Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Florence George Samizi (1 total)

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kulijali kundi hili la watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, tunaona kuwa, katika siku za kwanza 100 za uongozi wake amewezesha kundi hili la watu wenye ulemavu kuwa kwenye huu mpango mzima wa Bima ya Afya kwa Wote. Pamoja na haya mazuri, ninaiomba Serikali iendelee kuwatambua watu wenye ulemavu wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ili waendelee kunufaika na mpango huu.

Mheshimiwa Spika, pia, ninaiomba Serikali, majibu haya mazuri ambayo yameongelewa hapa kuwe kuna utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake kwa sababu huku site hali siyo nzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuwe kuna ufuatiliaji wa haya ambayo yamezungumzwa ili sasa kundi hili la watu wenye ulemavu na hasa hawa wagonjwa wa akili waweze kupata hizi dawa kwa wakati kwa sababu wasipozipata kwa wakati, wanafanya mambo ambayo yanakuwa hayana staha katika jamii yetu. Vilevile, wanashidwa kuendesha maisha yao kwa maana ya kushindwa kufanya kazi za msingi za kimaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mheshimiwa Naibu Waziri apange muda ili sasa aweze kukutana na kundi hili na aweze kusikia kutoka kwao wao wenyewe, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimeupokea ushauri.