Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohamed Mussa Utaly (1 total)

MHE. MOHAMED M. UTALY aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Mtange hadi Kineng’ene Kibaoni kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Mussa Utaly, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kipande cha Barabara ya Mtange – Kineng’ene chenye urefu wa kilometa 5.5 hadi kufika Kituo cha Afya Kineng’ene ni sehemu ya Barabara ya Mtange – Kibaoni yenye urefu wa kilometa 19.3 iliyopo katika Jimbo la Lindi Mjini. Ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami umekuwa ukifanyika kwa awamu, ambapo mpaka sasa kipande cha kilometa 2.3 tayari kimejengwa kwa kiwango cha lami kwa awamu tatu tofauti ambazo zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.449.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa urefu wa meta 600 kwa kiwango cha lami. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa mita 600 za kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu ili kuendelea na ujenzi wa barabara hii.