Supplementary Questions from Hon. Dotto Jasson Bahemu (3 total)
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vile vile, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini majibu kama haya si mara ya kwanza kuyasikia hapa Bungeni kwa sababu mwaka jana mwezi Aprili wakati Mheshimiwa Waziri akijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ngara aliyepita, alisema kwamba Serikali tayari ilikuwa katika hatua za mwisho za kumlipa mkandarasi ili kazi ianze kufanyika. Sasa leo, majibu ni kama yale yale ya mwaka jana. Sasa ningependa kupata kauli ya Serikali katika maswali yangu mawili.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, ni lini sasa kazi rasmi ya ujenzi itaanza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, katika eneo la Keza ambalo amesema ndiyo ujenzi utaanza; wanaanza kutoka Keza kwenda Nyakahura au Keza kwenda Murugarama kwa sababu Keza ni katikati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, miradi yetu inachukua muda mrefu na ndiyo maana bado hatujasimamisha, tunaendelea na utaratibu wa kuijenga. Pia, kama nilivyosema kwamba barabara hiyo itajengwa, itaendelea kujengwa na bajeti yake imeshakamilika na ndiyo maana tayari tumeshapata mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, barabara hiyo tutajenga kuanzia Keza – Nyakahura kwa hatua ya kwanza wakati tunasubiri lot ya pili kutoka Keza – Rulenge – Murugarama. Ahsante.
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sisi Hospitali yetu ya Wilaya ya Ngara, na ya Mbuba, pia kuna ujenzi ambao unaendelea, lakini jengo la mochwari, jengo la wodi za wagonjwa pamoja na theatre vilevile bado hayajakamilika. Je, ni mpango gani wa Serikali kuhakikisha kwamba haya majengo yanakamilika ili wananchi waendelee kupata huduma bora sana. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, sote tutakumbuka kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2026/2027 tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 52.25 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo, miundombinu katika hospitali zetu za Halmashauri 105. Nimhakikishie Mheshimiwa Bahemu, yupo ndani ya mpango, tutakwenda wote pamoja kuhakikisha kwamba hospitali hii tunakwenda kuikamilisha katika miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. katika Jimbo letu la Ngara, kuna Kata mbili, Murusagamba na Nyamagoma, ambapo kuna Vijiji vya Ntanga na Kumubuga, ambapo tuna Mradi wa Maji wa muda mrefu ambao ulikuwa unatekelezwa pale, lakini baadaye mkandarasi ni kama ameutelekeza kwa muda mrefu, sasa imefikia hatua wananchi wa vile vijiji...
MWENYEKITI: Uliza swali.
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sababu zipi ambazo zimesababisha ule mradi kusimama, na lini Serikali itaendeleza ule mradi, ili wananchi wa Ntanga na Kumubuga wapate majisafi na salama? Ahsante.
MWENYEKITI: Majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Samahani. Sijamsikia vizuri.
MWENYEKITI: Uliza hapo mwishoni kwa kifupi.
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itafuatilia kujua sababu za Mradi wa Maji wa Kumubuga na Ntanga kusimama ili uweze kufanya kazi na wananchi wa vijiji vile wapate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mbunge ni lini tutafuatilia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia leo tunafuatilia kujua sababu ambazo zimesababisha mkandarasi kutoendelea na mradi. Ahsante sana.