Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Paschal Inyasi Chinyele (2 total)

MHE. PASCHAL I. CHINYELE aliuliza:-

Je, kwa nini wananchi wa Kata ya Mbalawala wamezuiwa kuendeleza ardhi wanayomiliki kwa maelezo kuwa ni sehemu ya Bonde la Kati Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Inyasi Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini. Bonde la Mzakwe linasimamiwa na Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu Water Basin na Mamlaka ya DUWASA na siyo Bonde la Kati la Singida kama swali lilivyoelekezwa. Bonde hili lilipimwa kisheria na kusajiliwa Aprili, 2000 kwa ramani yenye Namba 45977.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo lina ukubwa wa hekta zaidi ya 34,000 na lipo katika Kata za Chihikwi, Kawawa, Matangizi, Makulu na Mtaa wa Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu zilizopelekea kuzuiwa kufanya maendelezo katika bonde hilo ni kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuwa kuna zaidi ya visima 20 vinavyotoa huduma ya maji yanayotumika na wananchi wa Dodoma Mjini na maeneo jirani, eneo ilo kitaalam lina kimo cha maji kilichopo juu. Serikali imechukua hatua za kusitisha upimaji na umilikishaji pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari ya kuendeleza eneo hilo.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga mabwawa ya umwagiliaji katika Kata za Mbabala, Mpunguzi, Matumbulu na Mbalawala ili vijana waweze kujihusisha na kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ili kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuvutia vijana kujishughulisha na shughuli za kilimo, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imechimba visima saba. Katika kata za Matumbulu, viwili; Mbabala, viwili; Mpunguzi, viwili; na Chisichili, kimoja, Mkoani Dodoma. Visima hivyo vina uwezo wa kumwagilia eneo lenye ukubwa wa ekari 280 na kunufaisha wakulima 378.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali katika mwaka wa fedha 2026/2027 itachimba visima vitatu. Katika Kata za Mbabala, kimoja; na Mbalawala, viwili. Aidha, Serikali inaangalia uwezekano wa kuchimba mabwawa madogo au kusimika matenki ya kuhifadhia maji yatayotumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo.