Answers to supplementary Questions by Hon Joel Arthur Nanauka (13 total)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yanalenga kuwatia moyo vijana, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mheshimiwa Waziri ni kiasi gani cha fedha kimetengwa kupitia Mfuko huu wa Maendeleo wa Vijana Taifa katika mwaka huu wa fedha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ili kuwasaidia na kuweka ahueni kwa vijana, Wizara haioni haja sasa ya kuya-hold hayo mashirika na maeneo mbalimbali ambayo wanataka kuwasaidia vijana ili waanzishe SACCOS maalum kwa vijana wa nchi hii na kupunguza zile afueni kwa ajili ya vijana ikiwemo riba? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Latifa, Mbunge wa Viti Maalum kwamba Serikali kwa miaka yote kupitia Idara ya Vijana iliyokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana, lakini utakumbuka kwamba Mheshimiwa Rais alielezea dhamira yake ya kuona namna anavyoongeza mitaji kwa ajili ya vijana katika kuwawezesha kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira hiyo ipo na Serikali muda mfupi ujao itatoa mpangilio wa namna ambavyo vijana wa Tanzania watanufaika na mitaji ambayo itatolewa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, pili Wizara yetu itaendelea kuratibu, kushirikiana na mashirika na wadau mbalimbali ambao wanajishughulisha na shughuli za vijana, nia na dhamira ikiwa ni kukusanya nguvu za pamoja kuwawezesha vijana katika nchi yetu sawasawa na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo uliboreshwa mwaka 2024. Ahsante sana.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Je, ni kwa namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha vijana wa mijini na vijijini wanashiriki kikamilifu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Mahawanga. Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Vijana imeweka mkakati maalum wa utekelezaji wa ushiriki wa vijana wa mijini na vijijini pia rika zote na wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza afua hizo na kuhakikisha kila kijana wa Tanzania anakuwa sehemu ya mambo muhimu yanayofanywa katika Taifa letu. Ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri utaungana na mimi, huwezi kumtaja kijana bila kuigusa Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano. Nilikuwa nataka kufahamu, Wizara ya Vijana mna ushirikiano gani wa karibu na Wizara hiyo ambayo nimeitaja katika kuzitafuta, kuzitangaza na kuzilinda ajira zote za nje ya nchi na pia kuwasimamia vijana wote ambao wanapata ajira nje ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri wewe unafahamu kwamba ajira na fursa nyingi hazipo tu katika Wizara ya Vijana, zipo pia katika Wizara nyingine za kisekta.
Je, Wizara au Serikali kupitia Wizara ya Vijana haioni haja sasa kuanzisha Youth Desk Officers katika kila Wizara ili kuona namna gani Wizara ya Vijana inazisimamia fursa zote zinazotoka katika wizara za kisekta? Nakushukuru sana. (Makofi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nimpongeze Mheshimiwa Latifa kwa kuwa mstari wa mbele kila wakati kufuatilia masuala yanayohusu vijana na kuongeza tija katika utekelezaji wake, kuhakikisha fursa zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoeleza, Serikali inafanya kazi kwa muunganiko na sisi kama Wizara ya Maendeleo ya Vijana, tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Kazi, Ajira pamoja na Mahusiano. Ahadi ya Chama Cha Mapinduzi ni kutoa ajira takribani 8,000,000 katika miaka mitano ijayo. Katika hilo, ilielekeza waziwazi kwamba inalenga pia kutafuta ajira nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano, mikataba mbalimbali imekuwa ikiingiwa kati ya Serikali na nchi mbalimbali. Mpaka sasa kuna vijana 7,593 ambao wameenda katika mataifa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchukua nafasi hii nitoe wito kwamba tumekuwa na changamoto ya vijana kadhaa ambao wamekuwa wakielezea changamoto kuhusiana na mchakato huu. Serikali inaingia mikataba hii kupitia Balozi zetu na Serikali ndiyo custodian wa mikataba ya ajira kupitia mawakala wa ajira binafsi ambao wamesajiliwa na Serikali. Mwezi Februari mwaka huu zaidi ya mawakala 148 walifanya kikao na Serikali, katika kuhakikisha kwamba vijana wanatumia utaratibu unaofaa, wakitembelea tovuti ya Serikali wataona mawakala hao ambao wameidhinishwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hayo ni kwamba vijana huwa wanapewa taarifa kwa maana ya kupewa mafunzo, wanapopata nafasi ya kwenda nje ya nchi ili kuepusha changamoto ambazo wanakutana nazo. Serikali itaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha fursa nyingi zinaendelea kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Latifa, ni kwamba Serikali ina Maafisa Maendeleo ya Vijana wanaopatikana katika halmashauri mbalimbali. Mara tu baada ya kuundwa kwa Wizara hii, mwezi Desemba tulifanya kikao cha pamoja cha uratibu na Maafisa Maendeleo ya Vijana wote wanaopatikana katika halmashauri zetu, nia ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika mfumo. Nimepokea wazo ulilolitoa kuhusiana na Youth Desk, na nikuahidi kwamba Serikali italifanyia kazi ili kuhakikisha taarifa zinawafikia vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tuna vijana wengi sana wamejiajiri hasa upande wa garage. Kwa mfano pale Jimbo la Bukoba Mjini, tuna vijana zaidi ya 250 wako kwenye garage ya Mnyonge, lakini wako barabarani.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuwatengea maeneo maalumU ya kufanyia shughuli zao hizo za garage ili waweze kwanza kuwa na uhakika wa shughuli zao, lakini waweze kuwa na sifa za kupata mikopo ya Serikali? Ahsante
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa swali la Mheshimiwa Mutasingwa na bahati nzuri nilishafanya ziara katika jimbo lake na nilipita katika maeneo ya garage na tulikuwa naye pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba vijana hawa kwanza tunawarasimisha ili kupata urahisi wa wao kupata fursa ambazo Serikali inazitengeneza. Mpaka sasa kupitia programu ya urasimishaji ambayo inafanyika kupitia VETA, mwaka huu pekee yake malengo ni kurasimisha vijana 14,400. Ninaamini vijana mojawapo watakaopata fursa hii ni vijana wanaopatikana katika jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupitia TAMISEMI kumekuwa na utaratibu wa kupanga maeneo rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanapata maeneo ambayo hawatabugudhiwa. Nimhakikishie, Serikali itaendelea kuratibu zoezi hilo na vijana wataendelea kupata nafasi na fursa za kufanya kazi katika maeneo ambayo ni rasmi. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, vijana wengi wamekuwa wanapata hizi fursa za mikopo na Serikali imejitahidi sana kufungua hizi fursa, lakini tumekuwa na shida kubwa sana kwa vijana kwa sababu wengi hawana nidhamu ya fedha (finance mistress), lakini sasa Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili waweze kujengewa uwezo wa kuwa na nidhamu ya fedha? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Serikali imeendelea kujitathmini kila wakati kuona namna ambavyo mikopo inayotolewa hasa kwenye kundi la vijana inakuwa na ufanisi. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Kapoma, ni kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana hasa katika urejeshaji, kwa mfano tukiangalia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana, zaidi ya shilingi bilioni 3.9 zimeshindwa kurejeshwa. Tumefanya tathmini kuangalia changamoto ni nini, ikiwepo pia na asilimia nne zinazotolewa kupitia halmashauri zetu. Moja ya changamoto tuliyoiona, ni elimu ya kifedha na ndiyo maana kupitia awamu hii ya mikopo tuliyoitoa, tumeingia utaratibu wa makubaliano rasmi na taasisi ya kifedha hasa CRDB, ambayo kabla kijana hajapata mkopo, huwa anapata fursa ya kupewa mafunzo maalum yanayohusiana na usimamizi wa kifedha, nidhamu pamoja na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya yanakuwa endelevu pia, ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kupata elimu hiyo kwa namna endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea wazo lako na ushauri wako juu ya kuwa na SACCOS za vijana, na kama ambavyo Serikali imeendelea kuwezesha kwenye vikundi, tutaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba vijana wanafikiwa kwa wingi. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa Wilaya ya Hanang, wameniagiza na kunituma, wanakuhitaji, Mheshimiwa Waziri, je, ni lini utakuja kukutana na vijana wa Wilaya ya Hanang?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Asia na nimpongeze pia kwa kuendelea kufuatilia masuala yanayohusu vijana hasa katika Jimbo lake la Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara, tunao utaratibu na ratiba ya kutembelea vijana katika maeneo mbalimbali kama ambavyo tumefanya tayari katika maeneo kadhaa ya nchi yetu. Nimhakikishie Mheshimiwa Asia, tutakapokuwa tunaweka ratiba kwa mara nyingine tena, basi tutafika pia katika Jimbo la Hanang kuweza kuwafikia na kuweza kusikia changamoto zao, lakini pia kuwaletea fursa ambazo zinapatikana. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tatizo la vijana sio mitaji na ajira pekee, lakini yako matatizo makubwa sana ya kisera kwenye sekta mbalimbali yanayowafanya vijana wasikue kwa haraka. Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba sera zote katika kila sekta zinapitiwa ili kuruhusu ukuaji wa wa mitaji na uwezo wa wa kiuchumi kwa vijana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Shangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba changamoto za vijana ni zaidi ya mitaji na ndiyo maana kwa mujibu wa Sera yetu ya Maendeleo ya Vijana Toleo la mwaka 2024, limeainisha maeneo 13 ambayo tunayalenga na mitaji ni sehemu mojawapo tu ndogo. Nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba tumeendelea kufanya marejeo na mapitio ya sera ambazo zitatusaidia pia kuelekea katika sheria. Moja ya mafanikio ya sera ya mwaka 2007 ilikuwa ni kutungwa kwa sheria ya asilimia nne katika halmashauri zetu, lakini pia 30% ya manunuzi kwa ajili ya makundi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutaendelea kufanya hivyo kama Serikali na kuhakikisha kwamba kila eneo ambalo vijana wanaweza wakapata fursa tunaendelea kuleta marekebisho hayo ya kisera zaidi. Nashukuru sana.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pia nimpongeze, tangu ameteuliwa kwa kweli amekuwa faraja na tabasamu kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza; kwa kuwa kwenye mikopo hii ya 10% ya halmashauri zipo halmashauri ambazo zinafanya vizuri na zipo halmashauri ambazo hazifanyi vizuri kutokana na makusanyo yao kuwa madogo. Wizara ya Mheshimiwa Waziri inahusika na vijana na baadhi ya maeneo hayo vijana wamekuwa hawapati fedha kwa sababu makusanyo ni madogo.
Je, Serikali kupitia Wizara yake ikishirikiana na TAMISEMI imejipangaje kwa halmashauri zile ambazo makusanyo ni madogo kuzitengea fedha ya ziada ili vijana waweze kupata mikopo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tumemwona Mheshimiwa Waziri maeneo mengi akienda kuzungumza na vijana. Vijana wa Rukwa wanaujuzi, ni wachapakazi, na wanatamani sana wamuone. Je, ni lini atafika Mkoa wa Rukwa kuzungumza na vijana wa Mkoa wa Rukwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Sylvia Sigula kwa niaba ya Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia masuala yanayowahusu vijana. Nipokee pongezi zao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais ambaye ndiye ametuagiza na kututuma kufanya kazi hii kwa ajili ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huwa ina utaratibu wa kufanya tathmini katika maeneo ambayo ameyataja kuwa na changamoto ya kupata fedha sasa katika halmashauri ambazo zinahusika. Kupitia tathmini hiyo inatuongoza kuona namna ambavyo tunaweza kuweka juhudi za ziada katika maeneo ambayo yana uchache wa fedha kulinganisha na idadi ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba kupitia tathmini hiyo ndiyo inatuongoza pia kutoa vipaumbele kupitia uwezeshaji mbalimbali ukiwemo uwezeshaji unaotokana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la pili, ameulizia kuhusiana na mimi kwenda Rukwa, si mara ya kwanza, najua ameuliza swali hili. Ninapenda nimhakikishie Mheshimiwa Sigula kwamba Rukwa pia kuna vikundi vilivyonufaika katika awamu ya kwanza ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; mojawapo ni katika Wilaya ya Kalambo. Baada ya Bunge hili kukamilika, ratiba itaanza kupitia maeneo mbalimbali na nitafika Rukwa, nitafika pia kukutana na vijana wa Rukwa.
MHE. LUCY D. S. KOMBANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, Serikali ina mkakati upi wa kuhakikisha vijana wa vijijini, hususani wa Mkoa wa Morogoro wanapata fursa hizi za ujuzi, mafunzo na hata mikopo kwa usawa, licha ya kuwa na changamoto ya miundombinu pamoja na ukubwa wa mkoa kijiografia?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Kombani. Nipende kumhakikishia kwamba katika utaratibu wa kiserikali tunaweka vipaumbele katika maeneo pia ambayo hayafikiki kirahisi. Wiki iliyopita tu nilikuwa Mkoani Morogoro, na tulishirikiana na vijana kutoka katika wilaya mbalimbali kuhakikisha kwamba wanapata taarifa hizi. Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu sana pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba vijana wa maeneo mbalimbali ambayo yako pembezoni mwa mji wanafikiwa na programu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wamehamasika na hamasa iliyofanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na hasa kwa kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha vijana, wakiwepo vijana wa Jimbo la Bunda Mjini. Wamefuzu vigezo na yeye anajua wamekwishakwenda katika ofisi yake, amekutana nao. Je, ni lini watapata mikopo ili waweze kujiinua kiuchumi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuendelea kufuatilia vijana wa Jimbo lake la Bunda. Kama anavyosema, ni kweli kwamba tumekwishaonana nao. Kwa sasa utaratibu uliopo ni kufanyiwa tathmini kupitia taasisi ya kifedha ambayo ni CRDB tulioingia nao makubaliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba vijana wa Bunda ni kati ya vijana ambao wamepata katika awamu ya kwanza, na tutakwenda jimboni pia ili kuhakikisha kwamba tumetimiza ahadi hiyo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninachukua fursa hii kushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wanawake wengi hawapati taarifa kwa wakati kuhusiana na uwepo wa mikopo hii na utaratibu ambao unapaswa kufuatwa. Je, Serikali inaweka utaratibu gani sasa wa uwazi ili wanawake wengi zaidi waweze kunufaika na mikopo hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; changamoto kubwa ya wanawake wajasiriamali ni ukosefu wa elimu ya ujasiriamali husika. Sasa ili kuacha alama kutokana na mkopo huo ambao umetolewa na Mheshimiwa Rais kwa wanawake wa nchi hii. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka utaratibu wa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ili kuhakikisha biashara zao zinakuwa endelevu na zina tija kwa wanawake husika na Taifa kwa ujumla?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, kwanza nimpongeze kwa kuendelea kuwasemea wanawake wa Arusha na Tanzania nzima. Kuhusiana na taarifa, tumeweka utaratibu mzuri wa kushirikiana kwanza na Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao wanapatikana kila eneo katika nchi yetu na katika kila halmashauri tunao Maafisa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana, tunao Maafisa Maendeleo ya Vijana ambao pia wanapatikana katika halmashauri zetu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tunaendelea kushirikiana na wawakilishi wa wananchi wakiwemo Wabunge na Waheshimiwa Madiwani ambao wanafanya mikutano mara kwa mara kuhakikisha kwamba taarifa hizi zinawafikia wanawake wa Arusha, lakini pia wanawake kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nimhakikishie Mheshimiwa Paresso kwamba katika suala la uwezeshaji, wanawake wanapewa kipaumbele sawasawa na sera yetu ya maendeleo ya vijana, lakini pia vipaumbele vya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili ameulizia kuhusiana na mafunzo; ni kweli kumekuwa na changamoto ya muda mrefu na takwimu zimeonesha kwamba urejeshaji wa mikopo hii, moja ya changamoto imekuwa ni kukosekana kwa elimu. Serikali mwaka jana Novemba, 2025 ilitoa mwongozo maalumu ambao unahusiana na usimamizi na uratibu wa mikopo inatolewa katika halmashauri zetu pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo huu kipengele 5.11 unaelezea umuhimu na uhitaji wa kufanya mafunzo kwa vikundi ambavyo bado havijapewa mkopo, lakini pia wakati wa mkopo na katika namna ya kuwafuatilia pia. Sisi kama Wizara tumeingia makubaliano maalumu na sekta binafsi ikiwemo taasisi za kifedha na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hatujatoa mikopo hii, sasa hivi kinachoendelea ni mafunzo yanayoendelea kwa ajili ya kuwapatia mikopo hii. Juzi tu, mkoani Kigoma tumekuwa na mafunzo haya kwa ajili ya kuwandaa watakaopata mikopo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kufanya hivyo kama sehemu ya kuimarisha wanufaika kwa mikopo hii. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri, hujapita Kiteto kuzungumza na vijana. Swali langu ni hivi, hizi pesa za Mheshimiwa Rais, nia yake ziguse kila mahali. Sasa na sisi tunaotoka vijijini kama Kiteto, ni nini kipya kutoka Wizara yenu kinachoonesha kwamba wale wananchi wa Kiteto waliohamasika wakiwemo vijana na akinamama watapata hizi pesa za Mheshimiwa Rais? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa swali la Mheshimiwa Olelekaita na ninamuahidi kwamba Kiteto nitafika ipo kwenye ratiba ya kuwafikia vijana huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo hii kama nilivyoeleza awali huwa tunafanya tathmini maeneo ambayo yamepata na maeneo ambayo hayajapata, hasa yale ambayo yako pembezoni. Kwa sababu inatolewa pia kupitia Wizara za Kisekta, tumeweka utaratibu maalumu wa vipaumbele vya kisekta katika maeneo tofauti tofauti kama vile ufugaji, uvuvi na biashara za kawaida kwa kulingana na eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema hii ni awamu ya kwanza, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu zinazofuata pia zitagusa katika eneo lako kulingana na sekta za kipaumbele ambapo ninafahamu kule kwako suala la mifugo ni suala la msingi pia na tutalizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi kwa niaba ya wananchi wa Butiama ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana, ni mkakati gani uliopo kuhakikisha kwamba akinamama na vijana wa Wilaya ya Butiama kwa Baba wa Taifa nao wananufaika na huu mkopo wa shilingi bilioni 200?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa swali la Mheshimiwa Dkt. Mahera, Mbunge wa Butiama na ninamhakikishia tu kama ambavyo nimetoa hakikisho hili kwa Wabunge wengine kwamba tumeanza awamu ya kwanza na kila jimbo la kila Mbunge aliyepo katika Bunge hili atafikiwa kwa awamu yake itakapofika. Kwa hiyo, asiwe na shaka yoyote, aendelee kuandaa vijana, awaambie wakae mkao wa kula, kwa sababu uwezeshaji huu utamfikia kila kijana wa nchi hii ya Tanzania.