kabisa hawalipi. Kwa hiyo, nina imani Serikali yetu ni sikivu na itasikia, Waziri yuko pale na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani hili suala litaenda vizuri kwa sababu tu kuna gharama ndugu zangu, kwa sababu tu ya muda ninashindwa kueleza zaidi, ukiwa mwenye ulemavu kuna gharama kubwa unaingia, hata kufika pale kazini, yule mwenye ulemavu anatumia gharama kubwa kufika ofisini, tofauti na mfanyakazi ambaye hana ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Wizara pia inaweza ikatufikiria watu wenye ulemavu kwenye kuongeza muda wa kustaafu. Kuna mamlaka ambayo ninajua wameongezewa kwa sababu zao wanazifahamu. Kwa upande wetu sisi ninarudia pale pale kwamba ukiwa mwenye ulemavu, nimeanza kusoma darasa la kwanza. Mfano, mwenye ulemavu ambaye anazaliwa nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mbalimbali mfano mtu asiyeona, analazimika aeleweshe nukta nundu kabla ya kuendelea na masomo mengine. Kwa hiyo, inamaanisha anatumia muda mwingine, ataelewa ile herufi, lakini bado masuala ya nukta nundu hataelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viziwi na wenyewe pia lugha ya alama, watoto wale wanafundishwa kujua ile lugha ya alama. Kwa hiyo najikuta nakuja kumaliza chuo nina miaka 30 mpaka 35, lakini asiye na ule mlemavu amemaliza chuo na miaka labda 20 mpaka 25 kwa hiyo, naona hapo utofauti, tunachoangalia hapo ni uwiano tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiongezewa muda wa kustaafu watu wenye ulemavu tutashukuru sana kwa ajili ya ku-cover ule muda ambao tumepoteza kwa ajili ya ulemavu, tumehangaika kwa ajili tu ya kuhangaikia masuala ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana kwa kunisikiliza. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara hii ya Katiba na Sheria. Kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi sote hapa kwa uzima na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninapenda kuipongeza Wizara, kiukweli inafanya kazi nzuri sana. Tumesikiliza taarifa yake hata taarifa ya Kamati pia inafanya kazi nzuri sana. Mfano mzuri ninampongeza Waziri kwa kuanzisha siku maalum ya sema na Mheshimiwa Waziri; kwa hiyo, ile ni nafasi ya pekee ambayo wananchi wanaitumia kwa ajili ya kueleza kero zao zinazohusiana na sheria. Kwa hiyo, ninawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuweka huduma ya uwakili kwa makundi maalum ikiwemo watu wenye ulemavu. Kwa kweli watu hawa, watu maalum, mfano wenye ulemavu unakuta hawana pesa ya kumlipa wakili au unakuta mwananchi wa kawaida hana uwezo wa kumlipa wakili, lakini Wizara imetoa hiyo huduma bure kwa haya makundi. Kwa hiyo, ninaipongeza sana Wizara sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pamoja na pongezi hizo kuna ambao wamesema kwamba Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, Fungu la 101 kwamba taarifa inaonyesha walitafsiri sheria mbalimbali kutoka lugha ya Kiingereza kuja ya Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sijasikia kwamba walitafsiri lugha ya watu wenye ulemavu, mfano, nukta nundu kwa wasioona kwa sababu wako wanasheria wengi sana wasioona, nadhani tunashuhudia kwamba wako mawakili pia wasioona. Sasa tusipotafsiri lugha hii kwenye nukta nundu kwa kujali haya makundi inaweza ikawa siyo ujumuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina imani kwa kupitia hii ninadhani wanaweza wakaboresha zaidi katika hilo kama hizo nukta nundu hazipo. Pia katika hili nina imani niko sehemu sahihi kulizungumzia, Tanzania iliridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu iliridhia mwaka 2009 na ilipaswa ku-submit ripoti ile initial report kwa sababu na sisi Tanzania ni wanachama. Kwa hiyo, ile initial report ilitakiwa ikabidhiwe baada ya miaka miwili na baada ya hapo inatakiwa ku-submit progress report kila baada ya miaka minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi naona process haifiki mwisho. Kwa lugha nyingine hata ukiangalia kwenye ile link hakuna ripoti ya Tanzania kuhusiana na masuala ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo pia yako mambo mengi mno ambayo nchi kama nchi imefanya kwa watu wenye ulemavu. Sifikirii kwamba hakuna kabisa, hapana! Maendeleo ni hatua, huwezi ukafananisha watu wenye ulemavu wa sasa hivi na wa miaka ile 2000 au miaka ya nyuma, kuna maendeleo hasa ukizingatia kwa Mheshimiwa Rais huyu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, amefanya mambo mengi sana; ukiangalia kwenye sekta ya elimu, ukiangalia kwenye afya, lakini bado kwenye uwekezaji kwenye dira tumejumuishwa mambo mengi sana matamu mazuri ya kuripoti kama nchi kwa masuala ya watu wenye ulemavu. Mpaka sasa tunaonekana hii Nchi ya Tanzania haifanyi chochote kuhusiana na mambo ya watu wenye ulemavu, lakini si kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana tuangalie namna ya kuripoti, kwa sababu tunavyozungumza sasa hivi hiyo USRPD ilitakiwa turipoti taarifa nne ukijumisha na ile initial report na tunakoelekea sasa hivi USRPD hiyo imeshaboreshwa tuko kwenye ADP ambayo na yenyewe tunatarajia Serikali iweze kuridhia kwa ajili ya kutekeleza mambo ya watu wenye ulemavu kwa muktadha wa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana ile USRPD ilikuwa kwa Kimataifa haiendani na mazingira ya Tanzania au ya Afrika. Kwa hiyo, wamekaa wameona hapana tutengeneze hii mkataba mwingine ambao ni itifaki ADP kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwa muktadha wa mazingira yetu kama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Serikali pale inapokwama sijui inakwamia wapi kwa nini isiripoti mambo mazuri mazuri, matamu ya watu wenye ulemavu na sisi tunajivunia na siyo tu sisi Serikali hata wadau wanazitumia hizi ripoti, wadau NGOs, CBOs na wadau wengi wanaojishughulisha na masuala ya watu wenye ulemavu, wanatamani nchi kama nchi itoe ripoti ambayo na wao itawasaidia katika mambo yao na activity zao za kuwaendeleza watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo pia kuna Tume ya Kurekebisha Sheria, Marekebisho ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.9 ya 2010 iko haiendani na mazingira ya sasa hivi: mazingira ya sasa hivi mfano kama sasa hivi yako ujasiriamali, wako TEHAMA yaani mambo mengi ambayo yameendelea kwenye ile sheria na ile sheria tunahitaji iboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema kwamba wamerekebisha sheria mbalimbali; tulikuwa tunaomba pia kama haipo Sheria ya Watu Wenye Ulemavu na ni kweli haipo ninaomba pia iweze kurekebishwa. Tunaomba Wizara watusaidie tuweze kurekebisha ili mambo yetu na sisi yaende vizuri yaendane na kasi ambayo ipo ya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo pia tunaishukuru Tume, ukisoma Ibara ya 12, 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; inasema hakuna aliye juu ya sheria. Kwa hiyo, hata hili suala linaenda moja kwa moja kwa Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wenye ulemavu siyo kwamba hatutendi makosa, wapo wanaotenda makosa na wanaadhibiwa kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria, yapo magereza je, yale magereza ni rafiki kwa watu wenye ulemavu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wawaangalie, lakini pia kuna sheria ambazo zipo zinafanyika kule magereza; ukiangalia mimi ninatumia vifaa saidizi: vifaa saidizi ni chuma na ukiangalia sheria za kule zinaweza zikanizuia nisiingie na gongo au kifasaidizi changu. Matokeo yake mwisho wa siku inakuwa inatweza utu wa watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeongea kwa mjumuisho katika hilo suala na nina imani Serikali yetu ni sikivu, nina imani Wizara wanafanya kazi vizuri sana, nina imani kabisa kwa sababu kama alikuwa hamjui basi wanajua kwa ajili ya kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kupongeza sana Wizara kwa mambo makubwa ambayo wanaendelea kuyafanya kama Wizara sisi watu wenye ulemavu tunawapongeza sana, tuna imani na wao, tuna imani na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amewapa hii kazi wasaidie katika kazi hii ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani mambo yetu ya watu wenye ulemavu hayatakwama badala yake yatasonga mbele hatua kwa hatua, maendeleo ni hatua. Tuna imani sasa hivi na tunakoelekea tulikotoka ni tofauti na kila kitu; sheria ndiyo msingi wa kila kitu. Kwa hiyo, tusipoangalia sheria tukaziweka vizuri na sisi watu wenye ulemavu tutakuwa hatujajumuishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani kabisa sheria zikikaa vizuri, sheria zikieleza vizuri watushirikishe pale ambapo wanaona hapa tunahitaji mawazo mengine, sisi tupo ambao ni wataalam, tumebobea na masuala haya ya watu wenye ulemavu kama Waheshimiwa Wabunge tutasongesha mbele mambo ya watu wenye ulemavu hasa katika sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante kwa mchango wako.

MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi