MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Muleba ni kati ya wilaya ambazo zina maeneo mengi oevu na barabara nyingi zimekatika. Kwa mfano, kutoka Runazi kwenda Kyebitembe mpaka daladala haziwezi kutoa huduma. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wilaya kama Muleba ambazo zina maeneo mengi oevu zinatengewa bajeti mbadala ili iweze kukarabati pindi mvua zinapoharibu barabara zetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nimpongeze Dkt. Kikoyo Mbunge wa Muleba Kusini, na nimhakikishie tu kwamba Serikali inatambua, kutokana na tofauti za hali za kijiografia katika nchi yetu, yapo maeneo yenye mvua nyingi na ardhi oevu zaidi. Pia yapo maeneo yenye milima mingi zaidi. Kwa hiyo, Serikali inapitia utaratibu wa formula ya kugawa fedha za barabara kwenye majimbo na wilaya zetu ili fedha ziendane na hali ya kijiografia na kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kikoyo, wakati formula hiyo itakapokuwa ipo tayari, tutahakikisha Jimbo la Muleba linapewa kipaumbele kinachostahili. (Makofi)