MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, Barabara ya Liwale - Nahoro, Liwale – Mpigamiti, Liwale – Ndapata, Liwale - Kikulyungu ni barabara zilizoharibika sana na mvua hizi zinazoendelea. Nini mpango wa Serikali kuzifanyia ukarabati barabara hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya Majimbo ambayo yamepata kipaumbele cha bajeti ya fedha za TARURA ni pamoja na Jimbo la Liwale kutokana na kuathirika kwa kiasi kikubwa na mvua, lakini barabara zake nyingi zilikuwa zimeharibika kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizo tunazitambua na tumeziweka kwenye mpango kwa ajili ya ukarabati kwa awamu. Niwahakikishie wananchi wa Jimbo la Liwale kwamba Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kupeleka fedha kwa awamu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara hizo zinapitika vizuri. (Makofi)