MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu, lakini nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri, je, watakubaliana nami kwamba, kutokana na uwepo wa vijana wengi sana wasiokuwa na ajira, ni dhahiri kwamba mipango yote iliyopo haijafanikiwa kutatua tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nilitoa ushauri huko nyuma kuhusu makambi ya kilimo kwa vijana. Siyo kweli kwamba kama yangetekelezwa, tatizo hili lingeisha kabisa na kuondoka katika Taifa hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunakubaliana sote kuwa suala la changamoto la ajira siyo kwa Tanzania pekee, hili ni suala la dunia nzima. Hata hivyo, Serikali imeendelea kutekeleza program na mikakati mbalimbali kama nilivyoeleza kwenye jibu la swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka 2024, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimepungua kutoka 8.2% mwaka 2021 hadi 6.2% mwaka 2024. Serikali itaendelea kupanga na kutekeleza mipango na program hizo na nyingine ili kuendelea kupunguza tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali lake la pili, Serikali ilipokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na moja ya utekelezaji wake ni Program ya Jenga Kesho Iliyobora ya BBT kutoka Wizara ya Kilimo ambapo vijana wanaendelea kunufaika na program hiyo. Aidha, Serikali itaendelea kuweka mikakati na kutekeleza kwa lengo la kuondoa au kupunguza tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)