Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deodatus Philip Mwanyika (2 total)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-
Je, kwa nini, Serikali isianzishe eneo mahsusi la viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya misitu litakalohudumia masoko mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa sekta ya mazao ya misitu katika kukuza uchumi wa nchi, kuongeza thamani ya mazao, kuchangia upatikanaji wa ajira, pamoja na kuchangia katika pato la Taifa. Mkoa wa Njombe, Serikali ina mkakati wa kuanzisha eneo maalum la kiuchumi litakalovutia uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani mazao ya misitu pamoja na mazao mengine ya kimkakati ikiwemo parachichi. Hatua mbalimbali tayari zimeanza kuchukuliwa, ikiwemo uchambuzi na utambuzi na upatikanaji wa maeneo ya ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, Serikali kupitia TISEZA inaendelea kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa ya Tanzania Bara, katika kuhamaisha utengaji wa maeneo mahsusi kwa ajili ya kuanzisha kongani za viwanda, ikiwemo viwanda vya kuongeza thamani mazao ya misitu siyo tu kwa Mkoa wa Njombe na hata Mikoa mingine kama Iringa, Katavi na Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa maji kwenye Mji Mdogo wa Kifanya katika Kata ya Kifanya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ya maji nchini unakamilika ili kuweza kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wake. Mradi wa maji kwa ajili ya kuhudumia miji Mji Mdogo wa Kifanya uliopo Wilaya ya Njombe umefanyiwa usanifu na kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa kazi zinazotarajiwa kutekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa kidakio (intake), ujenzi wa tanki la chini (sump well) ujazo wa lita 100,000 pamoja na tanki la kuhifadhia maji lita 300,000 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji vitano. Mradi unalenga kunufaisha zaidi ya wakazi 5,484 waishio kwenye Mji Mdogo wa Kifanya uliopo katika Wilaya ya Njombe Mkoani Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuanza utekelezaji wa mradi huo unaotarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.638.