MHE. ASHA OMAR RASHID aliuliza:-
Je, lini Serikali itaongeza idadi ya Madaktari katika Hospitali za Wilaya ili kuboresha Huduma za Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Omar Rashid, Mbunge wa Viti Maalum, akitokea Kaskazini Pemba lakini pia huyu ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga bajeti na kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya nchini. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2025/2026 jumla ya watumishi wa kada mbalimbali za afya 37,921 wameajiriwa. Wataalamu hao ni pamoja na madaktari (MD - Medical Doctors) 1,985 pamoja na kada nyingine 35,936. Aidha, zaidi ya 55% ya watumishi hawa wamepangwa katika hospitali za Halmashauri kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imeajiri watumishi 5,000 wa kada mbalimbali za afya ambapo watumishi 134 ni madaktari ambao wamepangiwa kutoa huduma kwenye Hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma za upasuaji wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti na kuajiri Madaktari na kuwapanga katika hospitali zenye upungufu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ASHA OMAR RASHID aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatafutia masoko ya Mwani Wakulima wa Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara kujibu swali Na. 12 kutoka kwa Mheshimiwa Asha Omar Rashid, Mbunge wa Viti Maalum, Kaskazini Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia upatikanaji wa soko la uhakika, Serikali imeweka mkakati mahsusi wa kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mwani. Mkakati huo unajumuisha kufanya tafiti kuhusiana na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya bidhaa za mwani, kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima na wanunuzi, pamoja na kutekeleza programu za kujenga uwezo ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango na mahitaji ya masoko ya Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira pamoja na TANTRADE, tutafanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya masuala haya ya kupata masoko ya uhakika ya zao la mwani. Ninaomba kuwasilisha.