Supplementary Questions from Hon. Asha Omar Rashid (3 total)
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninashukuru kwa kunipatia fursa hii nami kuuliza swali langu la nyongeza. Pale Mkoani kwangu Kaskazini Pemba pana Kituo cha Polisi cha muda mrefu. Kituo kile kilizinduliwa tarehe 25 Juni, 1979. Kwa kuongezeka wananchi katika Mkoa ule wa Kaskazini Pemba. Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi katika Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na jengo la RPC wa Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Asha Omar, Mbunge wa Viti Maalum, Kaskazini Pemba, kwa swali lake zuri; na nimpongeze sana kwa kuwa karibu sana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi na kubaini pia changamoto zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleza katika majibu yangu ya msingi wakati nikijibu wiki iliyopita, kwamba kwa upande wa ujenzi wa vituo vya polisi vya mkoa tulikuwa tunakiri kwamba tuna mikoa mitano ambayo ilikuwa haina vituo vya polisi; lakini kwa upande wake alikuwa anaongelea zaidi kuhakikisha kwamba anafanya ukarabati wa jengo la RPC katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambalo hilo nalo lipo kwenye mpango wa ukarabati kama ambavyo tunaendelea nao. Kwa sasa tuna miradi 56 ya ukarabati nchi nzima katika ngazi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo ninaamini kwamba tukienda kwenye hatua ya pili ya mpango wa kukarabati jengo hilo nalo litaingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa yale majengo mawili ya wilaya kwa maana Wilaya ya Wete na Wilaya ya Michiweni Kaskazini Pemba nayo yapo kwenye majengo 75 ambayo kwa sasa ama yapo kwenye hatua ya ukarabati ama ujenzi upya kwa wilaya zetu 75 za nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Jeshi la Polisi tupo kwenye hatua ya kukamilisha mpango mkakati wa miaka mitano ijayo. Wakati tukiendelea na hatua hiyo, tunaendelea vilevile kutathmini hali ya majengo ya vituo vya polisi, makazi ya askari na maeneo mengine yakiwemo hospitali na majengo ya mazoezi ya vikosi vyetu vya Field Force na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue, wapo Wabunge wengi ambao wamehitaji ama kujengewa ama kufanyiwa ukarabati vituo vya polisi. Kwa ruhusa yako ninaomba niwatambue Mheshimiwa Florence George Samizi, Mheshimiwa wa Kigoma, Mheshimiwa Joseph Copriano Isack au Kadogo wa Monduli wamehitaji hilo, ninatambua pia hitaji lake, Mheshimiwa Anne Kilango Malacela naye na nimemwahidi nitakwenda pia kwenye eneo lake, pamoja na Mheshimiwa Ester Bulaya naye pia alihitaji pale Bunda Mjini, naye nimemwahidi pia nitakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi niulize swali la nyongeza. Ninaishukuru sana Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kutujengea Kituo cha Polisi pale Matangatuani, lakini pale bado hatuna makazi ya Polisi. Je, ni lini Serikali itajenga makazi bora ya nyumba za Polisi pale Matangatuani Wilaya ya Micheweni Pemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, makazi ya Askari yanaendelea kujengwa hivi sasa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Kaskazini Pemba. Eneo la Matangatuani lipo kwenye mpango. Sasa, kwamba ni lini, itategemea na hali ya upatikanaji wa fedha ili tuweze kukamilisha ujenzi na pia kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa maswali mazuri ya Serikali. Pia, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suhulu Hassan, kipenzi chetu, kwa kutoa ajira 500 za madaktari Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nataka kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya madaktari katika vituo vya kutolea huduma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili. Je, Serikali imejipangaje kuwapatia semina elekezi madaktari na watoa huduma, ili waweze kutumia lugha iliyo fasaha hasa wakati wakipokea wakina mama wakienda kujifungua hospitalini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Asha Omar kwa kuuliza maswali ambayo yanagusa jamii yetu, wakina mama wetu, na watumishi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kujali maslahi ya watumishi wetu kote nchini. Katika mwaka wa fedha 2025/2026 na 2026/2027 tumetenga jumla ya shilingi bilioni 13 kwa ajili ya kulipa on calls, yaani madaktari wanapoitwa kazini, kwenda kufanya kazi zao za dharura. Pia, zimetengwa shilingi bilioni 10 za kulipa stahiki zao za likizo. Vilevile, tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya kulipa stahiki zao za uhamisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ninaomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya, tumeendelea kushirikiana kutoa miongozo na tumekuwa tukisisitiza sana madaktari wetu watoa huduma kuendelea kutoa lugha za staha, lugha za mawasiliano bora kazini, ili kuweza kuwahudumia wananchi wetu, kuwahudumia mama zetu, hasa wale wajawazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akituelekeza sana katika hili, kuendelea kuwa wazalendo na kuwatibu kwa lugha stahiki wagonjwa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)