Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa aliyofanya katika Mkoa wa Shinyanga. Ameweza kutujengea hospitali kubwa kuanzia mkoa hadi kwenye ngazi ya wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunavyoongea kwa sasa hivi Mheshimiwa Rais ameweza kuidhinisha fedha za kujenga maabara kubwa ya kisasa katika hospitali yetu ya rufaa pamoja na wodi ya mama na mtoto. Hiyo ni hatua kubwa sana sana kwa Mkoa wetu wa Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninapenda kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Hili jambo alilokuja nalo la Bima ya Afya kwa Wote, sisi kama Wabunge nina imani tunaenda kushikamana kwa pamoja kuitangaza bima hii ya afya. Tutahakikisha wananchi wanajiunga kwa wingi, maana kwa hali ya kawaida mgonjwa anapoenda hospitali kupata huduma ya cash, ni gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alisema hapa Bungeni, nitakapomaliza kipindi change, ninatamani kumwona kila mwananchi akiwa na tabasamu kwenye uso wake. Hili linaenda kumfanya mwananchi anakuwa na tabasamu kwenye uso wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake pamoja na Mganga wetu Mkuu. Jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Ni wachapa kazi na wamekuwa rahisi kufikika. Licha ya uchapakazi wao, sisi Mkoa wa Shinyanga bado tuna changamoto katika magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kuongelea ugonjwa wa figo, ugonjwa huu umekuwa ni tatizo, lakini kwa Mkoa wetu wa Shinyanga hatuna mashine za dialysis. Ninakupa mfano, mtu ambaye anatoka Jimbo la Ushetu, Ubagwe atalazimika kutembea kilomita 300 mpaka 400 kwenda kuifuata huduma hii ya figo ya kusafishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kupelekea baadhi ya watu ambao wanauguza watu hawa kwenda kufilisika kiuchumi kwa sababu ukiangalia huduma hii kwa wiki, anafanya mara tatu, na kwa Mkoa wa Shinyanga hakuna. Hawezi kwenda akatembea kilomita 300, 400 kuifuata huduma hii Mwanza na baada ya siku mbili, tena atarudi na mkoa wetu hauna huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilielekeza vyema kwamba, itahakikisha inashusha huduma ya afya katika kila mkoa, huduma bora. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, mtu anayeumwa figo huyo huyo anaweza akaumwa kisukari, huyo huyo anaweza akaumwa pressure. Pia, magonjwa haya yote yanaambatana kwa pamoja, na sasa hivi, hili limeshakuwa ni janga, watu wanaumwa magonjwa yasiyoambukiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara inatakiwa kwa sasa hivi ipambane kutoa matamko kuelimisha watu namna bora ya kuweza kujikinga na magonjwa haya. Maana lifestyle ya maisha inatupelekea kwenda kupata magonjwa haya yasiyoambukiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata watoto wadogo sasa hivi wamekuwa wakipata magonjwa haya yasiyoambukiza. Kama iliwezekana katika Virusi vya UKIMWI kufanya matangazo mara kwa mara, hata haya magonjwa yasiyoambukizwa ni wakati sasa hivi kuweza kuweka matangazo ya kutosha na elimu ya kutosha, kwa sababu hata mfuko huu wa bima ya afya tutakapokuwa nao pia utatulazimu kutumia gharama nyingi sana kwa hawa watu ambao watakuwa wanaumwa magonjwa haya ya figo na cancer. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri na ninategemea kwa sababu tuna zahanati zetu hata za kata huwezi ukakuta hili tangazo la jinsi ambavyo unaweza ukajilinda, ukajikinga usipate magonjwa haya yasiyoambukiza. Ninajua nia ya dhati ya Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais kuhakikisha tunajenga Muhimbili mpya ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojenga Muhimbili mpya ya kisasa bado tutahitajika tuwekeze pia katika hospitali za rufaa, hospitali za kikanda ili kuipunguzia mzigo Muhimbili. Pia, kituo cha dialysis kwa Mkoa wa Shinyanga ni milioni 300 tu. Ninaomba tuidhinishiwe hizi fedha, kwa sababu takribani kwa mwaka wagonjwa 300 wanasafiri kwenda kupata huduma hii kwenye mikoa ya jirani. Ahsante sana. (Makofi)