Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rashid Habib Ali (1 total)

MHE. RASHID HABIB ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Said Ali Mbarouk, ninaomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, taasisi nyingine za ulinzi na usalama hazikuwekwa katika mfumo huu. Je, ni vigezo gani vilivyotumika kuwekwa Jeshi la Polisi katika mfumo huo wa kikokotoo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili. Je, Serikali haioni haja sasa, kwa sababu ya malalamiko ya muda mrefu ya mfumo huu, kuwaondolea Jeshi la Polisi mfumo wa kikokotoo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Nampongeza Mheshimiwa Rashid, kwa niaba ya kuuliza swali hili, juu ya masuala ya kikokotoo kuhusu ni kwa nini, Jeshi la Polisi limeingia katika kundi hili, lisiwe kama taasisi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza niweke sawa; siyo Jeshi la Polisi pekee katika taasisi hizi za ulinzi na usalama ambazo zinahusika katika ulipaji wa mafao kwa njia hii. Pia, kuna taasisi kama Jeshi la Magereza na nyingine kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge si kwamba, Jeshi la Polisi kuwepo katika mfumo huu wanabaguliwa, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya jitihada kubwa kuhakikisha mifuko hii inazidi kuimarika. Mwaka 2018 mifuko hii iliunganishwa kwa sababu moja tu, ilikuwa haipo himilivu katika kulipa mafao. Katika kipindi hicho, kwa Mfuko wetu wa PSSF, kulikuwa na deni maarufu la pre-1999, la zaidi ya shilingi trilioni 4.6. Mpaka ninavyozungumza sasa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelipa deni la shilingi trilioni 4.2 na kiasi kilichobaki kipo katika uhakiki, ndani ya muda mfupi deni hilo lote la shilingi 4.6 litakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mfuko wetu wa NSSF pia, nako Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amelipa shilingi 4,483,000,000,000. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuimarisha uhimilivu wa mifuko hii kulipa mafao; kufuatia hivyo, mifuko hii imeweza kulipa. Kwa mfano, PSSF tuna kauli inayosema, “tunalipa kama jana”; mstaafu, anapostaafu leo, anaenda nyumbani jana, mafao yake yanakuwa yamelipwa. Nakuhakikishia kwa kadiri tunavyoendelea kuimarisha uhimilivu wa mifuko hii, hata mafao au kikokotoo kitaboreshwa kwa watumishi wote wa sekta binafsi na umma. (Makofi)