Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Onesmo Merdson Mnkondya (3 total)

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza. Pamoja na kufunguliwa kwa maghala nane na kampuni nane, lakini pia kuwepo kwa vituo 85 na mawakala 174 Wilayani Mbozi, kwa nini msimu huu mbolea aina ya DAP imechelewa kufika kwenye jimbo langu na imefika wakati wa msimu wa kilimo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Jimboni kwangu mpaka hivi ninavyozungumza, wananchi wanalia sana, wanalalamika sana, video zao ninazo na nimewatumia Mawaziri. Wanalalamika aina ya mbolea ambayo wametumia mwaka huu, pengine kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kukosa uaminifu ama kutokana na kuchelewa kwa mbolea aina ya DAP ambayo wameizoea, wametumia mbolea mbadala na badala yake haijakidhi vigezo tulivyovizoea. Imepelekea mazao kudumaa, wananchi wameingia hasara, wananchi wanalia.

Mheshimiwa Spika, ipi kauli ya Serikali kwa wananchi hawa; na Serikali itafanya nini kuhakikisha msimu ujao wananchi hawa hawapati hasara ya aina hii na mnadhibitije hali hii isitokee kwa wakulima wangu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mnkondya kwa maswali madogo mawili mazuri na yenye kufuatilia maslahi ya wananchi wa Jimbo lake la Mbozi na Mkoa mzima wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza amezungumzia kwa nini mbolea ya DAP imechelewa mwaka huu. Niseme tu kwamba mbolea ya DAP sisi kama nchi tunaagiza kutoka nje ya nchi, na mahitaji ya DAP duniani sasa hivi yameongezeka hususan Brazil na nchi ya India.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mahitaji makubwa, maana yake sasa kumekuwa kama tunanyang’anyana katika ununuzi wa zile mbolea. Kwa hiyo, wale waagizaji wote waliopewa leseni za uagizaji waliweka order, na zilichelewa kutokana na mahitaji makubwa ambapo order zilikuwa zimefanyika kule nje ya nchi kwa maana ya India pamoja na Brazil

Mheshimiwa Spika, sasa kutokana na mahitaji yao kuwa makubwa, sisi tumeendelea kuzileta hizo mbolea hapa nchini na tumeendelea kuzisambaza japo zilichelewa kufika kwa wakati. Kwa hiyo, nikiri kwamba sisi kama Serikali tumeahidi katika msimu wa kilimo unaofuatia tutahakikisha waagizaji wa mbolea wanafanya hivyo kabla ya ule muda ambao msimu unakuwa umetarajia kufikiwa.

Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusu kauli ya Serikali, sisi tunachokisema ni kwamba, moja, wananchi ama wakulima wote nchini wawe wananunua mbolea kupitia kwenye mfumo rasmi ambayo tumeuainisha, na tumetoa hiyo elimu kwa wananchi ili inapotokea mwananchi amenunua mbolea haijaleta matokeo, sisi kama Wizara tumkamate yule msambazaji wa mbolea ama wakala.

Mheshimiwa Spika, tutamkamata, tutamfungia leseni yake na vilevile tutakuwa na nafasi sasa ya kumshurutisha ikiwemo kulipa fidia kwa wananchi ambao wameathirika. Sasa, hiyo ndiyo kauli ya Serikali na ninataka wananchi wasimamie hivyo kwa kununua mbolea katika mifumo rasmi ambayo tumeiainisha kote.
MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo inaendelea kuyatoa, lakini ninaomba niwe na maswali mawili ya nyongeza kwa Waziri wangu wa Ulinzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi hawa tangu mwaka 2022 wamekuwa na uvumilivu wa hali ya juu sana 2023, 2024 hadi 2025 na leo 2026 mnawaambia waendelee kuvumilia na waendelee kuwa na subira. Hii subira ni mpaka lini watapewa fedha zao wananchi hawa ambao wana shida sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wananchi hawa pia wana madai ya kwamba, ardhi yao imepanda thamani kwa sababu ya kucheleweshewa malipo yao na wengine wanadai ardhi yao warudishiwe waweze kuiendeleza na kuitumia. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari mimi na yeye tuandae mkutano kwa ajili ya wananchi hawa, tuonanenao, tuzungumzenao, pengine awape majibu zaidi ya Serikali kwa ajili ya madai yao ya shilingi bilioni 5.7? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba ni kweli wananchi wetu wa Itaka wamekuwa wavumilivu, lakini Serikali imelipa kipaumbele hili suala. Ndiyo maana tayari tumewasilisha fedha hizo shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanalipwa na tayari tuliweka kwenye bajeti iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali, kwa maana ya Wizara yetu ya Ulinzi, inafanya mawasiliano ya karibu sana na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha kwamba kabla mwaka wa fedha haujaisha wananchi wetu wawe tayari wameanza kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge ameomba niweze kuambatana naye kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wetu wale. Niko tayari kwa ajili ya kuambatana na Mheshimiwa Mbunge, ili tuweze kutafuta suluhu ya maswali ambayo watauliza na kutoa ufafanuzi, ahsante.
MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa majibu ambayo imeyatoa kuhusiana na tawi hili la DIT, lakini ninaomba niwe na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kufuatia kile kinachofundishwa kwenye chuo hiki ambacho kiko chini ya Dar es Salaam Institute of Technology – DIT ambacho kimejikita zaidi kwenye ufundi, ni lini upanukaji wake utalenga taaluma ambazo zitaendana na mazingira ya Mkoa wa Songwe, hasa biashara, kilimo na kadhalika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ili kuusisimua Mkoa wetu wa Songwe, ikizingatiwa ni mkoa mchanga na kuupa uchumi na maendeleo zaidi, ni lini Serikali itajenga chuo kikuu Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe ambayo yapo Wilaya ya Mbozi ambapo tayari mahali hapa tuna maeneo ya kuanzia kujenga kama Msense, Mifugo Kata ya Isansa; Zelezeta, Mbozi Missiyon Kata ya Igamba; Ipunga pamoja na Hasamba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Onesmo kwa ufuatiliaji wake wa karibu kuhusu kuongeza vyuo vikuu katika Mkoa wa Songwe. Alishawahi kunifuata ofisini akifuatilia suala la Chuo cha VETA Songwe ambacho kwa sasa kinaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi, hivi sasa Serikali inaendelea na upanuzi wa chuo hicho, na nia ya kuongeza chuo hiki ni kuongeza udahili wa wanafunzi na taaluma ambazo zitatolewa katika chuo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mawazo ya Mheshimiwa Mbunge au ushauri unaenda sambamba na azma ya Serikali katika upanuzi wa chuo hicho. Kwa hiyo, ushauri wake au mawazo yake tumeyapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kama nilivyoeleza katika swali la msingi, kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu katika kutanua vyuo vikuu na kuongeza kampasi katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania. Mpaka hivi sasa mikoa 16 imeshapata kampasi ya vyuo mbalimbali ikiwemo hii ya DIT Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, UDSM imepeleka kampasi Lindi na Kagera, AIA imepeleka kampasi Manyara, TIA imepeleka kampasi Mwanza na maeneo mengine na mikoa mbalimbali ina kampasi mbalimbali za vyuo vya elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali itaendelea kuongeza taasisi hizi kulingana na uwezo na bajeti itakavyoruhusu. Hivyo, pale bajeti itakaporuhusu, basi tutaweza kupeleka chuo kikuu katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)