Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joshua Samwel Nassari (1 total)

MHE. JOSHUA S. NASSARI aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa fedha, ili kukamilisha miradi mikubwa ya maji, Meru, iliyosimama, ili kuondoa shida kubwa ya maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joshua Samwel Nassari, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama Ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi nane ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 10.1 katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mkoani Arusha. Kati ya miradi hiyo, miradi mikubwa miwili ya Kikatiti – Samaria na mradi wa Kata ya Uwiro, kwa pamoja inagharimu jumla ya shilingi bilioni 8.3, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 1.9 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Shilingi bilioni 6.4 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo mikubwa kwa pamoja imefikia wastani wa 40% za utekelezaji, ambapo inahusisha ujenzi wa dakio, ujenzi wa matanki matano yenye ujazo wa lita 1,800,000, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 69.04 sanjari na ujenzi wa vituo 37 vya kuchotea maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha kupeleka fedha za utekelezaji wa Miradi ya Kikatiti – Samaria na ule wa Kata ya Uwiro kulingana na hati za madai zinazowasilishwa na Wakandarasi ili iweze kukamilika na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.