MHE. OMARY M. MSIGWA aliuliza: -
Je, lini Serikali italeta fedha katika Jimbo la Madaba ili kutatua changamoto ya maji katika Vijiji vya Gumbiro, Ngadinda na Lilondo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Marcus Msigwa, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Gumbiro, Ngadinda na Lilondo vilivyopo Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma. Miradi hiyo kwa pamoja inagharimu jumla ya shilingi bilioni 2.451 ambapo inahusisha ujenzi wa vyanzo vya maji vitatu; ujenzi wa matanki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita 325,000, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 62.9, sanjari na ujenzi wa vituo 28 vya kuchotea maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2025/2026 na kunufaisha zaidi wananchi 12,570 waishio katika Vijiji vya Gumbiro, Ngadinda na Lilondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, hadi kufikia Mwezi Machi, 2026, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 1.536 katika utekelezaji wa miradi hiyo na itaendelea kupeleka fedha kadiri zinavyopatikana ili iweze kukamilika na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.
MHE. OMARY M. MSIGWA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaongeza Watumishi wa Sekta ya Afya wakiwemo Wataalamu wa Mionzi katika Jimbo la Madaba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Marcus Msigwa, Mbunge wa Jimbo la Madaba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga bajeti na kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya nchini. Katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2025/2026 jumla ya watumishi wa kada mbalimbali za afya 37,921 wameajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2025/2026 Serikali imeajiri jumla ya wataalam wa kada mbalimbali za afya 5,000 na kuwapanga katika halmashauri zenye upungufu ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba iliyopangiwa watumishi 84.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu na huduma katika vituo vya afya ngazi ya msingi hali iliyopelekea mahitaji ya wataalam wa kada za afya ikiwemo wataalam wa mionzi kuongezeka ambapo wanaohitajika ni 1,159 na kwa sasa wapo 338 sawa na 29%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri wataalam wa mionzi pamoja na kuwaendeleza wataalam wa kada nyingine 56 wakiwemo watumishi wawili kutoka Halmashauri ya Madaba wanaopata mafunzo ya muda mfupi ya mionzi katika Chuo cha Afya Hydom.