MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa watumishi wetu, vijana wetu wanajitolea katika sekta ya afya pamoja na elimu wanapotuma maombi huwa wanaambatanisha ile barua ya taasisi ambayo walikuwa wanajitolea, kwa nini hawapewi kipaumbele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kueleza kwenye swali letu la msingi, kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma kwamba ajira zote kwa sasa zinatolewa kwa njia ya ushindani ili kutenda haki kwa watu wote, ili kupata usawa, hivyo basi, msisitizo unaendelea kuwekwa kwamba vijana wanapopata nafasi ya kujitolea, wajitolee ili kujijengea uzoefu na wapate ujuzi na maarifa ili yale waliyoyapata darasani waende kuyatumia katika vitendo na mwisho linapotokea suala la ajira basi washiriki katika ushindani ili waweze kuajiriwa Serikalini.