Answers to supplementary Questions by Hon. Rahma Riyadh Kisuo (9 total)
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
kwanza kabisa nishukuru kwa majibu mazuri ya Wizara, na
niipongeze Serikali kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa sana
umefanyika katika sekta ya elimu. Kuna mikakati mingi imefanyika
na Serikali ya Awamu ya Sita, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na miradi
hii ya kimkakati kutoa ajira kwa vijana, je, Serikali ina mpango wa
kuweka Sera au miongozo itakayolazimisha miradi yote ya uwekezaji kutenga asilimia maalumu ya ajira za kitaalamu kwa
wahitimu hawa wa vyuo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO): Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakubaliana na mwuliza swali 100% kuwa miradi ya kimkakati
imeonesha uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira. Hata hivyo, Sera za
Ajira zinaelekeza ajira zitolewe kwa ushindani bila kutoa
upendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira, na Mahusiano inaendelea kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Na.1) ya
Mwaka 2015, ambapo pamoja na mambo mengine inaelekeza
wafanyakazi wa kigeni yaani wataalamu kurithisha ujuzi kwa
wazawa katika ajira za kitaalamu ili pale kibali cha kazi cha
wageni kitakapokwisha, mzawa aweze kuchukua nafasi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali itaendelea kutoa
kipaumbele kwa wafanyakazi wazawa katika miradi ya kimkakati
kwa nafasi za kazi ambazo utaalamu wake siyo adimu katika soko
la ndani ya ajira. (Makofi)
MHE. ASHA J. FERUZ: Mheshimiwa Mwenyekiti, jina langu ni
Asha Juma Feruz, Mwakilishi ninayewakilisha kundi la Vyuo Vikuu.
Ninaomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani
maalumu katika kutumia fursa za ajira katika kundi la vyuo na
vyuo vikuu kupitia mahusiano ya kikanda na kidiplomasia
tuliyonayo hasa zile kozi tunazoziita rare professionals? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO): Mheshimiwa Mwenyekiti,
Serikali kwa kushirikiana na vyuo na vyuo vikuu, imeanzisha
mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo
katika ngazi mbalimbali za elimu za vyuo na vyuo vikuu na vyuo
vya kati ikiwa ni sehemu ya mtaala ili kuwawezesha kuhitimu elimu
katika ngazi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inatoa Mafunzo ya
Internship yanayojumuisha wahitimu wa ujuzi wa ngazi mbalimbali
za elimu hususan elimu ya juu na kati ambapo wanapatiwa fursa
ya kujifunza kwa vitendo mahali pa kazi. Lengo la mafunzo hayo
ni kuwapatia wahitimu ujuzi, maadili ya kazi, uzoefu na kufanya
kazi za taaluma zao na kuwawezesha kuajirika. (Makofi)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya ngongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, utaungana na mimi kwamba, katika majibu yake ya msingi kuna programu mbalimbali ambazo wamezianzisha kupitia Wizara hii. Nataka kufahamu programu hizo zilizoanzishwa, kama Wizara, imechukua hatua gani ya kuwasaidia vijana, hasa wa vijijini kuzijua fursa hizo na kuweza kuzipata kwa urahisi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kuna vijana wana vipaji mbalimbali, lakini vijana hao Serikali bado haijawatambua na kuwawezesha kiujumlajumla. Nataka kujua ni upi mpango wa Serikali wa kuwasaidia vijana hao moja kwa moja, ili zinapotoka fursa hizo waweze kuzipata kwa haraka, hususan katika mikopo mbalimbali? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K. n. y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Latifa Juwakali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuwezesha programu hizi kuwafikia vijana wa vijijini imeanzisha utaratibu wa kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, redio na magazeti. Aidha, elimu imekuwa ikitolewa kupitia makongamano na maadhimisho mbalimbali. Vilevile, baadhi ya fursa hizi zimekuwa zikibandikwa katika mbao mbalimbali za matangazo za watendaji kata na vijiji.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Muhsin Ussi, swali la nyongeza. Mawili, endelea.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutambua vijana wenye vipaji na kuwaunganisha katika fursa mbalimbali Serikali, kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Mfuko wa Uwezeshaji wa shilingi bilioni 200 za Mama kwa Vijana, Wizara hii imepewa jumla ya shilingi bilioni 30 za kuwawezesha vijana katika sekta ya ubunifu nchini, ikiwemo wasanii, wanamuziki, watengeneza maudhui maarufu kama content creators, influencers, waandishi wa habari na wabunifu mbalimbali wa kazi za sanaa kwa kuwapatia mikopo. Hatua inayolenga kukuza uchumi na ubunifu kwa kutoa fursa zaidi za kiuchumi kwa vijana.
MHE. MUHSIN HAJI USSI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha wale vijana ambao wapo vijijini hawana smartphone na hawana uwezo wa ku-access mitandao ya kijamii, wanaweza kufikiwa kwa haraka kuweza kupata taarifa husika juu ya uwepo wa fursa hizi kwa vijana Tanzania? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K. n. y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, hili nimelijibu pia, kwenye swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Juwakali. Kwa wale ambao hawataweza kupata access ya social media, tunaweza kutoa elimu kupitia makongamano na maadhimisho mbalimbali. Vilevile baadhi ya fursa zimekuwa zikibandikwa katika mbao mbalimbali za matangazo za watendaji kata na vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tunajua kwamba uchumi wa Geita unategemea sana sekta ya madini na nia ni kuhakikisha kwamba tunapata miradi mbadala ambayo tutakuwa hatutegemei madini tu. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo uchaguzi ulifanyika mwaka 2025 ilionesha kwamba tunaenda kupata miradi ambayo itaenda kukuza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwa ajili ya uhakika kwamba vijana wanapata ajira na wanaenda kukua kiuchumi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga hii miradi ili hao vijana wa Geita waweze kupata sehemu ya kufanya kazi na kupata ajira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali zuri la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Chacha Wambura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati ili kuzalisha ajira na fursa mbalimbali kwa vijana wa Mkoa wa Geita. Ninataka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge, Serikali iko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ningependa pia kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba uanzishwaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati unategemea bajeti ya Serikali iliyotengwa. Hivyo basi, Mheshimiwa Mbunge ushauri wake umepokelewa na utafanyiwa kazi kadiri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu, lakini nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri, je, watakubaliana nami kwamba, kutokana na uwepo wa vijana wengi sana wasiokuwa na ajira, ni dhahiri kwamba mipango yote iliyopo haijafanikiwa kutatua tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nilitoa ushauri huko nyuma kuhusu makambi ya kilimo kwa vijana. Siyo kweli kwamba kama yangetekelezwa, tatizo hili lingeisha kabisa na kuondoka katika Taifa hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunakubaliana sote kuwa suala la changamoto la ajira siyo kwa Tanzania pekee, hili ni suala la dunia nzima. Hata hivyo, Serikali imeendelea kutekeleza program na mikakati mbalimbali kama nilivyoeleza kwenye jibu la swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka 2024, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimepungua kutoka 8.2% mwaka 2021 hadi 6.2% mwaka 2024. Serikali itaendelea kupanga na kutekeleza mipango na program hizo na nyingine ili kuendelea kupunguza tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali lake la pili, Serikali ilipokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na moja ya utekelezaji wake ni Program ya Jenga Kesho Iliyobora ya BBT kutoka Wizara ya Kilimo ambapo vijana wanaendelea kunufaika na program hiyo. Aidha, Serikali itaendelea kuweka mikakati na kutekeleza kwa lengo la kuondoa au kupunguza tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia fursa nami nipate kuuliza swali la nyongeza. Ni ukweli usiopingika kwamba, kasi ya Serikali ya uongezaji wa ajira kwa vijana haiendani na ongezeko la vijana nchini na badala yake vijana wameamua kuchagua fursa ya kujishughulisha na shughuli za usafirishaji kwa maana ya bodaboda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa mikopo na vijana wale wameona njia rahisi ya mikopo wanayopewa kwa sababu haikidhi kwenye mitaji mikubwa, wanapewa fedha ndogo wameamua kwenda kununua bodaboda. Tunawapa bodaboda vijana wetu wakiwa wazima, lakini baada ya miezi, miaka tunarudi kuja kuwapa mikopo wakiwa walemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuokoa vijana wa Taifa hili kwa ajili ya kuweza kuwa na viongozi, na kupunguza gharama kubwa za kuja kuwahudumia walemavu tunaowatengeneza sisi wenyewe kama Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali katika kuwawezesha vijana kujiajiri na kupata ajira. Hivyo, suala la Mheshimiwa Mbunge, sisi tumelipokea kama Serikali na hivi karibuni tutawajia hapa hapa kuwapa mkakati mzuri tuliopanga kama Serikali kuweza kumudu madhila yanayotokea ya vijana katika shughuli zao wanazozitumia kujitafutia riziki za kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, amethibitisha kwamba vijana 6,367 wamepata ajira nje ya nchi, na vijana wengi wamekuwa na utashi wa ajira hizi, lakini wanakwazwa na masuala ya lugha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuandaa program maalum kwa ajili ya Watanzania ili wawe na lugha nzuri ambayo inakubalika nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je,...
MWENYEKITI: Mheshimiwa, swali la nyongeza ni moja tu.
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasikia swali vizuri.
MWENYEKITI: Naibu Waziri, hajasikia vizuri, hebu uliza kwa ufasaha.
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, Serikali imekiri kwamba vijana 6,367 wamepata ajira nje ya nchi. Vijana wengi wamekuwa na ari ya kufanya ajira hizo, lakini wanakwazwa na masuala ya lugha. Serikali ina mpango gani wa kuwaandaa vijana wetu ili wakidhi kigezo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, tunatoa mafunzo maalum mahususi kwa vijana wanaokwenda nje kwa ajili ya kufanya kazi. Naomba tupokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, juu ya mafunzo ya lugha, tuongeze katika program yetu ya mafunzo ambayo vijana wanapewa kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. LUCY EDWARD MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, nchi yetu tunajua inakwenda kwenye ajenda ya fifty fifty katika uongozi. Je, wanawafikiriaje vijana wa kike katika kuwapa kipaumbele katika ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikalini hatutoi ajira kwa upendeleo, kwa maana ya kwamba sheria inasema tutatoa ajira bila kujali jinsia, rangi, wala kabila. Tutatoa ajira kwa usawa. Kwa hiyo, kuelekea Dira ya 2050 Serikali itaendeleza jitihada zake za kutoa ajira kwa usawa bila kujali jinsia ili kutekeleza Dira hiyo ya 2050.