Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninaanza kwa kuunga mkono hoja, lakini kubwa nimepata wasaa wa kuisoma Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ninasema bajeti imepangwa na imepangika, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepata nafasi ya kufanya ziara na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimeshiriki takribani mikoa nane katika ziara yake na kwa kushiriki hiyo ziara nikiwa kama kiongozi kijana kuna mengi ambayo nimejifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo nimejifunza ni kwamba, uongozi siyo cheo, uongozi ni matokeo, uongozi ni vitendo. Unapokuwa kiongozi unatakiwa uwe faraja, unapokuwa kiongozi unatakiwa uwe mtatuzi na unapokuwa kiongozi unatakiwa uwe kimbilio. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipohutubia katika hili Bunge amesema anataka kuacha faraja kwa Watanzania. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maeneo yote alipofanya ziara ameacha faraja kwa Watanzania, ambayo imewekwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika upande wangu wa maji, ninakumbuka tulipata crisis ya maji Dar es Salaam, viongozi wetu wakuu hawakutuacha, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika mpaka kwenye chanzo kule Ruvu Chini kuona hali halisi. Tulimweleza moja ya changamoto yetu, pamoja na hii crisis tunayopitia, ni pump.
Mheshimiwa Spika, ninataka nimweleze Mheshimiwa Waziri Mkuu, muda mfupi tangu amefanya ziara tumepokea zaidi ya pump nne, kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam. Hakwenda pale akaona suluhu ambayo inafanywa na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, juu ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda ambalo miaka yote limekuwa kwenye karatasi, akasema ninaomba nikajionee kazi ambayo inafanyika. Tumefika Kidunda, pamoja na mazingira yenye changamoto, lakini amefika huku mvua ikiwa inanyesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, amefika pale, moja ya changamoto kubwa tuliyokutana nayo ni mkandarasi anadai certificate ya zaidi ya shilingi 24,000,000,000. Ametoa maelekezo kwamba, tunapoangalia suala la maji hatuangalii gharama, Wizara ya Fedha ndani ya wiki moja shilingi 24,000,000,000 zitolewe. Ninaeleza shilingi 24,000,000,000 zote zimetolewa, huyu ndiye Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekwenda Mwanza. Tunajua pale Mwanza kuna mradi, kwa ajili ya kuhakikisha Wanajiji la Mwanza wanapata huduma ya maji safi na salama. Mradi wa Butimba umekamilika, sasa hivi tunakwenda kwenye usambazaji, mahitaji yamekuwa makubwa, tumeamua tuongeze extension, kwa ajili ya Mradi wa Capripoint. Moja ya changamoto kubwa ni suala la advance payment; Mheshimiwa Waziri Mkuu ziara aliyoifanya ameondoka ametoa maelekezo, tumetoa shilingi bilioni 4.5. Hiyo ni kazi ambayo imefanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda Tunduma maeneo ambayo yalikuwa na changamoto kwa muda mrefu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 amesema pale tupeleke mradi wa maji. Tumesaini mradi wa shilingi 119,000,000,000, mradi ambao unajengwa kwa fedha za ndani. Moja ya changamoto ambayo tulikuwa tukiipata ni suala la advance payment juu ya uanzaji wa mradi ule. Ninasema, Waheshimiwa Wabunge, ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tumekwenda na kwa muda mfupi tumepata shilingi 5,000,000,000, leo mkandarasi amelipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nini maana yangu? Ninachotaka kusema mbele ya Waheshimiwa Wabunge ni kuna mwanga chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Ninataka nimtie moyo, ukisoma Ezra inasema, inuka hii shughuli inakuhusu na ukaitende kwa moyo mkuu. Sisi wasaidizi wake tupo pamoja naye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, pamoja na mafunzo yote ambayo tumeyapitia, lakini funzo kubwa ambalo nimejifunza ni suala la uwajibikaji. Waheshimiwa Wabunge wote kila aliyesimama amezungumza suala la uwajibikaji, huko chini mpaka juu mifumo ipo, suala la operation, ni kwamba watu kuanzia chini wafanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha Watanzania wanapata matokeo na wanaachiwa tabasamu. Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na maelekezo makubwa halali usingizi, anafanya ziara mpaka kule chini kabisa, ninataka niwaambie tumtie moyo. Ukisoma maandiko yanasema, Zaburi ya 11:3, misingi ikiharibika mwenye haki atafanya nini?
Mheshimiwa Spika, anachofanya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ni kusimamia misingi. Watendaji kule chini wafanye kazi, ili Watanzania maskini waweze kupata maendeleo, wapate haki ambayo anaipigania Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninataka nimwambie, wapo baadhi ya watu wanaweza wasimwelewe, lakini muda utasema, watamwelewa kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Waziri Mkuu, chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wangu wa maji ninataka niseme, pamoja na mazuri ambayo amefanya Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati unamsifia ni sawa na kusifia chakula kwenye meza, basi ni lazima kunakuwa na wale wapikaji ambao wamepika, wameungua vidole. Ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote ambao wanafanya kazi chini ya Waziri Mkuu, wanamsaidia kwa vitendo; Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurungezi na wengine wote huko chini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, moja ya jukumu kubwa la Bunge ni kuisimamia Serikali. Tuisaidie Serikali yetu, tuishauri kwa upendo, ili kuhakikisha inatimiza wajibu ili Watanzania waweze kupata huduma hii kubwa na maendeleo kwa kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wetu wa maji, hoja kubwa ambazo zimeelekezwa katika Wizara yetu ya Maji ni madeni ya wakandarasi. Jambo lingine ambalo limeelezwa ni juu ya ukamilishaji wa miradi ya maji. Ninawaambia Waheshimiwa Wabunge sisi katika Wizara yetu ya Maji kulikuwa na madeni, Serikali imekaa na Kamati ya Bajeti ikaweka commitment, ninasema commitment ambayo imetolewa haijazidi wiki, Wizara ya Maji tumepokea shilingi 40,000,000,000 kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawaambia wakandarasi fedha tumeanza kuzilipa, waende wakafanye kazi, mkandarasi atakayezingua, tutazinguana. Biashara tumalize mchana kweupe kwa sababu, hawana kisingizio, fedha zimetolewa. Kwa hiyo, sisi tunachofanya ni kusimamia kuhakikisha malengo na dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua miradi ambayo inaendelea ni 1,000; miradi 867 inaendelea vijijini na mingine ni mjini. Ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, hii ni bajeti yetu ya kwanza, tumeweka msimamo, sisi kama Wizara ya Maji, tuna miaka mitano na kurudi kwenu katika Bunge ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Nikiwa kama kiongozi wa Wizara ya Maji hatutalala usingizi. Moja ya agenda yetu katika Bunge hili ni miradi yote ile ambayo tumeianza tunataka tuikamilishe ili kuhakikisha wananchi katika maeneo yao, wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine la msingi ambalo limepata dhamana na Mheshimiwa Rais kwa mara nyingine kuwa kiongozi katika Wizara yetu ya Maji, Menejimenti ya Wizara ya Maji tumefanya tathmini ya Wizara yetu ya Maji, ukitaka ujue unapokwenda lazima ujue wapi ulipotoka. Yapo maeneo tumefanya vizuri kama Wizara, lakini yapo maeneo yamekuwa yana changamoto.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi kama Wizara katika tathmini ambayo tumeifanya na kwa kuangalia Dira 2050 tumeona, ili twende katika Dira 2050 lazima tuwekeze kwa watendaji wetu, tufanye katika human capital, tuwekeze kwa maana human capacity, tuwajengee uwezo watendaji wetu. Tunataka watendaji ambao wanasema inawezekana, tunataka watendaji ambao wataleta matokeo na siyo visingizio. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamekuja kuibana Serikali wanataka matokeo, Watanzania wanataka maji, jukumu la Waziri wa Maji, faraja yetu ni watu wapate maji, tutasimamia wataalam wetu kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, sisi kama Wizara ya Maji tumejiwekea malengo ni mifumo na teknolojia zitumike kufanya mageuzi juu ya utendaji katika Wizara yetu ya Maji. Kwa dunia ya sasa kumwona mwananchi analalamika amebambikiziwa bili ya maji huo ni ushamba, hizo ni zilipendwa. Leo dunia ya sasa uone wananchi wanalalamika upotevu wa maji, hali mwananchi hana maji, haiwezekani! Tumetoa maelekezo kwa Wizara ya Maji tutumie private sector, tushirikiane nao, tutumie teknolojia kwa ajili ya kufanya mageuzi ndani ya sekta ya maji.
Mheshimiwa Spika, eneo la mita tunakwenda kwenye pre- paid meter, mwananchi anataka maji ya elfu tano atanunua ya elfu tano, yakiisha ataongeza bila kubambikiwa bili ya maji. Suala la ubambikizaji, suala la upotevu wa maji tumetumia Chuo chetu cha Maji, tumekuja na mfumo tunaamini tutakwenda nao ili kuondokana na malalamiko ambayo hayana ulazima.
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, ni suala zima la alternative financing. Tukisema tuitegemee Serikali sisi tumefanya tathmini, Tanzania kuna vijiji takriban 12,300. Mpaka sasa kupitia Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeshafika zaidi ya vijiji 10,000 tumebakisha vijiji 1,575 tu.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, malizia.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba vijiji 1,575 ambavyo vimebakia tumepewa maelekezo na Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi hiki cha miaka mitano, vijiji vyote tuweze kuvikamilisha ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, mwisho, nchi yetu ya Tanzania si maskini wa vyanzo vya maji, tunalo Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuwa tunakwenda kwenye Dira ya 2050, tuitoe Wizara ya Maji kuwa Wizara ya Maji ya kunywa iwe Wizara ya kiuchumi, twende kwenye umwagiliaji. Tunakwenda kutumia National Water Grid ili kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Special Address by His Excellency Hon. William Samoei Ruto, PhD, C.G.H., President of the Republic of Kenya and Commander-In-Chief of the Defence Forces, to the Parliament of the United Republic of Tanzania
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, moyo usiyokuwa na shukurani hukausha yaliyo mema yote. (Makofi)
Kwa dhati ya moyo, umenipa nafasi hii kutoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Tanga. Nimshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa moyo wake na upendo wake wa kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Samoei Ruto. Amezungumza mara nyingi sisi kwa wasaidizi wake kwamba Dkt. William Samoei Ruto ni kaka yake, na sisi kama wasaidizi wake, ametusisitiza mara kwa mara kufanya kazi kwa umoja na mshikamano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninataka nikuhakikishie Mheshimiwa Rais Dkt. William Samoei Ruto, mimi ni Waziri wa Maji ambaye nimepewa dhamana. Tunafanya kazi kwa ukaribu na Mheshimiwa Engineer Eric Mugaa, ambaye ni Waziri wako wa Maji na Umwagiliaji wa Jamhuri ya Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, dunia ya sasa inataka viongozi watakaoleta matokeo, na Baba wa Taifa aliwahi kusema uongozi siyo cheo, uongozi ni matokeo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Dkt. William Ruto, hawa ni viongozi wetu wa matokeo. Tuwapigie makofi mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Imam Shafii aliwahi kusema, nyoyo za binadamu zinaongeza mapenzi makubwa hasa kwa viongozi ambao wanatenda mambo yaliyo mema kwa watu wao. Kwa haya ambayo amezungumza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Kenya pamoja na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakika wataendelea kukumbukwa na kukumbukwa na kubaki katika historia kwa matendo mema ambayo wanawatendea hasa Watanzania pamoja na Jamhuri ya Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nimetokea Tanga, Mji wa Tanga tumekuwa tukitangatanga hasa katika maendeleo, lakini leo umezungumza hapa hakuna suala la ubinafsi katika maendeleo. Umesema refinery ikajengwe Tanga. Mungu atakubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninataka nikuhakikishie, tukiwa kama viongozi wa Mkoa wa Tanga, tumeupokea mradi huu wa kimkakati kwa umoja na mshikamano na wala hatutotangatanga. Tutaleta ushirikiano, tuna Mkuu wa Mkoa mzuri na tuna viongozi wazuri. Pamoja na Mheshimiwa Rais wetu na maelekezo ambayo atakayoyatoa, tutahakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na manufaa yanakuwa makubwa kwa Watanzania na Wakenya, pamoja na nchi hizi za Maziwa Makuu na wenzetu wa Uganda. (Makofi)
Mheshimiwa Rais, mimi sina maneno mengi sana ya kusema, ila kikubwa ukipata viongozi ambao wanawazia mema Watanzania pamoja na Wakenya, ni jambo kubwa. Mungu awabariki sana na Mungu atawalipa katika safari zenu. Ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)