MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, niwashukuru sana wizara hii kwa kutupatia mnara katika Kata ya Tandangongoro. Tandangongoro sasa inazungumza; je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Jimbo la Lindi, hususan katika maeneo ya Kata ya Chikonji, Kitumbikwela, Mbanja na Rasbura?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Lindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yetu tunatekeleza mpango wa miaka mitano wa kujenga minara katika mikoa na wilaya zote nchini ikiwemo Jimbo la Lindi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wetu huu tutafika katika jimbo lake na tutafanya kama anavyoomba kujenga minara ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF kutuma wataalamu katika jimbo hili kufanya tathmini ya uhitaji wa minara katika jimbo lake ili tuingize katika mpango wetu wa miaka mitano wa ujenzi wa minara nchi nzima. Nakushukuru.
MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ikiwemo pamoja na barabara iendayo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na barabara inayopita katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lindi zilishaidhinishwa kujengwa katika awamu hii ya mwaka 2025/2026 ambapo mwaka huu wa fedha unaishia mwezi Juni.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mpaka sasa TAMISEMI haijatoa kibali, ili TARURA iweze kusaini mkataba na mkandarasi. Je, ni lini TAMISEMI itatoa kibali ili TARURA iweze kusaini mkataba na mkandarasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mohamed Mussa Utaly, Mbunge wa Lindi Mjini kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Lindi Mjini.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kwa nia njema imeweka utaratibu, baada ya kutangaza zabuni na kupata wakandarasi kuna utaratibu wa kutoa kibali baada ya kujiridhisha na uwepo wa fedha ili miradi ikianza na wakandarasi wakiwa site kusiwe na mkwamo wa kukosa fedha.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kupitia TARURA imeshapokea maombi ya kupata kibali hicho na sasa wako hatua za mwisho za kutoa kibali hicho ili mkataba huu uanze kutekelezwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo. Ahsante sana.