Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Zacharia Paulo Issaay (2 total)

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ambao umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania imeendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa majengo ya Mahakama kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya utoaji haki katika ngazi mbalimbali. Mpango huu unahusisha ujenzi wa majengo mapya pamoja na ukarabati wa majengo yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mpango huo, ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ulianza katika mwaka wa fedha 2024/2025. Hata hivyo, mradi huo umechelewa kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake. Tayari changamoto hizo zimetatuliwa na ujenzi wa jengo hilo unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2026.
MHE. CECILIA D. PARESSO K.n.y. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutekeleza Mradi wa Maji wa Kimkakati wa Tsoray katika Tarafa ya Nambis - Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado inaendelea na utafutaji wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 70.1 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa maji wa kimkakati wa Tsoray uliopo Tarafa ya Nambis, Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara. Miongoni mwa kazi zinazotarajiwa kutekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 13.6 kwa siku, ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house), ununuzi na ufungaji wa pampu nne za kusukuma maji, sanjali na ujenzi wa vituo 160 vya kuchotea maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo unalenga kunufaisha zaidi ya wananchi 109,228 wa Wilaya ya Mbulu.