Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. NAOMY D. MWAIPOPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa pumzi, lakini kipekee ninashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu na nyeti kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa pongezi kwa Wizara, kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha miundombinu na pia madawa na vifaatiba vinapatikana kwenye hospitali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, ninaomba niishukuru Wizara pamoja na Rais kwa kuamua kujenga hospitali ya kanda katika Mkoa wa Kigoma. Kigoma ni mkoa wa pembezoni, lakini Kigoma ni mkoa wa kimkakati. Kwa nini ninashukuru?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma tumepakana na Burundi na Congo. Hii hospitali ikikamilika tutakuwa na utalii tiba. Watu watatoka Congo kuja kujifunza, lakini watakuja kutibiwa kwenye hospitali hii ya kanda. Kwa hiyo, nishukuru na nipongeze kwa jitihada kubwa za Serikali ambazo zimeifanya hospitali hii kujengwa kwenye Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninashukuru kwa bajeti ambayo imetengwa ya shilingi 8,000,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hii. Ninaomba kwenye bajeti ya mwaka 2025 tumeona ilitengwa, lakini fedha hazikuja. Kwa hiyo, kipekee kabisa Mheshimiwa Waziri tunaomba hii fedha ije ili tukamilishe ujenzi wa hospitali ile ya kanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa tu, Kigoma kunajengwa Chuo Huria cha Muhimbili. Kupitia hospitali hii, itakuwa rahisi kwa wanafunzi wa Chuo cha Muhimbili kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye hospitali ya kanda pale Kigoma. Kwa hiyo, hii inaonesha ni namna gani hii fedha inahitajika ije haraka kukamilisha kuendana na kasi ya ujenzi wa chuo, lakini iende sambamba na ujenzi wa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, sisi Wanakigoma, tunaomba hizi kasi za maendeleo ambazo Serikali imeamua kuzifanya kwenye mkoa wetu, tunashukuru, lakini tunaomba utekelezaji uwe kwa kasi kidogo. Ninaamini umenisikia na Mheshimiwa Waziri atalichukua; ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nizungumzie suala la ugonjwa wa ini. Kama nilivyosema, Kigoma tuko pembezoni. Ugonjwa wa ini Kigoma unamaliza ndugu zetu. Ugonjwa wa ini Kigoma unatafuna majirani na marafiki zetu. Ninaiomba Wizara, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-wind up atuambie amejipangaje kutoa elimu na kutokomeza ugonjwa huu kwenye Mkoa wa Kigoma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanakufa. Ninaiomba Wizara ije na mpango mkakati wa namna ya kuelewesha wanawake, lakini pia wananchi wa Mkoa wa Kigoma kujikinga, lakini pia kuwa makini na ngono zembe kwenye suala hili la ugonjwa wa homa ya ini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi hawana elimu, lakini Wizara ikichukua jitihada za makusudi kama zilivyochukuliwa kwenye VVU na UKIMWI, ninaamini kabisa elimu itafika kwa wahusika na watu watachukua tahadhari. Ninaiomba sana Wizara ije na mpango mkakati, tunatokaje kwenye suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ninaomba kwenye suala la watu wa figo, gharama za kufanya dialysis kwenye huu ugonjwa zimekuwa kubwa. Kwenye Private Sector huko watu wakienda watu wanakosa huduma kwa sababu ya kukosa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Wizara ije na namna nzuri ya kuwasaidia hawa watu kwa sababu mtu akishakuwa mgonjwa, hana uwezo wa kuingiza uchumi, hana uwezo wa kupata fedha kama alivyokuwa mzima. Kwa hiyo, Serikali ikiona namna ya kupunguza kidogo au kubeba hizi gharama itasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)