Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema kuniwezesha siku ya leo kuweza kusimama hapa katika Bunge lako hili Tukufu niweze kuongea machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu. Ni ukweli usiopingika, Mheshimiwa Rais wetu anaibadilisha Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuijua Tanzania ilivyokuwa miaka 10 kwenda nyuma, na leo, tuna mabadiliko makubwa sana. Huo ni ukweli na utaendelea kuwa ukweli na utakuwa ukweli ukweli ukweli. Tanzania imebadilika na aliyeibadilisha ni Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa vile ni mara ya kwanza napenda nikipongeze chama change, Chama cha Mapinduzi na kukishukuru, kuanzia ngazi ya Taifa, mkoa, wilaya, kata, tawi mpaka kwenye mashina pamoja na wale Wajumbe wa Mashina kwa kuniwezesha kunipa kura nyingi za kishindo, lakini chama changu ngazi ya Taifa kikaweza kunichagua kuwa mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakishukuru sana Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini na mimi nawaambia kama chama, sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba niwashukuru wapigakura wangu wote wa Jimbo la Temeke, hakika walinipa ushindi wa kishindo, ushindi uliotukuka. Kipekee napenda niwashukuru na kuwapongeza wale wote wagombea wenzangu 17 kutoka vyama mbalimbali katika Jimbo la Temeke kwa kuniunga mkono na kunisaidia baada ya kumaliza uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo moyo wa kizalendo. Ninawashukuru sana vyama vyote, tuko pamoja tunajenga pamoja Temeke yetu na ninawaambia karibuni sana katika Ofisi ya Mbunge Jimbo la Temeke muweze kutoa maoni yenu, kuleta yale ambayo mliyakusudia wakati mnagombea. Sasa mimi ndiye niliyapata Ubunge, karibuni tushirikiane tuijenge Temeke yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninawashukuru na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa kuteuliwa kwake, na kwa kuwasilisha vizuri sana hotuba yake ya bajeti ya mwaka huu 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote walioteuliwa na waliochaguliwa, wanafanya kazi nzuri. Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu na watendaji wote wa Serikali. Hakika katika kipindi hiki kifupi wameweza kutupa ushirikiano wa kutosha kabisa. Tunashukuru sana, endeleeni kuchapa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa siku ya leo, nitajikita katika Wizara mbili; Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano na TAMISEMI. Katika Wizara ya Ajira na Mahusiano, ninampongeza sana Mwenyekiti wangu wa Kamati, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wenzangu wa Kamati hiyo. Hakika Wizara hii imefanya kazi kubwa sana, tumeona miradi yao, tumeona mambo mbalimbali ambayo walipanga kuyafanya katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika wanafanya kazi nzuri sana. Mimi nitaingia kwenye maoni ya Kamati yetu. Tumeielekeza Serikali kwamba wafike sehemu waangalie jinsi ya kuongeza fedha katika ile project ya uanagenzi. Project ile ni muhimu sana kwa maendeleo ya kijana, ukizingatia Taifa letu sasa hivi tumelimbikwa na ukosefu wa ajira, Serikali haiwezi ikaajiri watu wote na sekta binafsi haiwezi ikajiri watu wote. Hivyo, mpango wa Serikali wa kuamua sasa kuwapeleka vijana katika mafunzo ya uanagenzi baadaye wakimaliza, waweze kujiwezesha wenyewe kwa kufanya shughuli mbalimbali za kuwaongezea kipato, ni mpango mzuri sana sana sana na changamoto iliyopo ni ukosefu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Serikali wawaongezee fedha kwa sababu ukiangalia bajeti, mwaka 2023/2024 walitakiwa wapewe shilingi 119,641,000,000 lakini kiasi walichopewa ni shilingi bilioni tisa. Ni kiwango kidogo sana. Najua hakuna kidogo, hata kidogo ni kikubwa, lakini kwa jinsi inavyoonekana na mwitikio wa vijana kwenda kujiunga kwenye hizo kozi, bado fedha zile hazitoshelezi. Tunaomba Serikali wawape fedha waweze kuendeleza hiyo kozi za uanagenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye mwaka 2024/2025 walitakiwa wapewe shilingi 77,000,858,000, lakini kiasi walichopata ni shilingi 10,800,000,000, bado ni kiwango kidogo. Ninaiomba Serikali katika bajeti hii, waangalie namna gani wanaweza wakaongeza bajeti hiyo kuwasaidia vijana. Sambamba na hilo, naomba utaratibu mzima wa kuwapata hao vijana uanagenzi uangaliwe upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninatoka Temeke na nimehudumu katika Kamati hiyo awamu iliyopita na awamu hii. Nimezunguka katika vyuo mbalimbali vya uanagenzi, sikuwahi kumwona hata mtoto mmoja aliyetoka Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, fursa hii lazima tugawane sawa. Fursa hiyo ya uanagenzi na kama itawezekana irudishwe kwenye halmashauri zetu tuone hapa Halmashauri ya Temeke waliokwenda kwenye mafunzo ya uanagenzi kutoka kwenye Mfuko wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni 20, Halmashauri ya Ubungo wamekwenda 20 na nyingine. Tukienda hivi nafikiri kila mmoja na kila kijana atafaidika na keki ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwenye suala zima la uanagenzi, lakini pia kwenye hiyo kodi ya SDL ambayo wanakatwa wafanyakazi katika sekta binafsi pia waangalie kwa sababu sekta binafsi ndio uti wa mgongo wa Taifa letu. Wao wanabeba watu wengi zaidi katika ajira zetu kuliko Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo sekta binafsi iangaliwe kwa sababu wao wanao wafanyakazi, lakini wale walioko viwandani na wao kama binadamu fungu hili zamani kabla halijaingizwa kwenye uanagenzi kupelekwa kwenye vyuo vikuu na maeneo mengine, lilikuwa linawasaidia wafanyakazi wa sekta binafsi na wao wakapate angalau refresher course ya zile kazi zao wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mpango ule ule tuhakikishe kama kuna viwanda viko katika eneo husika basi na wao watoe hata wawili au watatu waingie kwenye zile kozi kujiongezea ujuzi. Mtu akienda pale, kama alienda mbeba mizigo, hapana afike sehemu awe hata fundi bomba. Afike sehemu; ndiyo namna mwananchi wetu wa Kitanzania na yeye anaweza akapata promotion akiwa katika sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Wizara ya TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri na timu yake wanafanya kazi nzuri sana, lakini pamoja na kazi nzuri, bado kuna limbiko la watu maeneo fulani. Katika Jimbo langu la Temeke kwa mujibu wa sensa, nina takribani watu 570,000, lakini ninaishukuru TAMISEMI imejenga shule za sekondari katika kata zote, bado kata moja ambayo shule bado inajengwa, lakini hata hivyo haiwatoshelezi vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Shule ya Sekondari ya Buza ina watoto 1,889. Shule moja ina vyumba vya madarasa 14. Vyumba vinne vinavuja nyang’anyang’a kabisa. Mvua ikinyesha watoto hawawezi kusoma madarasani, hiyo ni changamoto tuangalie katika bajeti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Serikali, ilikwenda kwenye vile vyuo, shule za sekondari chakavu za muda mrefu, project hiyo imefanya vizuri sana. Sasa ije na mpango wa awamu ya pili ya kuboresha majengo na shule chakavu ili sasa vijana wetu waweze kusoma vizuri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, muda wako umeisha.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, lakini ninaomba pia kwenye sekta ya afya, nina Zahanati ya Sandari bado na Zahanati ya Kata ya Temeke. Kata ya Temeke ni kata mama, ilikuwa inategemea hospitali ya Temeke, lakini ile imekuwa ya rufaa, tunatakiwa tuanzishe hospitali. Ninaomba sana Serikali waangalie jinsi gani ya kupata zahanati au kituo cha afya katika Kata ya Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)