Supplementary Questions from Hon. Nuru Issa Kashakari (4 total)
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Afya cha Kazulamimba, Kituo cha Afya cha Kata ya Mwakinzega na ni lini pia Serikali…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge swali la nyongeza ni moja tu.
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge akiulizia kuhusu Kituo cha Afya cha Kazulamimba. Kituo cha Afya cha Kazulamimba ni pamoja na vituo vya afya 341 ambavyo tumeviainisha. Tutaendelea kutenga fedha za ndani za halmashauri na zile za Serikali Kuu ili kuhakikisha kituo hiki cha afya kinaanza kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza linalohusiana na lini Serikali itajenga Daraja la Mto Malagarasi kule Ilagala? Pia ni lini Serikali itajenga Barabara kutoka Simbo – Kalya ili kuwanusuru wananchi wa Sunuka, Herembe, Mwakizega, na Buhingu?
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa sababu pale tuna Hifadhi ya Mahale, kwa hiyo, inasababisha watalii kupata usumbufu mkubwa sana. Kwa hiyo, ninaomba jibu kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Daraja la Malagarasi maarufu kama Malagarasi Chini ambalo liko kwenye Barabara ya Simbo – Ilagala – Kalya ni daraja ambalo tumeshakamilisha usanifu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo daraja lipo, tutalihamisha, tutalipandisha kwa juu. Tumeshakamilisha usanifu, tupo tunaendelea na mazungumzo na wenzetu wa World Bank kupitia utaratibu wa CRW ili tuweze kulijenga daraja hilo. (Makofi)
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kigoma Kusini lina vituo vya Polisi vitano ambavyo ni Kituo cha Polisi Kazuramimba, Kituo cha Polisi Sigunga, Kituo cha Polisi Ilagala, na Kituo cha Polisi Buhingu. Vituo hivi havina majengo, badala yake wamekodi majengo binafsi kwa watu. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivi vya Polisi ili kuleta hadhi ya Jeshi la Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Nuru, Mbunge wa Kigoma Kusini kwa hoja yake ya kuimarisha vituo vya Polisi na kujenga vituo vya Polisi kwenye maeneo aliyoyatamka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyoeleza kwamba kimsingi, maswali yanayoongezeka tayari majibu yake tulishayatoa, sasa na hili swali kuhusu lini; maana yake ni kwamba tutaanza mwaka wa fedha wa 2026/2027 kama mpango wetu tulivyoutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaomba kuwasilisha.
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Daraja la Mto Malagarasi kule Ilagala ni nyeti sana kwani wananchi wa Kata za Mwakinzega, Ilagala, Sunuka, Sigunga, Herembe, Igalula, Buhingu, Karia na Hifadhi ya Mahale ni waathirika, wanaishi Tanzania kama hawaishi Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mto Malagarasi pale Ilagala, ukifika pale wewe mwenyewe ukajionea wananchi wanavyohangaika na kutaabika, kwa kweli inaumiza sana. Ninaomba kuuliza swali Serikali. Je, ni lini sasa huu mpango utakamilika ili kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini wanapata huduma za barabara na lile Daraja la Mto Malagarasi kule Ilagala?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anakubali kuambatana nami twende akajionee jinsi wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini wanavyopata adha katika nchi yao?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu, mimi ninajibu kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Kwa bahati mbaya wakati ninakuja sikumwuliza kama atakubali hii hoja ya pili ya kwenda. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba nitakwenda kumfikishia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na kumwomba ili aweze kuambatana naye. Kama atanituma mimi kwa idhini ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi pia sitakataa maelekezo hayo, nitafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hoja yake ya kwanza, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa barabara hii pamoja na daraja hilo; na ndiyo maana imeshaanza hatua za awali za kufanya usanifu wa kina na baadaye tutafute fedha ili kuhakikisha kwamba wananchi aliowataja na maeneo mengine wanaweza kupata huduma hiyo ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.