Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haji Kombo Mdowe (3 total)

MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukipandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kutokana na ukuaji wa mji huo kiutalii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi na kuuagiza kwamba unapaswa kuwasilisha hoja yao ya kutaka kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja, ambayo itashauri na kutoa mapendekezo yake kwenda Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo na ushauri wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar yatawasilishwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji wa kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi iwapo vigezo vya kiulinzi, kiutawala na miundombinu vinavyotakiwa vitakuwa vimekamilika.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga ukuta katika Fukwe za Bahari ya Nungwi Kiungani ili kuzuia bahari kuingia katika makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mmonyoko wa fukwe unaosababisha bahari kuingia katika makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hili, Serikali imefanikiwa kupata ufadhili kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) ambapo jumla ya dola za Marekani 500,000 sawa na takribani shilingi bilioni 1.3 za Kitanzania zimetolewa na mfuko husika kwa ajili ya kutekeleza mradi katika mwaka wa fedha 2025/2026 na 2026/2027 wa kuimarisha utayari wa Kisiwa cha Zanzibar kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu utaanza mara baada ya tathmini ya athari hizo kukamilika. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha vijana wanashirikishwa na kuwa sehemu ya upangaji miji ya kisasa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua vijana ni kundi muhimu katika ujenzi wa miji ya kisasa, miji jumuishi na endelevu. Serikali imeweka misingi ya kisera na kisheria, kupitia Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, Toleo la 2023, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya Mwaka 2000 na Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355, inayosisitiza upangaji shirikishi, matumizi endelevu ya ardhi na ushirikishwaji wa wadau wote katika maendeleo ya miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia matakwa hayo ya kisera na kisheria Serikali itaendelea kushirikisha makundi yote ya wadau wa uendelezaji wa miji, ikiwa ni pamoja na kundi la vijana ambalo ni muhimu katika kuchangia usanifu wa miji nchini. Ushiriki wa vijana ambao ni takribani asilimia 35 ya idadi ya watu nchini umekuwa ni nguzo muhimu katika upangaji miji ya kisasa na hivyo, kuwa na miji stahimilivu, jumuishi, salama na endelevu, ikiwa ni utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu Na. 11 na Ajenda Mpya ya Miji ya Mwaka 2016 – 2036. Ninaomba kuwasilisha.