Supplementary Questions from Hon. Eng. Ramadhani Hamza Singano (5 total)
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika mipango mizuri ni kuweka mipango ya muda mfupi ya kati na ya muda mrefu. Sasa kwa kuwa wananchi wa Tanga wameshahamasika sana na zao hili la maziwa, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuhakikisha kwamba wananusuru mapato haya yanayopotea katika zao la maziwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. Nami ninampongeza sana Mbunge mwingine wa Mkoa wa Tanga ambao kwa kweli kwa kiasi kikubwa wanafuatilia mgogoro huu kwa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza katika swali la msingi, mgogoro huu ni kipaumbele chetu kwa sasa. Tunaendelea kutafuta solution za muda mrefu, lakini hata za muda mfupi ikiwa ni pamoja na kuona namna gani tunaweza kutenga fedha kadri zinavyopatikana kuongeza juhudi ya kuhakikisha tunazuia upotevu wa malighafi hii ya maziwa kwa wafugaji wetu wa Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunaendelea kulifanyia kazi kwa karibu sana.
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Soni ni miongoni mwa miji mikubwa kibiashara kwa Jimbo la Bumbuli. Ni lini Serikali itafikiria kuwa na soko la kimkakati, kwa ajili ya kuongeza uchumi na kipato kwa wananchi wa Bumbuli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote yenye sifa za kujengewa miundombinu ya stendi, masoko na miundombinu mingine inaendelea kujengwa kwa awamu. Wajibu wa halmashauri ni kuandaa maeneo, kuandaa michoro, kuandaa makadirio na kuanza kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi na kuwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ili Serikali pia iendelee kuandaa bajeti, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Bumbuli, Engineer kwamba, tunatambua suala hilo. Serikali hii itakwenda kulitekeleza, lakini halmashauri pia waanze kutenga fedha kwa awamu, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Wilaya Lushoto miongoni ya wilaya ambazo maeneo machache yana changamoto ya maji juu ya ardhi ikiwemo Kata ya Milingano maeneo ya Kwebamba na Kishimai, lakini Kata ya Mbwei na Malibwi kwa Tarafa ya Mlola. Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kimkakati na wa kiutafiti kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanafanyiwa utafiti na kuwapatia suluhu ya changamoto ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ramadhani Singano, Mbunge wa Bumbuli, lakini kwa kumbukumbu yangu napata kujua kwamba kata hizi ambazo ameziongelea ziko katika Jimbo la Profesa Shemdoe ambazo ziko upande wa Lushoto, lakini kwa Kata ya Mbwei mwaka 2022 tulipata fedha za UVIKO kiasi cha shilingi milioni 430 mradi huu ulitekelezwa na unafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kuboresha kuna kuna chanzo cha mto fulani kitu kama Kiloleli, Kilole kitu kama hicho tunaendelea kufanya tafiti ili kubaini kama tuna uwezo wa kutumia chanzo hicho ili tupeleke maji tena kwenye Kata ya Mbwei lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ramadhani Singano ni mtaalamu wa masuala haya ya maji (water resources) tunatambua kwamba namna gani anatamani tuendelee kuhakikisha kwamba tunawatumia wataalam wa Wizara ya Maji kubaini vyanzo vipya ili tuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama. Tunaendelea kupokea maoni na ushauri ili tuendelee kuboresha upatikanaji wa huduma maji safi na salama kwa wananchi, ahsante sana.
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Mombo – Soni - Lushoto ni barabara ya kimkakati kwa majimbo matatu. Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuipanua barabara hii ili kukidhi haja katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge pia kwa kufuatilia barabara yake ambayo ni muhimu kwa sababu barabara ndiyo mishipa ya uchumi wa nchi yetu, lakini muombe awe na subira. Tutaendelea na mchakato Serikalini itakapokuwa tayari tutakwenda kuikamilisha na hivi ndivyo tunakwenda Serikalini kwa vipaumbele, baada ya kumaliza hatua moja tunakwenda hatua nyingine barabara moja tunakwenda barabara nyingine.
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze kwa majibu mazuri ya Serikali. Hapa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa NIDA ndiyo kitambulisho kikuu cha Kitaifa kwa vijana hawa ili waweze kuwa na sifa za kuomba hiyo mikopo, lakini katika Jimbo langu la Bumbuli maeneo mengi ni tatizo, je, ipi kauli ya Serikali kwa zile mamlaka zinazosimamia hili ili liweze kutekelezwa mara moja, vijana wasikose hii fursa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Serikali ina mpango gani madhubuti wa kufuatilia na kuhakikisha kwamba hili jambo linaenda kwa usawa katika maeneo ya majimbo yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Eng. Ramadhani Hamza Singano, Mbunge wa Bumbuli kwa namna ambavyo anawakilisha na kuwasemea wananchi wa Jimbo la Bumbuli kwa uthabiti wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba Serikali baada ya kuweka utaratibu, sheria na kanuni za mikopo ya 10%, eneo la mikopo ya vijana asilimia nne ni eneo ambalo linasimamiwa kwa ukaribu mkubwa kwa sababu Serikali inatambua changamoto ya ajira kwa vijana.
Mhesimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Bumbuli, na katika majimbo yote kote nchini ambako kuna changamoto ya vijana kupata mikopo hii kwa urahisi kwa wakati na kwa uwazi, Serikali itaendelea kuboresha mifumo yake kuendelea kufanya usimamizi na kutoa elimu ili vijana waweze kupata mikopo kiurahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mkakati wa Serikali ni kuendelea kuboresha, na ndiyo maana tumepitia kanuni zetu za mikopo 2024. Hata hivyo, tunaendelea kufanya tathmini kuona ufanisi wa utoaji wa hii mikopo na tutaendelea kuboresha, lengo likiwa makundi haya ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wapate mikopo kwa utaratibu mwepesi zaidi, lakini kwa ufanisi mkubwa zaidi.