MHE. RAMADHANI H. SINGANO aliuliza: -
Je, Serikali inahakikisha vipi kuwa mikopo ya pato la halmashauri linawafikia vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramadhani Hamza Singano, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahakikisha mikopo ya 10% inawafikia vijana kwa kuzingatia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, pamoja na Kanuni na Mwongozo wa Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2024. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari, 2026, jumla ya shilingi bilioni 118.03 zimetolewa kwa vikundi vya vijana 8,165 vyenye wanachama 44,754 nchini kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(b) cha Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2024, asilimia nne ya mapato ya ndani yasiyolindwa hutengwa mahususi kwa ajili ya vijana. Hivyo mapato haya hulindwa kikanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inatumia mfumo wa kielektroniki wa WEZESHA Portal katika usajili wa vikundi, uwasilishaji wa maombi na usimamizi wa utoaji wa mikopo, huku Maafisa Maendeleo ya Jamii wakiendelea kutoa elimu na kusaidia vijana kuandaa miradi yenye tija ili waweze kukopesheka kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mikopo hii ya uwezeshaji ili vijana wajiajiri, waongeze kipato na kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.