Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Ramadhani Hamza Singano (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa fursa hii ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji ambayo iko mbele yetu. Kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wa Ta'ala kwa kutuwezesha wote kukutana leo hapa, siyo uwezo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze na kuwashukuru watu wa Wizara ya Maji, Waziri Aweso na Naibu wake Engineer Kundo, lakini nisimsahau Katibu Mkuu na watendaji wake wote wa Wizara ya Maji mpaka level za chini. Niwashukuru RUWASA, niwashukuru watu wa mamlaka zote, lakini na wale wa Bodi za Maji za mabonde ambao ndiwo wanabeba maono, maana wao ndio wanalinda vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wana misemo yao; wapishi wa pilau pamoja na viungo vingi lakini walaji wa pilau wakasema kachumbari iwepo ile ladha ipatikane vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hotuba nzuri ya Waziri iliyogusa kila sehemu, iliyoleta matumaini kwa Watanzania mpaka walioko kule Bumbuli wakinisikiliza saa hizi, basi mimi nimeona kuna maeneo machache niyachangie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye maombi ya mradi mkubwa pale Soni unaotakiwa kuhudumia vijijini tisa kwa Kata ya Mbuzii na Soni. Ninaamini na vile viporo kama saba watakuwa vimevizingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye kushauri na kuchangia maeneo mengine muhimu. Moja ya eneo muhimu leo kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi katika sayari yetu, tumeona twende na vyanzo vya kudumu ambavyo ni mabwawa, lakini vyanzo hivi ili viweze kudumu lazima tusiwasahau wale watu walioko katika Bodi za Maji za Mabonde kwa sababu ndio watalinda vyanzo, ndio watasababisha hata tope kuelekea kwenye mabwawa haya lisije likaenda kupunguza vina tukahifadhi maji machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine la Gridi ya Maji ya Taifa (National Water Grid). National Water Grid tunategemea maziwa makuu, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa kwa sababu haya maji yake ni matamu lakini kipaumbele ni Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Victoria kidogo ni la kipekee, yale mengine yako kwenye bonde la ufa, lakini pale ni ardhi tu ilititia, land subsidence ikatengeneza ziwa lile lina historia ya tofauti, lakini ziwa lile lina taarifa mbili nilitaka niziweke wazi. Moja, ni taarifa ya kijiolojia inayosema ziwa lile lilitengenezwa miaka laki nne iliyopita na baada ya miaka laki moja iliyopita lilipata mabadiliko ya kukauka kabisa na tukio la mwisho ni miaka 27,000 iliyopita na hali ya hewa ikabadilika, ziwa hilo likajaa miaka 14,000 hadi 15,000 iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuanzia miaka ya 1920 na 1950 mpaka miaka ya 2000, tunachoshuhudia kihaidrolojia tunasema ni zile fluctuation au mabadiliko madogo madogo ya mita moja na mita mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya ya tabianchi siyo mabadiliko madogo, ni mabadiliko ya kuzingatia, lakini tunachojiamini, nimepitia Mkataba wa UN wa nchi ambazo ziko kwenye Maziwa Makuu hasa Ziwa Victoria. Nimepitia makubaliano ambayo ni ya mwaka 2011 ya nchi kumi, nimepitia pia na Itifaki ya Basin ya Mto Nile, lakini article zote ukizingalia zinatupa matumaini kwamba National Water Grid inaenda kutekelezeka bila wasiwasi. Kwa nini? Ni kwa sababu ukiangalia kuna kitu wanaita renewable water resources, maji ambayo ni rahisi kuyapata kwa wepesi kwa ajili ya matumizi. Hii ni bilioni 13 mita kumi kwa ziwa zima, lakini upande wa Tanzania tuna bilioni 6.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi yetu yote ya Basin ya Ziwa Victoria ambako ndiko tunatoa maji ni 0.38 billion metre cubic ambavyo ya ziwa tu ni 0.2 billion metre cubic. Kwa maana ile bilioni 6.6 bado hatujaigusa. Kwa hiyo, tuko kwenye comfort zone. Bado tunaweza tukatoa bomba lingine tuka Ziwa Victoria kwa mageuzi makubwa haya ambayo watu wa Wizara ya Maji wamefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo manne sasa ya kushauri kitaalamu. Jambo la kwanza, kwa sababu kinachotusababisha tuone tuko salama ni zile takwimu za ziwa zilizochukuliwa tangu mwaka 1964. Sasa hali hii iendelee ili tuweze kufanya ufuatiliaji mzuri, lakini la pili tutakapotengeneza intake sasa kwa ajili ya National Water Grid takwimu hizi zitumike vizuri tusije tukafika mahala mabomba yakajaa hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri jambo lingine kwamba level hizi za ziwa zitumike kushauri watu wa ardhi msigawe makazi pembezoni mwa ziwa bila kufuata level hii. Imekuwa kuna hoteli kubwa za kitalii kuna wakati zinazama kwenye ziwa, hii haileti tija. Watu wafanye mipango endelevu ya kushirikiana, Wizara ya Ardhi unagawaje eneo lenye chanzo cha maji bila ku-consult wenzako bila kuwasiliana na wenzako?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme sasa, vile vidakamaji kwenye maeneo ambayo ni intake vilindwe sasa kwa umadhubuti ili isifike mahala kule tulikoweka intake zetu kunaanza kuingia tope na vina vya ziwa vinapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri eneo lingine la ulinzi wa vyanzo au uchafuzi wa vyanzo. Tukubali kwamba kuna elimu ndogo kwa jamii. Bado Wizara inahitaji kuwezesha kwenye eneo hili ili kuwaelimisha watu. Ni kweli watu wanaongezeka, lakini sasa ifike mahala tuangalie mbadala inakuwa ni nini. Elimu kwa jamii, ushirikishwaji wa jamii na utekelezaji wa sheria na kanuni lazima uzingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka, nina mambo mengi, lakini mengine nimeshayafikisha kwenye meza ya Waziri kwa sababu nimeona kabisa kuna maeneo sita nyeti nimeyachambua kwa kina nisingeweza kuyachangia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni motisha kwa watendaji wetu. Watendaji wakikumbukwa wana kawaida ya kuongeza ari, kawaida ya uwajibikaji na kujitoa kwa dhati. Ninaposema wapewe motisha simaanishi fedha. Mtumishi anapopewa cheti tu cha utambuzi kwamba umefanya kazi nzuri, kwenye National Grid wewe ulikuwepo, basi mtumishi huyu anakuwa na furaha kubwa sana. Vilevile, mafunzo ya kujiendeleza kielimu, lakini na kupewa kipaumbele kwa miradi mingine ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la mfuko maalumu kwa ajili ya utafiti. Leo kuna maeneo hatuwezi kupata mito wala maziwa inabidi tutumie maji yaliyoko chini ya ardhi na lazima tutangulize utafiti. Eneo hili lina pwaya, kwa hiyo, mkipata hela mnaanza kukimbizana tena, kumbe mngeweza kufanya. Nimefurahi Waziri alivyosema tayari wanaenda kutengeneza master plan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine tunataka maeneo ya kujenga mabwawa tuyajue mapema...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaomba nimalizie nukta moja kwamba niombe tena kuwe na ufuatiliaji wa kudumu wa zile takwimu za maji, mwenendo na ubora, lakini na tope linaloekea kwenye mabwawa litatusaidia kwenye intake zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii kwa kupata muda wa kuchangia wakati huu. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndio mwingi wa rehema na anayetujalia hata uwepo wetu hapa. Suala la mazingira na Muungano ni mambo muhimu sana lakini nimshukuru sana kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hata ile Sera ya Mazingira ya Mwaka 1997 wakati akiwa huko kwa maono yake mazuri tayari 2021 tumepata sera mpya ambayo imeboresha zaidi masuala mazima ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa na kumpongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye Hotuba hii ambayo ni jambo tunalolijadili liko chini ya Wizara yake Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa jinsi anavyoendelea kuitafsiri tabasamu ya Mama Samia Suluhu Hassan hasa anapopita kwa Watanzania na hili tumelishuhudia katika ziara zake mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana pia Waziri wa Ofisi hii ya Mazingira na Muungano ndugu yangu Mheshimiwa Injinia Masauni na Mheshimiwa Naibu Waziri wake ndugu yangu Mheshimiwa Ruben Kwagilwa jinsi anavyomsaidia Waziri wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nilikuwa mtendaji niwashukuru watendaji wote wa NEMC kuanzia wa juu mpaka wa chini kwa kazi nzuri wanayoifanya na kumwezesha Mheshimiwa Waziri naye atuletee taarifa iliyonona na iliyopendeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala mtambuka na ni suala ambalo limeongelewa pia katika vitabu vya Dini. Imenukuliwa katika Kitabu cha Isaya ya 32:19: “kwamba lakini mvua ya mawe itakunya (kwa maana itanyesha kwa lugha nyingine) wakati ambao wakati wa kupunguza miti ya msituni na huo mji utadhalilika.” Hii ni dalili kwamba tunapochafua mazingira kuna madhara yanajitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mvua nyingi itanyesha na mji udhalilike, maana yake kinyume chake kuna wakati tunapata ukame pia. Hata katika Quran imenukuliwa katika Surat Nuur aya ya 40 Mwenyezi Mungu anasema, akiyazungumzia mazingira, “Dhwaharal fasad fiilbarri walbahar bimaaakasabat ay’yin naas.” Ufisadi, uharibifu umeongezeka mno kuanzia bara na baharini kuanzia nchi kavu na majini kwa sababu ya mikono ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika andiko lingine Mwenyezi Mungu anasema katika Surat Yunus aya ya 44, “Inna Allah laayadhrumu nnasa shaian walaakinna nnasa anfusahum yadhwirimun.” Hakika Mwenyezi Mungu hajawahi kuwadhulumu watu bali nafsi zao wenyewe, maamuzi yao mabaya wenyewe, ndiyo yanawaletea madhara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye michango yangu ambayo nimeikusudia wakati huu. Jambo la kwanza ni jambo la kuboresha tozo katika Wizara hii ikiwepo na taasisi yake ya NEMC. Niungane na wenzangu waliotangulia wakiizungumzia ile polluter pays principle kwamba anayechafua mazingira lazima ashikwe tozo au mazingira yakichafuliwa lazima yalipiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa najiuliza mpaka najikuna kichwa. NEMC ana dude kubwa tumempa la kusimamia mazingira. NEMC ndiyo anawakagua watu wa migodi, NEMC ndiyo anawakagua watu wa gesi, NEMC ndiyo anawakagua wachimba mafuta na ana gharama kubwa hapo anaingia; kwa nini asiwe na tozo la uhakika? Kwani akipata asilimia moja moja tu si anayafanya mazingira yanakaa vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi akipata asilimia moja ya madini, akapata ya mafuta (wale wanaochimba visima vya mafuta) kwa sababu yeye ndiyo mkaguzi, akapata kwenye visima vya gesi hamwoni kwamba NEMC anaenda kufanya jambo kubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama percent zote hizi asilimia zote hizi zinaenda Wizara ya Fedha basi kama wanachukua moja kwa nini wasigawane na NEMC? Upo msemo mmoja wa kanuni ya dini unasema, “maa laa yatiibul wajibu ilaabihi fahuwal waajib.” Kinachosababisha wajibu utimie ndio wajibu wa kwanza kabla ya wajibu wenyewe. Sasa kama tunataka NEMC awepo pale lazima tozo lake tulizungumzie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shida ni sheria kwa nini isije hapa tukaisimamia Waheshimiwa Wabunge mpaka ikakaa sawa matozo haya yakamsaidia. Sioni kwa nini NEMC asipate tozo ya uhakika kwa sababu vyanzo vipo ni suala tu la kuweka sawa sheria kama ndiyo yenye shida. Hapa Mheshimiwa nimwombe Waziri hili alichukue kwa herufi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo wanaweza wakaongeza mapato ni kwenye biashara hii ya kaboni ya hewa ukaa (biashara ya carbon ambayo pia ndiyo hewa ukaa). Tunaitumia carbon kwa sababu ndiyo reference. Nchi 192 zilikaa katika itifaki ya Kyoto ya Mwaka 1997. Nyingine zilikataa, lakini mwaka 2015 kwenye yale Makubaliano ya Paris zote zilikubaliana hapa ndio msingi wa hewa ukaa ilipoanzia. Ni biashara kubwa ambayo elimu ni ndogo katika maeneo tunayoyaishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwamba ipo mifano ya kuangalia katika Wilaya za Tanganyika na Nyanda za Juu Kusini kwa sababu tayari wameshaanza kupata pato hili. Kwa hiyo hili lielekezwe kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri jambo lingine kwamba hewa hukaa katika maeneo ya baharini ni zao kubwa sana kwa sababu miti ya mikoko huwezi ukailinganisha na misitu ya kawaida. Katika bahari, zao la hewa ukaa linaweza likawa ni mara tano au mara 10 zaidi ukisoma makala nyingi za kimazingira. Kwa hiyo, ina maana mpaka sasa hivi tumepoteza dola nyingi sana na trilioni nyingi sana za mazingira. Nishauri pia kwamba elimu ya hewa ukaa inatakiwa ifike kwa viongozi wa chini mpaka wa vijiji kwa sababu hawa ndiyo wabeba maono ya wale wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri lugha zitumike nyepesi. Unaweza ukatumia carbon credit isieleweke, lakini kwa nini usiseme, “fedha zinazopatikana kwa utunzaji mzuri wa misitu na matumizi ya hewa safi? Kwa nini lugha kama hizo zisitumike ili kuhakikisha wananchi wanang'amua vizuri na kufikia malengo tunayoyakusudia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu isipopatikana basi pato la hewa ukaa au pato la biashara ya carbon tutalisikia na hatutafikia malengo. Kwa kuwa kuna wenzetu ambao wameshaanza, basi wengine wakajifunze huko ili tuhakikishe kwamba tunaendana na maono ya Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mdogo, lakini NEMC inakotokea imesonga mbele sana lazima tuisifie. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Aliwahi kusema mwanafalsafa Dkt. Kwame Nkrumah wa Ghana akasema, “those who would judge us merely by the heights we have achieved, would do well to remember the depth from which we started.” Wale wanaotupima kwa kimo tulichofikia wangefanya vizuri zaidi kama wangeanzia kwenye kina tulipoanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikushukuru kwa kuniona ili niweze kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kila rehema za kuwepo hapa. Mwenyezi Mungu ambaye hata ambayo bado hayakuwa anajua ikiwa yatakuwa, yatakuwaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu kipenzi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi makubwa ya kuwa Rais wa maono kugusa nyoyo za watu, lakini kuwa na mipango ambayo siku zote inaleta tija katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, ambaye naye ni kiongozi wa maono akitembea kama alivyo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili tumelidhihirisha pale ambapo alikuwa katika ziara za kimikoa, alipopita katika Mkoa wa Tanga, lakini Wilaya ya Lushoto halafu akafika Jimbo la Bumbuli ambalo mimi ndiyo mwakilishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii iliweza kufika Bumbuli Jimbo ninaloliwakilisha katika Kiwanda cha Mponde na walitoa tabasamu kubwa kwa wananchi wa Mponde kwa kuongelea, kupokea na kushauri kuhusu matatizo ya kiwanda hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi mzuri utamwona. Katika mashairi ya Ndugu Shaaban Robert alieleza sifa ya viongozi wazuri na viongozi wabaya, lakini viongozi wabaya alitumia mnyama kuku kwa sababu kuku ni mnyama yupo karibu sana na binadamu. Kwa kutumia lugha za vinaya na lugha za majazi akasema:

“Kuku akipata nyama, hukimbia ale peke,
japo wenzake watamuandama waishike,
katu hatokubali, iondoke mdomoni,
atatafuta mahali, ajilie kwa makini,
kuku akipata nyama, hukimbia ale peke.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia hayuko hivyo. Mama Samia yuko kama yule kiongozi aliyesifiwa na mwanafalsafa mmoja akiitwa Christopher Robin akamwambia: “You are braver than you believe, you are stronger than you seem and you are smarter than you think.” Christopher Robin walikuwa wakibishana sana na huyu jamaa yake, lakini kwa sababu ni mzalendo hakuacha kumsifia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye yale maeneo machache ambayo ninataka niyagusie. Kwanza kabisa ni eneo la afya. Ninashukuru sana Katika Jimbo la Bumbuli Mama Samia wakati ameingia tayari ametupatia zahanati 17. Mambo ya ajabu sana, mapinduzi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vituo vinne vya afya ambavyo viwili wakati wake vilianza na vingine ameviboresha hapo nyuma. Niombe sasa kidogo, maana imeandikwa katika Waraka wa Kwanza wa Wathesalonike 5:17-18 kwamba, “Ombeni pasipo na kikomo na shukuruni katika kila jambo.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiki Kituo kimoja cha Milingano, kimejengwa lakini hakijaweza kukamilika. Sasa ili tabasamu liwafikie wana Bumbuli niombe katika Wizara hii ya TAMISEMI sasa wakikumbuke kituo hiki ambacho kitaleta tabasamu kwa Watanzania walioko Bumbuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nihame niende kwenye eneo la elimu. Eneo la elimu Katika Jimbo la Bumbuli kuna mageuzi makubwa na Mama Samia avishwe taji lake. Hata hivyo, zipo shule chache kwa sababu ya umbali, basi hapa tutahitaji kupata mabweni kutoka eneo moja linaitwa Kwebamba kuja Kata ya Milingano, Sekondari ya Mibukwe. Kumbukeni Waheshimiwa Wabunge, umri tuliosoma sisi miaka ile ni tofauti na sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabinti wanachukuliwa kule kilometa 30, wanaenda sekondari inabidi wapangishiwe maeneo ya kuishi bila uangalizi. Kwa hiyo, eneo hili linahitaji mabweni ambayo yatasaidia watoto wa kike kupata haki yao ya elimu katika hali ya utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye eneo la vijana, wenzangu wamegusa maeneo mengi muhimu. Ninaomba nikumbushie tu suala la NIDA ni tatizo na niombe tamko maalum litoke ili wale wanaopaswa kutekeleza hilo wafanye mara moja, kwa maana vijana wanakosa fursa hii ya mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee tena katika eneo muhimu, eneo nyeti la barabara. Kwanza nianze kuomba kabla sijashauri niombe Barabara ya Mbelei – Ibaga – Mgwashi – Mkongowi – Milingano kilometa 42 ni barabara ya kimkakati. Ilijengwa kidogo na TARURA, lakini labda ni kwa sababu ya bajeti ghafla wakaondoka. Niombe hii ikumbukwe ili kuzidi kuleta tabasamu kwa Watanzania walioko pembeni mwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo ni kipaumbele pia kwa Wanabumbuli ni kilometa 22 kutoka Soni hadi Bumbuli – Dindila, lakini awamu ya kwanza kilometa 22 upande wa Bumbuli na kilometa 9.3 kwa upande wa Korogwe Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi muda ni mchache, lakini niombe kuna barabara ya kimkakati inayounga majimbo matatu: Jimbo la Mlalo, Jimbo la Lushoto, Jimbo la Bumbuli na hatimaye Korogwe Vijijini kilometa 87.3 ambayo ni Barabara ya Magamba – Mlola – Makanya – Milingano – Mashewa, hii nayo ni barabara ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mfupi niende kushauri kwa wenzangu wa TARURA, mimi ni Mhandisi niliyesajiliwa na Bodi ya Uhandisi nilitaka niwashauri kidogo katika mambo ya kitaalam. Muda usipotosha basi nitafikisha kwenye meza ya ndugu yangu Mheshimiwa Shemdoe ili aweze kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kwa sababu ya mvua nyingi na mabadiliko ya tabia ya nchi ndiyo yanasababisha hilo. Basi ni vizuri sanifu zetu ziwe ni Climate Resilience Design, kwa maana miundombinu iweze kustahimili mvua nyingi katika maeneo ya milima na maeneo mengine ya tambarare, lakini mifereji ya pembeni (side drains) ziwe za kutosha, lakini na mitaro ya kupunguza kasi ya maji ambayo kitaalam wanaita catch water drains. Kwa sehemu za tambarare kuna vitu vingine tunaita mitre drains zikiwekwa za kutosha zitaweza kuondoa maji haraka barabarani, lakini kutumia makaravati mengi na madaraja kwa maeneo ya milima huwa barabara zetu hazina tofauti na mfano wa nyoka kwa sababu ya kwenda na contour za milima..

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukakuta mto mmoja umeukatiza mara tano. Kwa hiyo, maeneo ya milima yapewe kipaumbele cha makalavati ili maji ndiyo adui wa kwanza. Wakati ninasoma Chuo Kikuu profesa wangu alinishangaza sana aliniambia adui wa kwanza wa barabara ni maji, adui wa tatu ni maji, wa pili na wa tatu kwenye barabara ni maji. Kwa hiyo, hii alikuwa akionesha msisitizo kwamba maji yasipotafutiwa njia yana kawaida ya kutafuta njia yake na hapo ndipo uharibifu utakapokuwa unatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe tunadhibiti maporomoko katika maeneo ya milima. Tujitahidi kuweka buffer zones ambazo mtu haruhusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu ikiwepo kilimo na kupanda nyasi pamoja na miti rafiki ambayo itazuia mmomonyoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine, mambo ni mengi, lakini nitayaandika ila niende eneo la ushirikishwaji wa jamii katika kutunza barabara. Hili jambo hapo nyuma lilikuwepo na wenzetu wa TANROADS kabla ya TARURA zilikuwepo hata kambi za ujenzi, ilikuwepo pale Mkuranga, ilikuwepo kambi ya ujenzi pale Manga ukielekea Tanga na maeneo mengine. Hizi zilifanya vizuri kwa sababu emergence zikitokea (dharura zikitokea) walikuwa wakizikabili mara moja. Sasa kwa sababu sina wasiwasi na TARURA, sina wasiwasi na wataalam wa Tanzania ninadhani walikalie hilo waliangalie upya, lakini jamii ishirikishwe kwa matengenezo madogo madogo na mikataba midogo midogo ambayo ni community-based contracts.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa elimu ni muhimu kwa jamii hii athari gani itapatikana ikiwa mifereji itakuwa haijadhibitiwa, ikiwa mifereji itakuwa imezibwa na watu wanaofanya shughuli za kilimo. Pia, kuunda vikundi vya ulinzi wa barabara kwa maeneo husika, leo barabara imekuwa ndiyo moyo wa Watanzania, barabara leo kama haipitiki, shughuli za biashara hazitafanyika, watoto hawataenda shule kwa sababu zitabomoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia katika eneo la kuweka vipaumbele katika barabara: barabara zetu ni lazima tuziwekee vipaumbele, tutenge barabara kwa makundi, ziwepo barabara za kiuchumi kwa maana ya barabara ambapo tutapitisha mazao na kwenda kwenye minada na masoko. Ziwepo barabara za huduma muhimu kwa mfano huduma za hospitali, lakini na kwenda shule, hizi barabara zipewe kipaumbele. Ukiangalia katika mtandao, Wilaya ya Lushoto ni zaidi kilometa 1,200 na kwa Bumbuli tuna kilometa 544. Kwa kuwa haya mambo ni ya kitaalam zaidi niombe niyafikishe kwenye meza ya Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Shemdoe, nami sina wasiwasi naye, atayafanyia kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache nikushukuru sana na niwashukuru viongozi wetu kwa kujitahidi kuonyesha tabasamu kwa Watanzania. Ninashukuru sana kwa kupata nafasi hii. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako.

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)