Answers to Primary Questions by Hon. Mohammed Mahmoud Ayoub (8 total)
MHE. SAID I. MZIMBA aliuliza: -
Je, lini Serikali itatenga Bajeti kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya Polisi Mtambile na Kengeja kwa kuwa vimechakaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Said Ibrahim Mzimba, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishafanya tathmini ili kubaini gharama halisi za ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha Kengeja baada ya kituo kinachotumika sasa kuwa kichakavu na kwamba hakiwezi kufanyiwa ukarabati. Kiasi cha fedha shilingi milioni 165 zinahitajika. Tathmini kwa ajili ya kubaini gharama halisi ya ukarabati wa Kituo cha Polisi Mtambile zimefanyika na kiasi cha fedha cha shilingi milioni 90 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Polisi vya Kengeja na Mtambile zinatarajiwa kutengwa toka kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027.
MHE. ALI VUAI KHAMIS aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga kituo cha Polisi katika Kijiji cha Matemwe Jimbo la Mkwajuni Unguja kutokana na uwekezaji mkubwa uliopo katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kumjibu swali Mheshimiwa Ali Vuai Khamis, Mbunge wa Mkwajuni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Matemwe Jimbo la Mkwajuni, hakuna sehemu iliyotengwa rasmi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi. Napenda kutumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu, kumshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na Kamisheni ya Ardhi Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kutenga eneo kwa ajili Kituo cha Polisi Matemwe, ili Serikali iweze kutenga fedha kutoka kwenye bajeti yake kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha Polisi.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: -
Je, lini Serikali itafanya maboresho ya makazi ya askari pamoja na kununua magari mapya Gereza la Babati Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Khambay, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Babati ni miongoni mwa Magereza yaliyojengwa miaka mingi tangu mwaka 1974 hali iliyosababisha uchakavu wa miundombinu ya gereza pamoja na majengo ya makazi ya Askari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limeanza kutekeleza mpango mkakati wa muda mfupi na muda mrefu ambapo kwa Gereza Babati ziko nyumba tatu zinaendelea na ujenzi kwa kutumia mapato ya vyanzo vya ndani vya ubunifu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi 5,380,000,000/= kwa ajili ya ununuzi wa magari 31 kwa shughuli za Utawala na kusafirisha Mahabusu. Pindi magari hayo yatakapofika, Gereza la Babati litapatiwa gari moja mpya kwa matumizi ya kituo.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukipandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kutokana na ukuaji wa mji huo kiutalii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi na kuuagiza kwamba unapaswa kuwasilisha hoja yao ya kutaka kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kaskazini āAā Unguja, ambayo itashauri na kutoa mapendekezo yake kwenda Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo na ushauri wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar yatawasilishwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji wa kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi iwapo vigezo vya kiulinzi, kiutawala na miundombinu vinavyotakiwa vitakuwa vimekamilika.
MHE. AZZA H. HAMAD K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-
Je, lini Serikali itatoa fedha, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kujenga Kituo cha Polisi, Ushetu, kwenye kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 6,456 kilichopo katika eneo la Nyamilangano. Fedha, kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho zinatarajiwa kutengwa na kutolewa kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2027/2028. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. ASHA JUMA KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga upya Kituo cha Polisi cha Mfenesini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Asha na ninampongeza. Hivyo kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Juma Kombo, Mbunge wa Mfenesini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kujenga kituo kipya cha Polisi Daraja āCā katika eneo la Mfenesini, ambacho kitagharimu kiasi cha fedha shilingi 165,228,990. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2027/2028. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Magereza Tunduru kwa kuwa jengo lililopo haliendani na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Ado Shaibu Ado kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua hali ya uchakavu wa majengo katika magereza mengi hapa nchini likiwemo Gereza la Tunduru. Kwa sasa Serikali kupitia Jeshi la Magereza ina mpango wa ukarabati na upanuzi wa gereza hilo kwa awamu, ambapo tathmini ya uchakavu pamoja na michoro imekamilika na inatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 465 katika ukarabati na upanuzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza itaendelea kutenga fedha kwenye bajeti kila mwaka pamoja na kutumia vyanzo vya ndani vya ubunifu ili kuhakikisha inatekeleza mpango mkakati wa ukarabati na ujenzi wa magereza nchini likiwemo Gereza la Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. OMARI ISSA KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali imefikia hatua gani ya kuanza ujenzi wa Ofisi ya NIDA katika Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekamilisha kazi ya usanifu (design) wa michoro ya majengo na miundombinu ya TEHAMA, na inaendelea na taratibu za kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ambapo zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi huo imetangazwa na taratibu za manunuzi zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Machi, 2026, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekamilisha kazi ya tathmini ya hali ya mazingira (Environmental Impact Assessment) pamoja na uchunguzi wa hali ya udongo na ardhi (Geotechnical Investigation) katika viwanja hivyo kwa lengo la kuhakikisha usanifu na ujenzi wa ofisi hizo unafanyika kwa kuzingatia hali ya mazingira na udongo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Mamlaka imelipa fidia kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni waliokuwa wakifanya shughuli zao katika kiwanja hicho kwa ajili ya kupisha ujenzi wa ofisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa awamu ya kwanza ambao ilihusisha ujenzi wa Kituo cha Kanzidata, Kituo cha Uokozi wakati wa Majanga na Ofisi za Usajili za Wilaya 13, Serikali kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa (National ID System Expansion Project- Phase II) ambao unahusisha ujenzi wa Jengo la Makao Makuu Jijini Dodoma, ujenzi wa Kituo cha matengenezo ya vifaa vya TEHAMA na ujenzi wa Ofisi za Usajili katika Wilaya 31 ikiwemo wilaya ya Micheweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ujenzi huo pia utahusika na kuboresha na kuimarisha Mfumo wa Usajili na Utambuzi kwa kuongeza njia za uhakiki kwa kutumia alama ya mboni za macho na sura (Iris and Facial Recognition System) ili kuwa na alama za uhakika zaidi za kibaiolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.