Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joshua Samwel Nassari (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi angalau kwa dakika mbili tatu niweze kuzungumza kwenye Wizara hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza, kwanza nitumie nafasi hii kulipongeza Bunge lako. Bunge hili la Kumi na Tatu kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu kwa siku nzima ya jana na mimi nikiwa ni Mbunge kijana ambaye niliwahi kuingia hapa ndani nikiwa Mbunge mdogo kuliko wote Tanzania, Bunge hili limeweka historia kwa kutumia siku nzima kujadili masuala ya vijana ndani ya Bunge, haijawahi kutokea tangu uhuru wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limewezekana pekee; hatuwezi kulipongeza Bunge tukaacha kumpongeza mbeba maono ambaye aliona kwamba kuna umuhimu wa nchi yetu kuwa na Wizara maalum na mahususi kwa ajili ya masuala ya maendeleo ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tumelilia kwa miaka mingi, tukaongea habari ya Baraza la Vijana, tukaongea habari ya namna gani, lakini Rais mwenyewe ameona kwamba siyo suala la Baraza tu ni habari ya kuwa na Wizara ambayo inahusika moja kwa moja na masuala ya vijana. Kwa hiyo, kwa hilo nianze kwa kulipongeza Bunge lako na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hayo maono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia habari ya vijana kwa mfano kama ambavyo tumefanya jana, we are talking of future. Tunaongea habari ya siku zijazo, miaka ijayo future ya nchi na dunia yetu hii ambayo tunaishi. Tunapozungumza habari ya future ya dunia hii, hatuwezi kuacha kuzungumzia habari ya mazingira. Mheshimiwa Kampala alikuwa anazungumza akasema kilimo kinategemea mazingira, akasema viwanda vinategemea mazingira na vitu vingine vingi alivyovitaja: siyo wanyama, siyo sisi wanadamu, siyo utalii, siyo nishati, sekta karibu zote zinategemea zinategemea mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwongezee Mheshimiwa Kampala niseme kwamba future yetu sisi, future ya nchi na future ya ulimwengu ambao tunaishi inategemea namna gani ambavyo tuta-handle mazingira yetu ya hapa duniani tunakoishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipongeze kazi kubwa ambayo imefanywa na Wizara katika suala zima la utunzaji wa mazingira na usimamizi. Kwa dakika chache ambazo umenipa na sitazitumia zote, nitajikita kwenye jambo moja tu kwa sababu mengi yamezungumzwa and I wouldn’t like to repeat yale ambayo yameshazungumzwa na Waheshimiwa Wabunge, lakini ninazungumzia sana sana ni habari ya suala la NEMC hapa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza hili la Usimamizi wa Mazingira lilianzishwa mwaka 1983. Mimi ninayezungumza hapa nilikuwa sijazaliwa, lakini Baraza lile likaanza kazi mwaka 1986. Wakati huo ndiyo ninazaliwa, lakini sheria iliyotengenezwa ya mazingira ya wakati ule na mazingira ya sasa ni tofauti. Dunia imekwenda mbele ni zaidi ya over 40 years karibu miaka 50 na kitu sasa tangu wakati ule lilipoanzishwa Baraza hili mpaka sasa hivi mazingira yamebadilika, mahitaji ya wakati yamebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati dunia nzima tunazungumza habari ya mazingira, sisi tumebaki na taasisi ambayo haina meno, haina nguvu inaitwa Baraza. Sasa jamani kule kwetu mitaani kule tunakotoka tuna Mamlaka za Miji, Miji Midogo, Halmashauri zinasimamiwa na Mabaraza ya Madiwani, halafu leo kuna habari hapa ya kitaifa ambapo dunia nzima inaongea habari ya mazingira na nini tunaitengenezea Baraza. Kwa nini hatuna Authority kwa nini tusiipe mamlaka kamili kama ambavyo tumetoa kwenye mamlaka zingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanyamapori tumewapa mamlaka kamili kutoka kuwa Idara. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maliasili na Utalii ninakumbuka ilivyokuwa. Leo ukienda TRA ni mamlaka kamili, kwa nini haikuachwa ndani ya Wizara ya fedha kwamba Wizara ya fedha ndiyo ikakusanye mapato? Ikusanye kodi ikatengenezewa mamlaka kamili? Kwa nini leo suala la mazingira ambalo ni nyeti tunalizungumza ndiyo future ya dunia yetu, lakini tuna kaweka kama ni kakitu fulani tukaatamie kakae huko chini halafu huku juu ionekane Wizara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Wizara ni habari ya kutunga sera na usimamizi wa utekelezaji wa sera, lakini siyo kazi ya Wizara tena kazi hiyo hiyo iwe ndiyo kazi hiyo kwamba ni kama ya kuatamia mpaka majukumu ambayo yanapaswa yafanywe na mamlaka zingine ambazo zinapaswa ziachwe zifanye kazi hiyo. Hivi leo ungemwona Waziri wa Fedha yuko huko mtaani anakusanya kodi anafanya nini? Unamwona afisa, Katibu Mkuu unamwona nani. Inawezekana kweli hiyo? Au umwone Waziri wa TAMISEMI yuko kule mtaani kule anasimamia, anahangaika na nini na vyoo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye ugatuzi na ndiyo maana kuna halmashauri huko chini zinafanya. Ndiyo maana kuna vijiji zina Maafisa Ardhi wake. Ukienda leo kwenye kijiji wanaweza wakakutoa ardhi mpaka ekari 50 imepewa mamlaka kamili ukienda kwenye halmashauri hali kadhalika; lakini leo hii sisi Baraza hili la kwetu, Baraza la Mawaziri limekaa wamezungumza kuhusu habari hii, lakini kila siku bado kuna mkwamo. Kiongozi wetu mkubwa kabisa wa nchi amezungumza na ametoa maelekezo na yeye akazungumza kabisa kuonesha nia ya kutaka kwamba sheria iletwe hapa, ibadilishwe ili watu hawa wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira wawe ni mamlaka kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu kwenye Muungano huu Zanzibar wana Mamlaka inaitwa ni ZEMA (Zanzibar Environmental Management Authority) sisi tumebaki hivyo. Mataifa yote yanayotuzunguka yote yanazo mamlaka kamili, sisi tumeendelea kubaki hivo kwa nini? Yaani kigugumizi ni kitu gani? Nini kinachotufanya tuendelee ku-lag behind, I don't see a reason. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa wameeleza faida ni zipi wameeleza na pros and cons …

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninaomba kabisa kabisa kwamba, leo kama alivyosema ndugu yangu Kampala na mimi niseme Mheshimiwa Waziri wetu Masauni yuko hapo asubuhi ametambulishwa na familia yake iko hapo …

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Nassari

TAARIFA

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba tu kumpatia Taarifa Mheshimiwa Mbunge mara NEMC itakapobadilishwa na kuwa mamlaka itapunguza bureaucracy na maamuzi yatafanyika kwa haraka. Ninaomba kutoa Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nassari.

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo ninaipokea kabisa kwa sababu it goes in line with what I was saying na hatuongei hapa kwa sababu kuna maslahi au namna gani tunaongea hivi kwa sababu ni ukweli ulio wazi. Kama Mkuu wa Nchi mwenyewe ameona, Baraza la Mawaziri limekaa na limeridhia, kwa nini kila linapokuja Bungeni wanasema tutaleta sheria ya Bunge hili? Tutaleta Bunge lijalo, tutafanya Bunge lijalo, kwa nini tunakwenda hatua 10 mbele, tunarudi hatua nyingi nyuma halafu tunajipongeza? Why?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii tumejadili kwa mfano tu kwenye Kamati yetu pale kuna mamlaka inaitwa TTB (Bodi ya Utalii Tanzania) ambayo kazi yake imewekwa kule ni kutangaza utalii, ni kufanya nini, lakini kwenye Kamati kule tukajikuta tunalalamika kwamba unajikuta yenyewe haipewi mamlaka kamili ya kufanya kazi hiyo wakati Rais anataka nchi yetu ifikishe watalii milioni nane. Mamlaka ile ambayo inapaswa ifanye kazi hiyo ya kutangaza inaendelea kuatamiwa, unakuta wanaotangaza ni zile taasisi TANAPA, sijui TAWA sijui nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunakwenda mbele tunarudi nyuma na hali kadhalika kwenye suala la mazingira tumeunda Baraza hili hapa, tangu miaka ya 1980 mpaka leo bado tunaliacha vilevile wakati dunia ndiyo ipo kwenye masuala ya mazingira, tunazidi kuachwa, tunazidi kubaki hapo tulipo wakati wenzetu wanapiga hatua, sisi tunarudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika hatua sasa Mheshimiwa Waziri Serikali ituletee sheria, hapa tufanye mabadiliko watu wa NEMC wapate mamlaka kamili ili waweze kufanya kazi kulingana na mandate ambayo itakuwa itatengenezwa na sheria husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono ahsante sana. (Makofi)