Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Paschal Inyasi Chinyele (9 total)

MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mitaa hii mitano na siyo Kata, Mitaa hii mitano ilipimwa kama vijiji mwaka 1973. Je, ni hatua gani Serikali inachukua kuwanusuru wakazi wa Kata hii ya Mbalawala wapatao takriban 12,000 ambao wanategemea ardhi hii kwa maisha yao ya kila siku? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati Serikali inajiandaa kutwaa Bonde la Mzakwe iliwafidia wakazi wa vilivyokuwa vijiji vya Mzakwe na Mchemwa, baadhi kuwahamishia katika Kata ya Chahwa ambayo sasa hivi iko kwenye Jimbo la Mtumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wakazi wa mitaa hii ya Kata ya Mbalawala ili wapishe Bonde la Mto Ruvu kama ilivyowafidia waliokuwa wakazi wa Vijiji vya Mzakwe na Chahwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Inyasi, Mbunge wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la pili, kwa maana kwamba sisi TAMISEMI ndiyo wamiliki wa ardhi, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona namna gani ya kuendelea kuwafidia wale ambao hawajapata kwa sababu Serikali imeendelea kutoa fidia katika maeneo mengi sana nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Ardhi kuona namna gani tunaweza tukafikisha maendeleo haya kwa wananchi wetu kwa maana ya kwamba vijiji vimeshapimwa toka mwaka 1973, tuone namna gani sahihi ya kuendeleza eneo hili. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itatekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda katika kongani za viwanda katika kata za Nala pamoja na Mpunguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini, kwa kuwatetea wananchi wa Dodoma, hususan wananchi wa Nala na wananchi wa Mpunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wetu wa miaka minne, tume-commit kuanzisha miradi saba ya kielelezo (National Flagship Programs). Katika ile miradi saba ya kielelezo, tunakuja kuanzisha kongani ya viwanda eneo la Nala ambayo kimsingi tunaweka pale viwanda vya kuchenjua dhahabu kwenye madini ambayo ni rare na critical, kwa mfano lithium, cobalt, nickel na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo la Mpunguzi tumelitenga kama eneo la mkakati kwa sababu Mpunguzi wanazalisha sana zabibu. Kwa hiyo, ninamwondoa mashaka Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini, kwamba hili lipo kwenye mpango wetu wa miaka mitano. Pia, tumeliingiza na kwenye mpango wa mwaka mmoja, tumelitengea bajeti. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wakazi wa Mitaa ya Kata za Chang’ombe, Nkuhungu, Mnadani pamoja na Nala, wanakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa maji. Hii ni kutokana na kuzidiwa kwa Mfumo wa Maji wa Mzakwe. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi ya maji ya Nzuguni, Nala pamoja na Zuzu ili kuepusha uhaba huo wa maji? Katika kata hizi, vipo vituo vya afya kama Chang’ombe pamoja na Zuzu, lakini havina maji. Ni lini Serikali itashughulikia tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jiji la Dodoma ambapo nikiri kabisa kwamba hata ofisini kwetu ameshakuja mara kadhaa, ili kuendelea kuwasemea wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini, wakiwemo Wabunge wanaoishi katika Jiji la Dodoma. Mheshimiwa Chinyele, kwenye suala la miradi yetu, tunao mradi wa Nzuguni, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi 9,000,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nzuguni One ambapo mradi huo umefikia 98% bado tu kidogo ukamilike. Pia tuna Nzuguni Two ambao unaendelea. Tuna mradi wa Nala ambao pia Serikali imewekeza shilingi 4,000,000,000, tunao Mradi wa Zuzu ambao tumeweka shilingi 7,000,000,000 ambapo kwa ujumla wake huo, mahitaji ya Jiji la Dodoma ni lita 160,000,000 mpaka sasa uzalishaji wetu ni lita 80,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii mitatu yote itakapokamilika tutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 80,000,000 mpaka lita 120,000,000. Maana yake ni kwamba tutakuwa tumefikia zaidi ya 80% ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea na michakato ya miradi hii, na ipo katika hatua nzuri kabisa. Miradi hii itakapokamilika wananchi wa Jiji la Dodoma pamoja na Jimbo la Mtumba itakuwa ina uhakika wa kupata majisafi na salama, wakiwemo Wabunge wanaoishi katika Jiji hili la Dodoma.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi (Dodoma Polytechnic College) katika Mtaa wa Lugala, Kata ya Mbalawala. Je, ni lini Serikali itaanza kuchukua wanafunzi katika chuo hicho ambacho kiko ndani ya Jiji la Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chinyele, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imekamilisha kwa kiasi fulani ujenzi wa Dodoma Polytechnic, na kama Mheshimiwa Mbunge anakumbuka vizuri tulifanya ziara pamoja katika chuo kile na hatua iliyofikia ni nzuri. Kwa hiyo, tu nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaenda kumalizia ukamilishaji wa chuo kile na matarajio ya mafunzo ni kuanza mwaka huu wa 2026/2027. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, Serikali imeamua kuhamia Dodoma, na kwa kuwa, Jiji la Dodoma linazidi kupanuka siku hadi siku, na kwa kuwa, katika baadhi ya kata za pembezoni, sasa ujenzi unafanyika kiholela kwa sababu hakuna barabara za mitaani, je, Serikali haioni kiwango hicho cha shilingi bilioni 10 kilichotengwa ni kidogo kulingana na hali halisi ya Jiji la Dodoma linavyopanuka na linahitaji barabara nyingi zaidi, kwamba walau Serikali ingeweka zaidi ya shilingi bilioni 10 ingekuwa na afadhali? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali imejipanga vipi kujenga barabara za lami katika mitaa ya Makole, Medeli, Matumbulu, Chigongwe, Mbabala, Mbalawala, Nala, pamoja na Mpunguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Paschal Chinyele, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kazi kubwa anayoifanya na kwa hakika anawasemea wananchi wa Dodoma Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunajenga makao makuu ya nchi ya kisasa yenye barabara na miundombinu bora. Ndiyo maana katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeendelea kujenga barabara za mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunafahamu, pamoja na fedha hizi ambazo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, Serikali imekuja na mpango mahsusi kwa ajili ya kujenga barabara katika Jiji la Dodoma. Mpango ambao unaitwa Dodoma Integrated Sustainable Transport Program ambao barabara za TANROADS pamoja na za TARURA zitajengwa kwa kiwango kikubwa. Hivi sasa Serikali iko hatua za manunuzi kwa ajili ya kumpata Consultant kwa ajili ya design ya mradi na kuhakikisha tunajenga barabara hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni kuendelea kuboresha barabara katika kata za pembezoni ambazo amezitaja: Kata ya Mbalawala, Mbabala, Matumbulu, Mpunguzi, Chigongwe na Nala. Hizi ni sehemu ya barabara ambazo zitakwenda kujengwa kuhakikisha kwamba jiji letu linakuwa na barabara bora, pamoja na barabara za mitaa yote. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufanya upanuzi wa barabara tatu zinazokwenda Mikoa ya Iringa - Singida pamoja na Arusha. Hata hivyo, Serikali bado hawajalipa fidia wakazi wa Jiji la Dodoma hasa katika Kata za Kikuyu, Mkonze, Mnadani, Nala, Chamwino, Mnadani pamoja na Miyuji. Je, Serikali ina mpango gani kuwalipa wakazi hao kabda ya upanuzi wa barabara hizi haujaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Chinyele kwa kufuatilia ulipaji wa fidia wa wananchi wake kwa wale hasa ambao watapitiwa na miradi ya kupanua barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kuanza kujenga barabara ya njia nne kutoka katikati ya Jiji kwenda njia ya Dar es Salaam, kwenda njia ya Arusha, na pia kwenda njia ya Iringa ili kupunguza msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tumeshaanza kufanya uthamini kwa maana ya wananchi watakaopisha mradi, na tutahakikisha kwamba hatumbomolei mwanachi yeyote ambaye amefuatwa na barabara kabla hatujamlipa fidia. Kama kuna changamoto mahali popote kwenye Kata yoyote, Mheshimiwa Mbunge tunaomba tuwasiliane ili tuweze kufika na kuondoa changamoto kwa sababu ni utaratibu mwananchi yeyote anapopisha ujenzi wa barabara, anastahili kulipwa fidia, ahsante.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Kituo cha Polisi cha Chang'ombe katika Jiji la Dodoma ni moja ya vituo bora kabisa na vya kisasa ambavyo vimejengwa hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi. Hata hivyo kituo hiki kinazungukwa na makazi ya watu
waliosongamana.

Je, ni lini Serikali itajenga uzio katika kituo hiki ili kulinda
usalama wa kituo pamoja na mahabusu pamoja na polisi wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Chinyele Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye ameulizia kuhusu ujenzi wa uzio wa Kituo cha Polisi cha Chang'ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahnsate kwanza nikiri ni kweli Kituo cha Polisi cha Chang'ombe kipo kwenye mzunguko wa makazi na mimi mwenyewe binafsi katika njia zangu zisizo rasmi mara baada ya kuteuliwa tu nafasi hii nikiwa Dodoma nilikitembelea hicho bila
wenyewe hata pia kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba upo umuhimu kwa mzunguko ule wa wa makazi uliopo kwenye eneo lile na hasa kwa hali halisi ya usalama ilivyo basi kituo hicho kiweze kujengewa uzio. Nataka nimwahidi tu kwamba tuko tayari kuangalia hali ya fedha ya mwaka wa fedha 2026/2027 endapo itaruhusu na kwa sababu pia yeye ni Makamu Mwenyekiti wetu wa Kamati ya NUU kwa hiyo, nimwahidi kwamba tutajitahidi iwezekanavyo tuweze kumsaidia katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, wakazi wa Kata za Kikuyu Kusini, Mkonze pamoja na Zuzu ni miongoni mwa Watanzania waliopata bahati ya kupitiwa na reli ya SGR. Hata hivyo, iko changamoto kubwa ambayo imepelekea wakazi hawa kushindwa kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine kujitafutia riziki hasa maeneo ya mjini.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madaraja ya juu hasa zinaitwa overpass ili wakazi hawa waweze kuvuka kirahisi na hususan eneo la Michese katika Jimbo la Dodoma Mjini ambalo lina wakazi wengi sana walau wajengewe overpass moja tu waweze kupita maana sasa wanajua kutembea hadi kilometa nne ili kuvuka upande wa pili.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye ametaka kufahamu mpango wa Serikali katika kujenga madaraja ya juu, vivuko vya juu katika maeneo mbalimbali ili kusaidia wananchi wake wa Kikuyu Kusini, Michese, Mkonze, Zuzu na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza, ni Mbunge ambaye ndiyo ameingia kwa mara ya kwanza, lakini unaweza kuona jinsi ambavyo anakesha kupambana na kupigania wananchi wa jimbo lake. Kweli nampongeza sana kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wetu na hata Waziri pale huwa anamsumbua sana kila wakati anaenda pale, mara amemwambia habari za Kizota mara Zuzu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nataka pia kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza uwekaji wa madaraja au vivuko vya chini na juu vinafanywa kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni na kwa kawaida vinapangwa kabla mradi haujaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunapozungumza, kuanzia Dar es Salaam mpaka Kigoma na mpaka Mwanza tayari Serikali ilikwishatambua maeneo ambayo yanapaswa kuwekewa vivuko hivyo. Kwa kuwa ameleta hoja hii mpya, ninawaelekeza Shirika la Reli waende wakaangalie maeneo hayo na kutazama, kulinganisha na mipango iliyopo Serikalini ili kama linawezekana basi tuone namna bora ya kuweza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu pia ni changamoto, ni vigumu kusema kwamba kila palipo na watu tukaweke daraja la juu, kwa sababu ni gharama kubwa sana, lakini ushauri wake tumeupokea na ninaamini Mkurugenzi wa Shirika la Reli atakwenda kulitazama eneo hilo, na baada ya hapo chini ya maelekezo ya Mheshimiwa Waziri tutaona namna bora ya kuweza kufanyia kazi. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; visima ambavyo vimechimbwa katika Kata za Matumbulu pamoja na Mpunguzi havijafanyiwa pump test na pia havijawekewa miundombinu kwa ajili ya umwagiliaji kama mabwawa. Je, ni lini Wizara itachimba mabwawa na kuyaweka maji, ili kuwasaidia vijana katika kipindi hiki ambacho ni cha ukame?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kisima ambacho kilitakiwa kichimbwe Kata ya Mbabala katika Mtaa wa Musu hakikuchimbwa kutokana na mgogoro wa ardhi uliopo. Pia, kisima kilichochimbwa katika Mtaa wa Mapinduzi katika Kata ya Mbabala kilitoa maji kidogo sana kama vile hakukuwa na maji. Katika Mtaa wa Chisichili Kata ya Mkonze kisima kilichimbwa lakini hakikutoa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima hivyo upya, ili kuweka miundombinu na kusaidia vijana ambao kwa sasa hawafanyi kazi yoyote kwa sababu ya hali ngumu ya ukame ambayo inaukumba Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Paschal Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini kwa maswali yake mawili ya msingi. Jambo la kwanza nimthibitishie tu kwamba Serikali itafanya pump test na kuweka miundombinu katika maeneo yale, kwa sababu tumeshapokea pump za solar kutoka India ambazo tulikuwa tumeshaziagiza, na ipo katika utaratibu wa kuzisambaza. Kwa hiyo, tupo kwenye hatua za mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika yale maeneo ambayo ameyaainisha, hususan katika nneo la Mfuso ambalo kuna kisima ambacho hakikutoa maji; Serikali, moja ya jukumu tulilonalo, kama eneo maji hayapatikani, tunachimba eneo lingine ambapo maji yanapatikana. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wananchi wa eneo husika, watuoneshe eneo lingine ili tupime na tuwachimbie kisima kingine. Ahsante sana.