Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Haji Kombo Mdowe (4 total)

MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa ruhusa yako. Kwanza ninaomba niishukuru na kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya katika nchi yetu. Pia ninashukuru kwa majibu yao ambayo wamenipa, kwa sababu majibu haya yametoa mwongozo mzuri katika suala letu hili. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza katika jambo hili: -

(a) Je, ni vigezo gani vya kiulinzi, kiutawala na kimiundombinu vinavyotakiwa kukamilika ili kituo cha Polisi kiweze kupandishwa hadhi?

(b) Je, ni jukumu la nani hasa kukamilisha vigezo vya kiulinzi na kimiundombinu katika vituo vya Polisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Jimbo la Nungwi kwa maswali yake mawili ya nyongeza, ambayo ni muhimu sana. Ninapenda kumfahamisha Mheshimiwa Mdowe kwamba, vigezo vya kimiundombinu ni madaraja ya majengo ya Jeshi la Polisi ambayo yapo kwenye daraja la C1, C, B na E, kutegemeana na aina au eneo linalotaka kujengwa kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ombi ambalo wamewasilisha wao kwa Kituo cha Polisi cha Nungwi, kwa sasa kipo kwenye daraja C. Kwa hiyo, kinaomba kupandishwa hadhi kwenda kwenye daraja B. Ili kufikia kiwango cha daraja B, basi ni lazima miundombinu hiyo ya jengo la kituo cha Polisi iwe imekidhi vigezo vya daraja B la vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika vigezo vya kiulinzi ni kuangalia parameter za eneo ambalo linaombewa kupandishwa daraja la eneo hilo. Kwa mfano, hivi sasa Jeshi la Polisi linayo maeneo ambayo yamepewa hadhi ya mikoa, lakini kiutawala yapo hadhi ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano halisi ni kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambao umepewa kanda maalum, na ndani yake zile wilaya zimepewa hadhi ya mikoa. Hiyo inatokana na hali ya kiutawala, na pia mahitaji ya kiulinzi katika eneo la Mkoa husika wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa vigezo hivyo, watakapowasilisha maombi yao kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa maana ya Kamati ya Usalama ya Wilaya, itaweza kuchakata na kutathmini hali ya vigezo vyote vitatu kama vitakuwa vimefikiwa na kushauri ipasavyo kwenye ngazi inayofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kwamba, ni nani ambaye ana jukumu hilo, nilieleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, ninauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi kwamba uwasilishe pendekezo hilo kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa maana ya Kamati ya Usalama ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Nungwi wanataka kujua, ni lini tathmini hiyo itakamilika? Kwa sababu kuanzia mwaka wa fedha wa 2023/2024 majibu ya Serikali yalikuja kuhusu tathmini. Ninanukuu; Waziri wa wakati huo alijibu: "Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar imetenga fedha jumla ya shilingi milioni 650..."

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kombo, utakuwa kama unachangia, uliza tu swali.

MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa tathmini hiyo itakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuwa mbaya. Sasa tunataka kujua sisi kama wananchi wa Nungwi, ni zipi hatua za dharura ambazo Serikali zitaichukua kukabiliana na hali ile pale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ameshafika ofisini kwetu takribani mara tatu au mara nne kwa ajili ya kufuatilia jambo hili. Hata jana alikuwepo ofisini kwetu. Tayari imeshafanyika tathmini ya awali kwa Zanzibar yote, na tumebaini maeneo karibia 148 ambayo yameathirika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo maeneo 148, maeneo 123 yako Pemba na maeneo 25 yako Unguja. Serikali baada ya kufanya tathmini hiyo imeanza kutekeleza mradi wa mabadiliko ya tabianchi kukabiliana nayo katika ngazi ya jamii. Tayari tumeshaanza kwa awali na halmashauri 11 kule Zanzibar na halmashauri 54 Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayofuata baada ya tathmini hii kukamilika, tunakwenda kufanya tathmini ya kubaini gharama kwa kila eneo ambalo limeathirika yakiwemo maeneo anayotokea Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, ametaka kujua ni hatua za dharura ambazo Serikali inachukua. Kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge Wilaya ya Kati tumebaini maeneo matatu ambayo yameathirika zaidi kuliko maeneo mengine. Maeneo hayo ni Wadi ya Cheju, Wadi ya Chakwa, pamoja na eneo la Wadi ya Ubago.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii tunayokwenda kuitekeleza kwenye bajeti ambayo Bunge hili limetupitishia, tumetenga kwa nchi nzima kwa maana ya pande zote mbili kupitia Fungu 31, zaidi ya shilingi bilioni 31 ambazo zitatekeleza miradi hii ya mabadiliko ya tabianchi kwa awamu na awamu itakapofika tutajielekeza kwenye maeneo hayo ya Cheju, Chakwa na Ubago. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri anayoendelea kutupatia hapa, lakini mimi nina swali
moja tu dogo la nyongeza ambalo ninapenda kujua ni mpango gani wa Serikali katika suala zima la kuongeza thamani mazao ya uvuvi ili kuongeza kipato kwa wavuvi wetu?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ni kweli kuna haja ya kuongeza thamani ya mazao ya samaki ikiwa ni pamoja na kuwezesha viwanda vya samaki ambavyo vina..., samahani. Ili kuongeza thamani ya samaki itategemea kuongeza thamani ya...

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba arudie swali lake. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haji, tafadhali ongeza sauti na Waheshimiwa Wabunge tunaomba utulivu ili muuliza swali na mjibu swali waweze kusikilizana.

MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi swali langu ni dogo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba kujua mpango wa
Serikali katika suala zima la kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi ili tuweze kuwasaidia wavuvi wetu kupata kipato zaidi. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo kubwa la upotevu wa mavuno ya samaki baada ya kuvunwa na inafikia asilimia kama 30 ya upotevu (post-harvest loses). Ili kuongeza thamani itabidi kuwa na mifumo na teknolojia za kutunza samaki hao wasipotee na hasa mfumo wa vipozeo na Serikali iko inafanya mazungumzo na baadhi ya makampuni ambayo yana teknolojia za kutunza samaki ama kwa njia ya magari au kwa njia ya fridge na vifaa vingine vidogo vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa mfano kwa upande wa dagaa, dagaa wengi hupotea uoza kwa hiyo tuna teknolojia pia ya ukaushaji wa hao samaki ili waweze pia kufika masokoni.

Kwa hiyo, Serikali ina mkakati kwa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kwamba wavuvi wanapata vifaa vya teknolojia vya kuhifadhi samaki baada ya kuvuna ili kupunguza kiwango hicho cha upotevu wa samaki kwa 30% ambayo ni kiwango kikubwa sana na kwa maana hiyo, hiyo itasaidia kuongeza thamani ya samaki nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, ambayo ametupatia hapa, lakini pia, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujua, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuhakikisha mipango ya miji inatenga na kulinda maeneo yatakayowezesha vijana kupata fursa za biashara, kilimo na uwekezaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili; je, Serikali iko tayari kufanya tathmini maalum ya ushiriki wa vijana katika upangaji wa miji na kuweka utaratibu wa kuhakikisha maoni yao yanaingizwa kwenye mipango ya maendeleo ya miji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakushukuru sana Mheshimiwa Mdowe na kukupongeza kwa sababu, umekuwa na vijana, unawawakilisha vijana na kuwatetea na kuangalia hatima yao katika uwekezaji ambao kimsingi ndiyo dira ilivyosema ya mwaka 2050. Kuwa, vijana ni kundi ambalo linalochochea uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipanga na inaendelea kutekeleza mpango wake wa kuwahusisha vijana katika sekta zote. Kama tunavyofahamu, sekta yetu ya ardhi ni wezeshi, tunashirikiana na sekta zote za uzalishaji, ikiwemo viwanda na biashara, kilimo na sekta nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu nikuhakikishie, Wizara ya Viwanda na Biashara na pia, Wizara ya Uwekezaji pamoja na Mipango, imeweka mipango mikakati kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi kwa kutenga maeneo maalum katika ngazi ya Kitaifa, ambayo ni special economic zone. Pia, katika kila halmashauri tuna kongani, ambapo katika kongani hizo tumewaangalia vijana nao waweze kupata fursa, ili waweze kuwekeza. Hivyo natoa wito kwa vijana tutumie fursa hii kutembelea kongani hizo na kushirikiana na halmashauri kutumia fursa katika uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu tathmini. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, si tathmini tu, sisi tunaendelea na utekelezaji kwa sababu, mipango yetu imejionesha wazi kabisa. Takribani 35% ya wananchi wote Tanzania hapa ni vijana kwa hiyo, tathmini ya kwanza ni kujua umuhimu wa vijana kwa sababu, wako wengi katika maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika ushirikishwaji wa upangaji. Tayari tumeanza kuwahusisha kisera na kisheria ndiyomaana tumeweza hata kutenga maeneo haya. Leo hii hata ukimuuliza Waziri wa Mifugo atakuambia kuna mpango wa ekari zaidi ya milioni sita ifikapo 2030 ambapo vijana hao watakuwa wanahusishwa katika kutumia fursa hizo. Ninaomba kuwasilisha.