MHE. PROF. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, kwa kuwa taaluma ya teknolojia ya TEHAMA sasa hivi ni taaluma ya msingi sana katika maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali kwamba ujenzi wa chuo hicho uweze kupata kipaumbele. Hii itawezesha kwanza kunufaisha vijana ambao wakipata elimu hiyo wataweza kujiajiri kwa sababu ya ile elimu waliyoipata. Pia, hiyo itasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kutumia teknolojia ya maendeleo vijana wetu watakuwa wamepata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo basi, ombi letu ni kwamba, Serikali ione jinsi gani iweze kupata uwezeshaji wa ujenzi wa hicho chuo, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Profesa, amekuwa akilifuatilia suala hili kwa karibu kwa Mheshimiwa Waziri na pia kwangu. Hii inaonyesha kwamba ana hamasa kubwa ya masuala ya teknolojia ya Habari, na Wananchi wa Buhigwe pia wana hamasa hiyo. Nimhakikishie kwamba ombi lake tumelipokea, na tutatoa kipaumbele kikubwa katika ukamilishaji wa chuo hicho.
MHE. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi ninaomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi ujenzi wa ghala la kuhifadhia tangawizi katika Kata ya Munzeze, Jimbo la Buhigwe pamoja na mitambo ya kukausha tangawizi ili kuweza kuongeza ubora wa zao hilo. Pia Serikali iliagiza halmashauri iweze kuandaa eneo la kuwekeza kuweka hilo ghala pamoja na miundombinu mingine na halmashauri ilishaandaa eneo takribani eka 15 na ikaandaa hati pacha kati ya Wizara ya Kilimo na Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, swali langu ni kwamba, ni lini Wizara itaweza kuwezesha hilo ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo na kuweza kuboresha zao na tangawizi katika Wilaya ya Buhigwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninamshukuru pia Mheshimiwa Pius Yanda, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe. Jambo moja tu nimwambie kwamba haya yote aliyoyazungumza ni sehemu ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais hususan wakati anagombea Urais katika jimbo lake la kuhakikisha tunajenga ghala katika eneo lake aliloliainisha hapo pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kukaushia tangawizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Wizara ya Kilimo tukishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara tupo katika mpango huo wa utekelezaji na tuko katika hatua za tathmini na tukishamaliza tutafika katika eneo lake na kuanza hii shughuli. Ahsante sana.