Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Switbert Zacharia Mkama (20 total)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru nimepata majibu ya Serikali yamejieleza kwa kina, lakini tunapoongelea uchumi wa kidijiti component mojawapo kubwa ni intanenti ndio kufikia huo uchumi wa kidijiti. Kwa sasa hivi ukiangalia watumiaji wengi wa intanenti ambao inawasaidia kwenye biashara gharama imekuwa ni kubwa sana. Maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Wizara ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara ya Vijana ni upi mkakati wa kuwafikia vijana kwenye makundi mbalimbali ambao wanatumia intanenti mfano vyuo vikuu, watumiaji wa kusafirisha abiria mtandaoni mfano Uber na Bolt, wauza nguo wadogowadogo ambao wanafanya biashara zao kupitia online wakae nao katika hayo makundi waelezee uhalisia na makundi mengineyo namna ambavyo wanapata changamoto kubwa kupitia intanenti na watumiaji wengine?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali inaonaje ikae na taasisi binafsi ambazo zinatoa huduma hizi kwa ajili ya kuwaomba kupunguza gharama za internet, mfano Kampuni ya Vodacom na kampuni nyingine, kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za vifurushi ili ambao wanajiajiri kupitia sekta hii iweze kuwasaidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu ushauri wake wa kukaa na vijana kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Vijana, tumeupokea na tutakutana na vikundi mbalimbali vya vijana ili kujua mahitaji yao na changamoto zao wanazozipata katika upatikanaji wa internet katika shughuli zao. Kwa hiyo, tutawasiliana na wenzetu wa Wizara inayohusika na Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya kulishughulikia suala hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kukaa na taasisi binafsi kwa ajili ya kupunguza gharama za vifurushi, mwaka jana (2025) Serikali ilikaa na taasisi binafsi na tukapunguza bei za vifurushi vya internet na kwa sasa katika Afrika Mashariki ukiiondoa Rwanda, Tanzania ndiyo nchi yenye vifurushi nafuu kuliko nchi nyingine zote, zaidi ya Rwanda. Kwa hiyo, tutaendelea pia kukaa na hizi taasisi binafsi tuangalie namna gani tunavyoweza kuboresha zaidi gharama za vifurushi ili tuweze kufikia lengo la kuwa na Uchumi wa Kidijiti. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tumepokea ushauri wako na tutaufanyia kazi kwa kadiri inavyowezekana ili tufikie hilo lengo. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni pamekuwa na ongezeko kubwa sana la watumiaji wako wa simu kwenye baadhi ya maeneo ndani ya Jimbo la Tunduru Kusini, hali hiyo imesababisha baadhi ya minara kuzidiwa na ubora wa mawasiliano kutoka kwenye minara hiyo kupungua.

(a) Je, Serikali haioni haja ya kwenda kufanya review, kwa maana ya mapitio kwenye baadhi ya minara ili kuangalia uwezekano wa ama kuongeza masafa au kujenga minara mingine karibu na maeneo hayo?

(b) Je, kama inakubaliana na mimi, kazi hiyo itaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mhandisi Fadhili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kufanya tathmini upya ni kweli baadhi ya minara kutokana na kuongezeka kwa watumiaji inakuwa inazidiwa. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kutuma wataalam katika maeneo ya Jimbo la Tunduru Kusini ili wafanye tathmini na kubaini changamoto hiyo haraka iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja la nyongeza. Kuna vijiji takribani vitano katika Jimbo la Chato Kaskazini, ambavyo ni Vijiji vya Mkungo, Nyakato, Buzirayombo, Itale na sehemu kubwa ya Ilyamchele. Vijiji hivi havipati mawasiliano kwa sababu hakuna mtandao na hii husababisha utoaji wa elimu hasa kwenye shule za msingi na Sekondari ambako sasa wanatumia TEHAMA wanafunzi wanashindwa kupata haki yao kama wanafunzi wengine. Je, Wizara ina mpango gani wa kwenda kuweka mtandao katika maeneo hayo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la ndugu Mheshimiwa Magembe, Mbunge wa Chato Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la swali la msingi, tunatambua changamoto ya mawasiliano nchi nzima na ninaamini kila Mbunge aliyemo katika jengo hili ana changamoto ya mawasiliano katika Jimbo lake kwenye sehemu moja au nyingine. Ndiyo maana sisi kama Wizara tunaandaa mkakati wa miaka mitano wa kuyafikia maeneo yote yenye changamo ya mawasiliano na tunaamini katika kipindi hiki cha miaka mitano, tutafika kila eneo kule ambako hakuna minara, tutajenga minara mipya, kule ambako minara imezidiwa, tutaiongezea nguvu ili kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 changamoto ya mawasiliano katika Majimbo mbalimbali na hapa nchini iwe imepungua kwa kiasi kikubwa au tumeimaliza kabisa. (Makofi)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga minara katika Kata za Mtunguru, Mkwedu, Chilangala pamoja na Mikumbi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Nawanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Wizara inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Minara 280 katika bajeti hii na katika bajeti ijayo tutatekeleza tena mradi wa kujenga minara mingine 280 ambayo katika mradi huo Kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge nazo tutazipatia kipaumbele. (Makofi)
MHE. HAIDERALI H. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mnara wa mawasiliano katika Kata ya Mughunga, Ilongero Singida Vijijini? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Singida Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la swali la msingi, kwamba tumeandaa mkakati mahsusi wa miaka mitano wa kujenga minara mbalimbali nchini katika maeneo yote yenye changamoto ya mawasiliano. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mkakati huo na eneo lake hilo lenye changamoto pia tutalifikia.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa na mimi nafasi ya swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Kitwai na Naberera Wilayani Simanjiro?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mkakati wetu wa miaka mitano wa kuhakikisha kwamba nchi hii yote inapata mawasiliano, tutajenga minara, kama nilivyosema, katika maeneo mbalimbali ili kuyafikia maeneo yote yenye changamoto. Yale ambayo yana minara, lakini hayana mawasiliano ya kutosha au yana changamoto tutaiongezea nguvu. Kwenye eneo lake hili la Simanjiro ambalo hakuna minara ndani ya hiki kipindi cha miaka mitano tuna uhakika tutakuwa tumefika na tumejenga minara kwa ajili ya kuondoa changamoto hiyo.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo, hasa katika Jimbo la Nanyumbu, minara ipo lakini wananchi wanahitaji huduma zaidi ya ule mnara wa mawasiliano. Je, Serikali haiko tayari kuwashauri wawekezaji wengine wakatumia ule mnara mmoja ili kurahisisha upatikanaji wa mawasiliano wa maeneo yote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari kampuni za simu zinachangia baadhi ya minara katika baadhi ya maeneo; mnara mmoja kampuni mbili ama matatu zinaweka vifaa vyao vya mawasiliano. Kwa hiyo nichukue nafasi hii pia kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kulifanyia kazi suala hili ili hiyo minara kama ina changamoto au imezidiwa, basi waangalie uwezekano wa kuwasiliana na kampuni ili waongezewe nguvu. Kama kuna uwezekano mwingine pia basi kampuni ziruhusiwe kuwekeza zaidi kwenye mnara huo ili kampuni mbili ama tatu yaweze kutoa huduma kwa kutumia mnara mmoja. Zoezi hilo litafanyika kwenye baadhi ya maeneo.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tarime Vijijini lipo mpakani mwa Kenya. Kwa hiyo Kata za Susuni, Mwema, Sirari, Nyanungu, Gwitiryo tunapata mawasiliano kutoka Kenya; lakini vilevile maeneo kama Mrito kwenye mgodi pale wa dhahabu, Gorong’a karibu na Hifadhi ya Serengeti hakuna mawasiliano kabisa. Nimeuliza swali hili miaka mitano imepita sasa ninaomba Serikali iniambie. Je, ni kwa nini wananchi wa maeneo hayo wanapata shida ya mawasiliano mpaka leo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa kupata nafasi na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Niombe kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Waitara. Tunatambua changamoto iliyopo uhafifu wa mawasiliano hasa katika maeneo ya mipakani ikiwemo Sirari, Tarime pamoja na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine, kama Serikali tunaendelea kufanyia kazi kuhakikisha tunaongeza nguvu katika minara iliyopo katika maeneo ya mipakani; na sasa katika awamu yetu ya kumi na moja eneo hilo litakuwa la kipaumbele ikiwemo maeneo yanayopita SGR, lakini pia maeneo ya barabara kuu pamoja na maeneo ya mipakani kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo imekuwa ikitukabili unajikuta mkifanya adjustment katika maeneo ya minara katika maeneo ya mipakani baada ya muda nchi za wenzetu pia wamekuwa wakifanya adjustments. Kwa hiyo unajikuta unarekebisha hali leo baada ya muda unajikuta pia changamoto inaendelea kurudi pale pale na inakuwa inapelekea masuala ya roaming na kusoma minara mingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kufanya ukaguzi na usimamizi zaidi mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba kutakuwa na adjustment ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata mitandao kutoka mawasiliano ya Tanzania pekee. Ninakushukuru.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; bado Jimbo la Tabora Mjini kwenye kata za pembezoni nilizozitaja hapo zina changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Kuna baadhi ya maeneo walitoa maelekezo ikajengwe minara hiyo ya Halotel lakini haijajengwa. Nini mpango wa Serikali kwenda kujenga hata hiyo Minara ya Halotel wanayoisema ili wananchi wa kata hizi za pembezoni zilizoko kwenye Jimbo la Tabora Mjini waweze kupata mawasiliano ya uhakika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; pamoja na sasa hivi kuwa tuko kwenye awamu ya uwezo wa mitandao yetu 5G lakini mpaka leo Tabora Mjini bado tunapokea mawasiliano kwa kutumia 2G. Nini mpango na mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka minara yenye nguvu ya uwezo wa kupeleka 5G ili wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini ambalo linakua kwa kasi waweze kupata mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa minara kwenye maeneo aliyoyataja pembezoni mwa Mji wa Tabora, kama nilivyoeleza kwenye jibu la swali namba 74 nilieleza kwamba tunatambua changamoto ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini na tuna mkakati mahususi wa miaka mitano kuanzia mwaka huu 2025 mpaka 2030 ambapo tutayafikia maeneo yote yenye changamoto za mawasiliano ikiwemo ni pamoja na eneo lake la Tabora Mjini.

Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo ambayo yana minara na ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano, tutatuma wataalam wetu wakafanye tathmini na pale ambapo kutaonekana kuna uhitaji wa kuiongezea nguvu hiyo minara tutaiongezea nguvu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya kuwepo minara ya 2G katika maeneo ya mjini. Ni kweli bado kuna maeneo hapa nchini yanasoma minara ya 2G lakini kwa maeneo ya mjini mengi yameshafikiwa na minara ya 3G na 4G. Iwapo bado kuna maeneo ya Mjini Tabora yanasoma minara ya 2G, ninaomba kupitia Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nimwelekeze Mkurugenzi Mkuu wa TCRA apeleke timu yake ya wataalam kufanya tathimini katika eneo la Jimbo la Tabora Mjini ili kutambua ni kwa nini bado kunasoma minara ya 2G ambayo katika maeneo ya mjini mengi hakuna changamoto kama hiyo.
MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Kwa kuwa tatizo la mawasiliano ni la nchi nzima na katika Jimbo langu la Uyui tatizo kama hili lipo na linasumbua sana katika Kata ya Ibili, Ibelamirundi, Ndono, Makazi na Bukumbi. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam ili waangalie maeneo ambayo yanafaa kuweka mnara waweze kuweka haraka iwezekanavyo ili wananchi waache kupanda miti kutafuta mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Uyui kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumwelekeza tena Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kutuma timu ya wataalam katika Jimbo la Uyui kuweza kufanya tathmini na kutambua changamoto zilizopo za mawasiliano katika jimbo hilo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Bunda Mjini kata za pembezoni pia kuna changamoto ya mawasiliano kama Kunzugu, Bukole, Nyamatoke na Mihali. Ni lini changamoto hiyo itatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mheshimiwa Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tuna mkakati maalum na mahususi ambao tunauandaa Wizarani na utakamilika hivi karibuni. Mkakati huu tunakusudia kuyafikia maeneo yote yenye changamoto za mawasiliano likiwemo Jimbo la Mheshimiwa Bulaya. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa kwamba katika mkakati wetu huu na siku si nyingi tutamfikia katika maeneo yake yenye changamoto na nimpongeze pia kwa jinsi anavyowapigania wapigakura wake wa Bunda Mjini. Kwa kweli wamechagua Mbunge mahiri. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Pili ninaishukuru Serikali kwa kuanza kujenga mnara wa simu katika Kata ya Kikolo, na pia kufikiria kuanza kufanya tathmini ya kujenga mnara wa simu katika Kata ya Kagugu. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mradi unaoanza kutekelezwa kujengwa mnara katika Kata ya Kikolo unakwenda kwa kusuasua. Nataka nijue, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mnara huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kijiji cha Ruangai eneo la Kipungu Kata ya Mpepai kuna changamoto kubwa ya mawasiliano ya simu. Ni lini Serikali itaweka mkakati wa kuhakikisha kwamba inajenga mnara wa simu katika eneo hili ili wananchi waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa mnara tulioutaja katika Kijiji cha Kikolo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii itakamilika tarehe 30 Juni, 2026, kwa sababu tayari mkandarasi ameshapatikana na anaendelea na mobilization. Atakapokamilisha mobilization, ujenzi utaanza mara moja. Ifikapo tarehe 30 mwezi wa Sita, ujenzi huu utakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ya mawasiliano katika Kijiji cha Luhangali, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mkakati wetu wa Serikali wa miaka mitano kuanzia mwaka 2025 kwenda mwaka 2030, tutafanya tathmini katika maeneo yote yenye changamoto na tutayafikia. Tutaanza na maeneo ya changamoto kubwa, changamoto za kati na changamoto zenye unafuu. Kwa hiyo, tutapitia zote na kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 kila Mwananchi wa Tanzania atakuwa na uso wenye furaha katika sekta hii ya mawasiliano.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ni utaratibu gani unaotumika kwa kutumia mkongo wa Taifa katika kupeleka mawasiliano kule Zanzibar ili kufikisha huduma kwa wateja kwa haraka sana na kwa maeneo ambayo hayafikiki?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaotumika katika kupeleka mawasiliano Zanzibar kupitia mkongo wa Taifa, huwa kwanza inafanyika tathmini, kuangalia uhitaji wa maeneo husika, ikishafanyika, Shirika la Mawasiliano Nchini hupeleka mawasiliano hayo kulingana na uhitaji wa eneo husika.
MHE. PROF. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, kwa kuwa taaluma ya teknolojia ya TEHAMA sasa hivi ni taaluma ya msingi sana katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali kwamba ujenzi wa chuo hicho uweze kupata kipaumbele. Hii itawezesha kwanza kunufaisha vijana ambao wakipata elimu hiyo wataweza kujiajiri kwa sababu ya ile elimu waliyoipata. Pia, hiyo itasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kutumia teknolojia ya maendeleo vijana wetu watakuwa wamepata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo basi, ombi letu ni kwamba, Serikali ione jinsi gani iweze kupata uwezeshaji wa ujenzi wa hicho chuo, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Profesa, amekuwa akilifuatilia suala hili kwa karibu kwa Mheshimiwa Waziri na pia kwangu. Hii inaonyesha kwamba ana hamasa kubwa ya masuala ya teknolojia ya Habari, na Wananchi wa Buhigwe pia wana hamasa hiyo. Nimhakikishie kwamba ombi lake tumelipokea, na tutatoa kipaumbele kikubwa katika ukamilishaji wa chuo hicho.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nitoe pongezi zangu kwa Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya kuhakikisha mawasiliano yanapatikana, na hasa ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeona juzi tu, tarehe 10 Aprili, 2026 alizindua minara 785 kwa ajili ya mawasiliano nchini. Pongezi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mawasiliano yanaendelea kuimarika, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa urahisi hasa ukizingatia wafanyabiashara wengi wanatumia mitandao kwa ajili ya kufanya biashara zao wakiwemo wanawake?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninamshukuru kwa pongezi kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anayofanya kuhakikisha kwamba nchi hii yote inakuwa na mtandao wa kuaminika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye jibu lake kwamba Wizara yetu ina mpango mkakati mkubwa wa miaka mitano ya kuhakikisha kwamba nchi hii yote inakuwa na mtandao wa mawasiliano wa kuaminika na katika hilo, hii itatoa kipaumbele kikubwa kwa makundi maalum yakiwemo akina mama, vijana, wenye ulemavu na watu wengine wote walio katika makundi hayo kama wazee na watu wasiokuwa na uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kuhakikisha, ndani ya miaka hii mitano, kila mwananchi na kila kundi maalum litakuwa na uso wa furaha katika sekta hii ya mawasiliano.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi. Pia, ninaishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri ambayo wameyatoa na ninashukuru kwa miradi hii ambayo imefanyika. Ni kweli minara hii imejengwa na haya maeneo yanapata mawasiliano, lakini kama Serikali ilivyojibu Kata ya Nyamigogo ina vijiji vinne na vyote hakuna hata kijiji kimoja chenye mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, eneo hili la Migango, Kata ya Runazi, ambalo umelitaja lina wakazi zaidi ya 10,000 lakini hawana mawasiliano kabisa. Ninajua mmesema ipo kwenye mpango; mpango ni 2025 – 2030. Kwa kuwa hawa watu ni wengi na wanategemea mawasiliano, ninaweza kupata kauli thabiti ya Serikali inayonihakikishia kwamba haitaweza kusubiri mpaka mwishoni kwa sababu bajeti inafanyika kila mwaka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipate kauli ya Serikali inayoweza kuni-assure kwamba mpango utakapoanza, hawa wananchi watapelekewa hiyo huduma haraka ili waweze kupata sub-station kwa sababu ni wengi na wanahitaji huduma ya simu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Mheshimiwa Waziri amesema Kijiji cha Busiri feasibility study inaendelea, lakini jirani na Busiri kuna eneo moja linaitwa Iloganzara kwenye Kata ya Nyakahura. Kuna Kata ya Bisibo eneo la Rwakilinda na Muungano, ni maeneo yenye watu wengi sana lakini hawana mawasiliano pia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba kupata kauli ya Mheshimiwa Waziri na Serikali kwamba hata haya maeneo mawili yatakuwa considered kwenye kufanya feasibility study ili mtakapoanza kujenga hii minara Biharamulo, basi na wao waweze kupata mawasiliano haya kwa ajili ya kuendeleza huduma za wananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika maeneo yote aliyoyataja, kwa sababu amesema kuna changamoto kubwa ya mawasiliano, tutayapa kipaumbele kikubwa katika mkakati wetu tunaoendelea kuutekeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya udharura alioueleza, ninamwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF apeleke wataalamu kule katika hali ya udharura ili wakague na kufanya tathmini katika maeneo hayo kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunaweka mawasiliano mapema ili wananchi wengi aliowataja katika maeneo hayo waweze kupata mawasiliano ya uhakika. (Makofi)
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, viko baadhi ya vijiji mpaka leo havina minara kama alivyosema hapo Mheshimiwa Waziri. Kipekee ninaomba nizungumzie Kijiji cha Mtengashari kilichopo Kata ya Ligunga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Kijiji kile hakina mawasiliano kabisa, wananchi wale wanapata shida. Ni nini sasa mkakati wa Serikali katika kuhakikisha tunakwenda kujenga minara katika kijiji kile na wananchi wetu waendelee kupata huduma ya mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali katika kujenga minara tumeuweka katika mkakati wetu mahsusi wa Serikali wa miaka mitano ambapo tunakusudia kuyafikia maeneo yote yenye changamoto ya mawasiliano nchini ukianza na maeneo ambayo yana changamoto kubwa. Tumeyatenga katika maeneo yenye changamoto kubwa sana, changamoto za kati na changamoto ndogo.

Mheshimiwa Spika, tutaanza na maeneo yenye changamoto kubwa katika mkakati wetu wa miaka mitano na ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafika pia katika maeneo yake kwa ajili ya kuweka mawasiliano ya uhakika kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia kwamba ndani ya hii miaka mitano mkakati wetu utakapokamilika kila eneo lenye changamoto ya mawasiliano hapa nchini litakuwa limepata mawasiliano ya uhakika. (Makofi)
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi. Jimbo la Ulyankulu ni miongoni mwa majimbo yenye hali ngumu ya kimawasiliano hasa katika Kata ya Uyowa, Kijiji cha Mwamnange chenye wakazi wengi na kijiji cha kibiashara Kata za Sasu, Ilege na Nhwande kwa maana ya Kata ya Mwongozo. Lini Wizara itakwenda kujenga minara kwenye maeneo hayo ili wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto ya mawasiliano iliyopo katika jimbo hili na hivi karibuni, ninadhani wiki hii iliyopita wataalamu wa UCSAF walikuwa kwenye eneo la jimbo hili kufanya tathmini. Tunasubiri taarifa yao ili utekelezaji uanze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya taarifa hiyo ya wataalamu kuwasilishwa Wizarani tutafanya mpango wa dharura wa kuhakikisha kwamba katika maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa katika Jimbo lake la Ulyankulu yanafanyiwa kazi, ninashukuru.
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itatatua tatizo la upatikanaji wa simu katika maeneo yafuatayo katika Jimbo la Newala Mjini: Kata ya Nanguruwe, Kijiji cha Nanguruwe, Mnanje, na Mtawe; Kata ya Mcholi I, Kijiji cha Chikwedu na Chiunjila; Kata ya Namiyonga, Kijiji cha Nakachela na Mandumba; Kata ya Mnekachi Kijiji cha Kazamoyo; na Kata ya Mtumachi, Kijiji cha Mcholi Godauni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikieleza katika majibu yangu kwamba Serikali imeandaa mkakati wa miaka mitano wa kuyafikia maeneo yote nchini ambayo yana changamoto ya mawasiliano. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge katika mkakati wetu wa miaka mitano maeneo yake hayo pia tutayafikia, lakini kwa sababu ameeleza kwamba ana changamoto kubwa, tutayapa kipaumbele wakati wa kutekeleza mkakati wetu huu wa Serikali, ninakushukuru.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mamba Kusini katika Jimbo la Vunjo imekuwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu ili tuweze kupata mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kata aliyoieleza Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Vunjo pia itahusishwa katika mkakati wetu wa Wizara, kwa sababu pia amesema kwamba ina changamoto kubwa. Ni kati ya zile kata ambazo na sisi tumepanga kwamba katika maeneo yenye changamoto kubwa tutayapa kipaumbele tunapoendelea na utekelezaji wa mkakati wetu huu wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kikubwa kwa Jimbo lake la Vunjo katika maeneo yote yenye changamoto kubwa, hasa wakati wa utekelezaji wa mkakati mahsusi wa Wizara wa hii miaka mitano tunayoendelea na utekelezaji wake. (Makofi)