Supplementary Questions from Hon. Rebeca Sanga Nsemwa (3 total)
MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuiwezesha timu ya Taifa ya Mpira wa Pete, kwani timu hii imekuwa ikifanya vibaya sana katika mashindano ya Kimataifa, lakini pia imekuwa ikienda kushiriki katika mashindano haya ikiwa haijakaa kambi, wala haina jezi zenye nembo ya bendera yetu ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rebeca kwa swali zuri. Serikali imekuwa ikiigharamia mara kwa mara Timu ya Mpira wa Pete, na kama anavyosema, hatujawahi kuwa na matokeo mazuri sana katika miaka ya karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunaendelea na juhudi mbalimbali za kuiwezesha timu hii, na kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha tunahakikisha ya kwamba timu hii inakaa kambi na kuwa na vifaa vya kutosha na inaweza kusafiri na kuweza kuhudhuria mashindano mbalimbali kwa ajili ya kuiwakilisha nchi yetu. Bado tunafanya juhudi nyingi kuhakikisha uwezo na ubora wa timu hiyo unaimarika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutaendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Pete ili kuhakikisha tunaimarisha timu hii.
MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa, hali ya barabara hiyo kwa sasa ni mbaya sana kutokana na mvua nyingi zilizonyesha, je, ni nini kauli ya Serikali ya kufanya matengenezo ya dharura kwa barabara hiyo, ili wananchi wa Wilaya ya Makete waendelee na shughuli zao za kiuchumi, ukizingatia hao ni wakulima hodari na wafanyabiashara maarufu nchini Tanzania?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mkandarasi anayejenga Barabara ya Matamba Mjini kilometa moja na meta 800, ameondoka site muda mrefu, licha ya kuwa amelipwa fedha zake. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa mkandarasi huyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo ilipo barabara hii ni la miinuko na lina mvua nyingi. Barabara hii ndiyo kwanza imepanda hadhi kuja TANROADS. Kwa hiyo, tunachofanya, kwanza, ni kuhakikisha kwamba tunaitoa katika hali iliyokuwa na kuileta kwenye viwango vya TANROADS. Ndiyo maana tumeamua kwanza kukarabati na kutengeneza yale maeneo korofi ili iweze kupitika, lakini mpango ukiwa ni kuitengeneza barabara yote.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge na ninatoa maelekezo hapa kwa Meneja wa TANROADS kwamba, mvua imepungua sana katika maeneo hayo, aweze sasa kuitembelea hiyo barabara ili yale maeneo yote ambayo yanafanya wananchi wasiweze kupita kwenye hiyo barabara, basi aweze kuyatengeneza kwa sababu, mkandarasi ambaye amepangiwa hiyo kazi, yupo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Barabara ya Matamba – Mjini; kwa kuwa, mkandarasi amelipwa na nina hakika mvua imepungua, Meneja wa Mkoa wa Njombe ahakikishe kwamba, mkandarasi anarudi na kukamilisha hiyo kazi ambayo amepewa na Serikali, ahsante.
MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, wananchi wa Wilaya ya Makete ni wazalishaji wakubwa wa zao la ngano. Licha ya zao hilo kutumika kutengeneza vitafunwa mbalimbali kama mikate, maandazi na chapati, lakini zao hili katika Wilaya ya Makete hutumika pia kupikia ugali ambao ni chakula kikuu kwa wananchi wengi wa Tanzania.
Je, ni lini Serikali itaweza kuwatafutia masoko wananchi hawa ili zao hili liuzwe kwa bei ambayo itaweza kuwanufaisha wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimthibitishie tu dada yangu Mheshimiwa Rebeca Nsemwa kwamba soko la ngano nchini, ndiyo ninaweza nikasema ni soko la uhakika kwa sababu ngano tunaagiza, ninaweza nikasema karibu 100% kutoka nje ya nchi. Pia tunatumia fedha nyingi sana kwa mwaka, zaidi ya shilingi bilioni 400 kuagiza ngano kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ni soko la uhakika na moja ya mkakati wa Wizara (Serikali), ni kuhakikisha zao la ngano ndiyo linapewa kipaumbele. Katika hizo jitihada tunazofanya ni pamoja na Halmashauri ya Makete, Mbunge wa Jimbo hapa anafahamu, kila mwaka tumekuwa tukipeleka mbegu za ruzuku bure ili kuli-boost hilo zao. Tunaamini tukishaongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa, maana yake itatusaidia kupunguza ile tunasema gap ya uagizaji wa ngano kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, soko letu hapa nchini ni la uhakika na tutaingia katika kilimo cha mkataba ili kuhakikisha wale wananchi wanapokuwa wanalima, wanauza moja kwa moja kwa wadau, ahsante.