MHE. MARIAM A. MUNGULA K.n.y. MHE. ASHA R. BARAKA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaunda Tume itakayotatua migogoro ya ardhi nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ninaomba kujibu swali Na. Nane la Mheshimiwa Asha Ramadhani Baraka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi, kufuatia hali hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliekeleza Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kuandaa mapendekezo yatakayowezesha kupata suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na taasisi zilizobainishwa, imeandaa rasimu ya mkakati wa utambuzi wa migogoro ya ardhi nchini, utekelezaji wa mkakati huo utahusisha wadau wote muhimu katika utatuzi na udhibiti wa migogoro ya ardhi. Aidha, mkakati huo utakuwa na kanzidata moja ya migogoro ya ardhi, hivyo kuimarisha uelewa, uwazi, uwajibikaji na kasi katika kushughulikia migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile utekelezaji wa mkakati utaimarisha amani, umoja na mshikamano katika jamii hivyo kuboresha mazingira ya uwekezaji katika ardhi na kukuza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.