Contributions by Hon. Patali Shida Patali (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishukuru kwa nafasi hii uliyonipa. Mchango wangu kimsingi ninaomba ujikite kwenye maeneo, hasa eneo kubwa la mbolea. Ninaomba nifikishe salamu za Wanambeya Vijijini kwa kuwasemea maeneo mawili kwa haraka. Kwanza ni kuhusu pareto. Mbeya Vijijini ni moja ya wilaya ambayo inaongoza kwa kilimo cha pareto nchini, kwa mujibu wa taarifa za Bodi ya Pareto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya kuboresha biashara ya zao hili. Hivi karibuni na kwa kupitia Taarifa iliyowasilishwa, kuna mpango wa ujenzi wa haya makaushio 150 na sisi Mbeya vijijini tunayo 40. Tuiombe Serikali ituharakishie ujenzi huu wa haya makaushio kwa ajili ya kuboresha hili zao la pareto Mbeya Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie bei; moja ya changamoto kubwa kwenye zao hili la pareto ni kuwa na vishoka wengi ambao wanadidimiza jitihada za makusudi za wakulima. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Chongolo wawaangazie macho hawa vishoka ambao wanaingilia kati kwenye hizi bei za hili zao la pareto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie mazao. Jimbo la Mbeya Vijijini tunazalisha zaidi ya tani laki sita za mazao ya chakula lakini mahitaji yetu ni takribani tani laki moja na tisini hadi laki mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika Bunge hili, tusipoliangalia vyema hili suala la masoko nchini, tunaenda kuzalisha mazao mengi na tukakosa masoko kwa kwenda kuyauza. Cha kwanza, ninaomba nisisitize kuboresha masoko ya ndani, ikiwa ni pamoja na kujenga masoko kwenye kila wilaya ambazo zinaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukawaza hizi tani 400,000 sisi Mbeya Vijijini ambazo tunazalisha ziada ya chakula dhidi ya mahitaji yetu tutazipeleka wapi endapo hatutaboresha au kuchukua hatua za makusudi kujenga masoko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ninatamani kujikita ni suala la mbolea; na hapa ninaomba nichangie haraka haraka kwa sababu ya muda mfupi. Nchi yetu hii inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 tutakuwa na takribani ya wastani ya watu wasiopungua milioni 77.55. Watu hawa wote wanahitaji ardhi kwa ajili ya kilimo ili kuelekea ule uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 kama Dira yetu ya Taifa inavyoeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kilimo chetu kiwe na tija ni lazima tuangalie uwezekano na kuchukua jitihada za makusudi katika kuimarisha upatikanaji wa mbolea nchini. Hali ilivyo sasa, tunapata mbolea ya ruzuku na hapa ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais; lakini bado kuna changamoto ya kuchelewesha mbolea na pia kuingiliwa na walanguzi wanaoficha mbolea. Wakati mwingine zinaadimika sokoni na kuwalazimisha wakulima wazitafute kwa njia nyingine. Ni kwa sababu mkulima anakosa option, kwa hiyo inabidi awatafute walanguzi. Niiombe Wizara ya Kilimo kupitia TFRA, ninatambua wanafanya kazi nzuri sana, lakini waboreshe eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ili kutatua hii adha ni kuhakikisha viwanda vyetu vya ndani tunavipa nguvu katika maana ya uwekezaji. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema tuna takribani viwanda 48 vya uzalishaji wa mbolea, lakini viwanda viwili tu; INTRACOM na Minjingu ndivyo at least vinazalisha, vinabeba viwanda vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa kumalizia, tutafute uwezekano wa kuwekeza kwenye viwanda hivi ili kuongeza tija ya upatikanaji wa mbolea na kuwarahisishia wakulima ili kupata mbolea na kilimo ambacho wanalima kiwe na tija na cha uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba muhimu ya Wizara hii nyeti ya Maji. Awali ya yote, niungane na Wabunge wote waliotoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji kutoka shilingi 898,000,000,000 mpaka shilingi trilioni 1.1, hili ni jambo kubwa, ni jambo la kujivunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii adhimu niwashukuru na kuwapongeza timu nzima ya Wizara ya Maji ikiongozwa na Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso, lakini pia Naibu Waziri wake, kaka yangu Mheshimiwa Mathew Kundo, Katibu Mkuu Engineer Mwajuma, CEOs na MDs wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji. Kipekee salamu zangu za pongezi ziwaendee maafisa wanaosimamia huduma za maji Mkoa wa Mbeya. Mimi jimbo langu linahudumiwa na taasisi mbili: Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya CPA. Gilbert Kayange pamoja na Engineer Hancy Patrick kwa upande wa RUWASA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze kwa kusema mambo mawili; hatuwapongezi kwa sababu wapo Wizara ya Maji, tunawapongeza kwa sababu ya kupandisha utoaji wa huduma ya maji kufikia zaidi ya 92.5% mijini na 85.2% vijijini. Pia, tunawapongeza kwa sababu ya kupunguza malalamiko ya wateja kwenye sekta ya maji, jambo ambalo lilikuwa limekithiri miaka ya nyuma. Tunawapongeza kwa sababu ya kuja na mpango mkakati wa Gridi ya Taifa kutatua changamoto ya maji nchi nzima na tunaamini suala hili lilikamilika linaenda kuwa mwarobaini wa changamoto za maji nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza kwa sababu wanatupa uthabiti na matumaini ya Watanzania wote kwa kuwa na uhakika wa huduma ya maji kwa sababu maji ndiyo huduma pekee ambayo haina mbadala. Tunawapongeza kwa sababu wanatii maandiko. Ukisoma Kitabu cha Waebrania 13:17 kinasema; “Watiini viongozi wenu, na kushika amri zao, wao huchunga roho zenu usiku na mchana na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu, kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha la sivyo watazifanya kwa huzuni.” Wao ndiyo wanampa furaha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu hana stress, wanaisimamia vyema Wizara ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa pamoja na salamu zangu niseme mambo machache: Mbeya Vijijini, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetuletea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Hata hivyo, ninaomba nimwombe Waziri, Mheshimiwa Aweso tuna miradi saba inayoendelea, hii miradi inasuasua tunaomba fedha ili wakandarasi warudi site kwa ajili ya kutekeleza mradi. Mathalani Mradi wa Izyra ambao upo 55%; Mbagala Iyunga, Mwakasita upo 50%; Mradi wa Masoko upo 40%; Ilea - Ihango upo 80%; Iwalanje-Tembela 75%; na Isuto kisima pale kipo 95%, tunaomba fedha ili miradi hii ikatekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, ninaomba nijikite na nijielekeze kwenye ushauri. Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha uliopita ilikuwa inadai taasisi za Serikali shilingi bilioni 61. Mkoa wa Mbeya tuna Mradi wa Maji wa Mto Kiwira una takribani zaidi ya shilingi bilioni 119. Mradi huu unaendelea vyema lakini tunaamini hizi fedha ambazo tunadai kwenye taasisi zingepatikana leo hii Wanambeya wote na huu mradi unaenda Mbeya Vijijini kwenye kata tano: unapita Swaya, Utengule Usongwe, Nsalala, Kata ya Bonde la Songwe, Iwindi na baadhi ya maeneo ya karibu ya Mshewe. Zikilipwa hizi fedha miradi kama hii ingemalizika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tukubaliane kuiunga mkono Wizara ya Maji na sisi tumwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Mtendaji Mkuu wa Serikali aziandikie taasisi hizi ziweze kulipa madeni haya ili miradi mingine iendelee kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuna utaratibu lazima tukubaliane, umewasilisha na saa hizi tunaelekea kuweka ushirikiano mkubwa na sekta binafsi. Sekta binafsi haijalishi ni mtu mmoja au watu sita, kuna utaratibu kupitia Sheria ya Maji inayosimamia rasilimali za maji Namba 11 ya Mwaka 2009, kwa wateja kuchimba visima. Utaratibu huu umekuwa na malalamiko kidogo na muda mwingine taasisi kukinzana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mteja anatakiwa aombe kibali cha kuchimba kisima kwenye Bodi za Mabonde, lakini waliokasimiwa kisheria ya kutoa huduma hasa mijini ni Mamlaka za Maji. Sasa Sheria ile inaeleza, mteja apewe kibali mahali ambapo mtandao haujapita. Mheshimiwa Waziri, ninaomba sana uliangalie hili, watekelezaji wa kutoa kibali cha uchimbaji wa kisima wapewe Mamlaka za Maji. Wao ndiyo wanajua wapi hakuna maji, wapi tutapeleka maji na lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Hii itaondoa migongano, lakini pia itaondoa migongano ya taasisi kwa taasisi lakini pamoja pia na wateja kupata huduma kwa haraka kwa kuondoa bureaucracy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kwa heshima sana kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kwanza katika kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo, ahadi ya siku 100 kuhakikisha anaajiri watumishi 7,000 nchini kote. Nasi Mbeya Vijijini, kwenye ajira hizi 7,000 tumenufaika kwa kupata watumishi 115 wa kada mbalimbali zikiwemo afya, elimu pamoja na ugani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuupongeza uongozi mzima wa Wizara hii nyeti ya Utumishi wa Umma, ikiongozwa na Waziri, kaka yangu Ridhiwani Jakaya Kikwete, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu wote wanaohudumu kwenye hii wizara. Sambamba na hili, kwa kutambua kwamba hii ndiyo wizara inayosimamia utumishi wa umma nchini, leo hii tunapojadili na kupitisha bajeti hii maana yake inawagusa watumishi wa umma wote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwanza, watumishi wote wa Jimbo la Mbeya Vijijini; watumishi wanaohudumu kwenye afya, watumishi wanaohudumu kwenye kilimo, watumishi wanaohudumu kwenye elimu (walimu), watumishi ambao wanaohudumu kwenye ugani na sehemu zote, wote waliopo Jimbo la Mbeya Vijijini. Pia niwapongeze watumishi wote ambao ni watumishi wa umma Tanzania nzima; tunatambua kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba nchi inakuwa yetu yenye ustawi kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende haraka sasa kutoa mchango wangu kwenye baadhi ya maeneo. Kwa sababu ya muda niaomba uridhie kwamba, nitakuwa ninaongea kifupi na kutoa ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia kiwango cha juu cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 tunahitaji sana mchango madhubuti wa utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninataka kusema jambo moja hapa; ninaomba niwakumbushe Wabunge wote na viongozi wote ambao wapo katika Bunge hili, lakini pia na wale viongozi wa utumishi wa umma, wakiwemo Ma-CEO katika maana ya Wakurugenzi wote, na maafisa usimamizi wa taasisi mbalimbali, kwamba ni lazima tuweke jitihada za makusudi za kuulinda utumishi wa umma. Tusikubali hata kidogo utumishi wa umma ukabagazwa ama ukatwezwa kwa namna yoyote ile, kwa sababu, ukirejea kwenye Mpango wa Maendeleo 2026/2027 utekelezaji wake gharama tunahitaji takribani shilingi trilioni 86.3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji na namna tutakavyogharamia huo mpango, 69% ni sekta binafsi, ambayo ni sawa na shilingi trilioni 60, na 30.4% sawa na shilingi trilioni 26 ni sekta ya umma; katika maana ya kwamba ni watumishi wa umma watakao-play part kuhakikisha kwamba mpango huu unatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; pamoja na hizi ajira ambazo zinaendelea kutolewa na Serikali yetu, ninaishauri Serikali kuongeza wigo wa ajira nchini. Hapa nishauri mambo machache. Ni lazima tukubaliane nchi yetu inapambana sana kuhakikisha kwamba inaziba lile gap la ajira nchini; lakini bado tuna vijana wengi wasiokuwa na ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, kwa kuwa kuna utaratibu unaoendelea wa kuandaa andiko la mpango wa zile ajira za part time; niiombe wizara hii iharakishe iulete haraka ili tupitishe ili hizi ajira za muda ziweze kutambulika na ziingie sokoni ili kupunguza gap la watumishi la vijana wetu ambao hawapo kwenye utumishi wa umma, wapo mtaani tu bila ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kwa hawa watumishi wanaojitolea. Mimi nimekuwa mtumishi, watumishi wa umma hawatoshi nchini. Mara nyingi tumekuwa tukitatua majukumu mbalimbali kupitia watumishi wanaojitolea. Hapa nishauri jambo dogo, ninaomba, ninafahamu hofu iliyo na dhamira njema ya Wizara hii na viongozi hawa juu ya watumishi wanaojitolea. Watumishi hawa wanaojitolea wakati ajira zinatoka wapewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano wa watumishi ambao wanahudumu mwaka mmoja, hadi miaka miwili, akitoa huduma ya kujitolea kwa uzalendo ajira zinapotoka hapati zile ajira, lakini ametumikia miaka miwili. Hili jambo si sawa, liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri sehemu nyingine, eneo la vetting (upekuzi). Kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma hasa kwenye nafasi za madaraka, ili mtumishi a-qualify pamoja na qualification zingine, kuhudumu nafasi ya madaraka kwenye utumishi wa umma ni lazima apitie process za upekuzi (vetting).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kupitia wizara hii ninaomba nishauri machache. Kwanza, ninaomba sana, ikiwezekana, kwa sababu zile veting, hivi sasa hivi kwenye taasisi nyingi sana, hasa mashirika binafsi, ukienda unakuta watumishi wengi wa umma wenye nafasi za uongozi hawana hizo nafasi katika utimilifu wao bali wanakaimu. Hii inatokana na sababu kwamba mchakato wa kufanya upekuzi kwenye nchi yetu unachukua muda mrefu. Unachukua kuanzia miezi sita, miezi nane na wakati mwingine hata mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa kushauri jambo moja, kuona uwezekano wa upekuzi kufanyika katika local level, katika maana ya mikoani na wilaya. Ninafahamu, kwamba Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi kupitia Ofisi ya GSO (Government Security Office) inashirikiana na RSO inashirikiana na ma-GSO kufanya upekuzi. Wawaache hawa ma-RSO, ma-GSO wafanye upekuzi ili wawaletee taarifa kuharakisha huu utaratibu wa upekuzi kwa watumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uhamisho na hapa ninaomba nisisitize jambo moja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Baadaye nitaleta taarifa; moja ya jambo ambalo ni janga la Taifa ni hili suala la uhamisho. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya watumishi wa umma kukataliwa uhamisho. Sisi kama Bunge, tuielekeze Wizara ya Utumishi. Kwa mujibu wa kanuni mtumishi anapokuwa amekaa ile miaka stahili miaka mitatu kwenye kituo chake aruhusiwe kuhama…
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)