Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kaspar Kaspar Mmuya (1 total)

Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaomba nianze kuchangia hoja hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufika siku ya leo tukiwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini na kuweza kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuwashukuru sana wapiga kura wangu kutoka Jimbo la Ruangwa. Kwa kweli wanazidi kuniamini na kuniunga mkono huku wakijua kuwa kwa dhamana niliyopewa ni ya kitaifa. Mara nyingi ninawa-miss kuwa jimboni, lakini wanaelewa kuwa jambo hili ni la Wana-Ruangwa na ni jambo la kitaifa na tunaendelea kuchapa kazi kwa kulinda nchi yetu kupitia shughuli zote zilizopo katika sekta ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niendelee tena kumshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Leonard Akwilapo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Baba huyu amekuwa mwalimu kwangu, amekuwa mlezi kwangu na amenifanya kweli niwe msaidizi wake kwa kunipa majukumu ambayo naendelea kumsaidia. Ana miongozo pale ambapo anaona ninakosea ananiambia fanya hivi. Ninakushukuru sana sana, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kumshukuru mke wangu Elizabeth Eston Mbilinyi. Jana alikuwa hapa ametoka Ruangwa akiwa na watoto wake akasema naomba nije kushuhudia tukio hili. Kazi yake kubwa anayoifanya ni kunifanya niwe imara kwa kunipa utulivu, lakini ananiongoza katika sala ya kumtegemea Mungu katika kazi yangu. Ninamshukuru sana kwa malezi anayoyafanya kwenye familia yangu wakati mimi naendelea kufanya shughuli za siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninawashukuru sana sana Wabunge wote kwa kuchangia vizuri huku mkiwa na nia njema ya kuleta mabadiliko yenye kuleta matokeo kwenye Wizara hii ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi mmezungumza mengi na mnategemea Wizara hii ifanye mabadiliko na sio mabadiliko tu, tulete majibu ambayo yataleta tabasamu kwa wananchi. Mimi ninawashukuru sana Wabunge. Ninajua tulikotoka ni mbali, lakini tulikotoka huko kuna mengi yamefanyika. Wengi mmeshukuru kwa mambo mengi mazuri ambayo yamefanyika. Ninawaombeni tuwe sehemu ya kuleta matokeo na tuwe sehemu ya kuleta majawabu. Mliyoyaleta sio malalamiko, ni mapendekezo ya maboresho. Tunaendelea kuwa na ninyi, ninawaombeni sana tutakavyokuwa tunatembelea kwenye wilaya au majimbo yenu tuwe sehemu ya kuleta tabasamu kwa wananchi. Ninawashukuru sana sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaeleza mambo machache tu na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi atafanya ufafanuzi wa hoja katika maeneo mbalimbali ambazo mmeeleza katika michango yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa eneo la utoaji wa hati. Waheshimiwa Wabunge wengi mmekiri hapa kuna changamoto kubwa sana katika eneo hili la utoaji wa hati. Ni ukweli tulikotoka huko ndiko hali ilivyo, lakini kama jambo hilo umelifuatilia kwa kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan utaungana na Wizara hii kusema kuna mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mwaka 2021 tulitoa hati ndani ya mwaka mmoja hazikuzidi hati 67,331. Hivi ninavyoongea mwaka huu tu katika mwaka mmoja tumetoa hati 107,683 na hatujamaliza mwaka. Nilishawaambia Wizara hii ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Leonard Akwilapo alinipa majukumu mahsusi sana katika eneo hili la kutoa hati kuhakikisha tunatoa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, aliniambia simamia Tume ya Taifa ya Mipango ya Ardhi, simamia eneo la utoaji wa hati, simamia mifumo yote ya Wizara ili ilete ufanisi na tija katika kazi zetu. Nilimwambia ahadi yangu kwake ni kutolala na kuhakikisha kuwa kila mmoja atapata hati. Nitakuja kwenye eneo kama hili siku yoyote ile kuja kuwaambia nani hajapata hati ambaye ameomba nitamtafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawahakikishia kila mmoja mwenye kipande cha ardhi, anayemiliki kihalali, aliyeomba mwenyewe akimaliza wajibu wake wa kuambatisha viambatisho vyake vyote huku akijihakikishia eneo hilo ni la halali, halina mgogoro wowote, huna sababu ya kutopata hati, utapata hati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ila tu ukija na vikwazo ambavyo kuna mgogoro ukaomba lazima kwenda mbele na kurudi utakuwa umesababisha wewe mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe wito kwa Wabunge na Watanzania wote, kumiliki ardhi ni haki yako tena ni haki ya kikatiba na haki hiyo sisi tunakupa ile hati kama kutimiza wajibu, wewe wajibu wako ni kuhakikisha eneo lako hilo unalilinda kwa kutafuta hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba viwanja vingi tunamiliki Watanzania, lakini hatuombi kumiliki kisheria. Ninawasihi sana maeneo yote ambayo yana mipango pia yana master plan, lakini yamepimwa na mchoro wake umekuwa approved, tafadhali ombeni hati na utapewa. Ninawahakikishia kwenye mifumo yote ukiomba hiyo hati unaweza kupewa chini ya saa 48 kama viambatisho vyote umefanya usipoweza unapewa baada ya siku 14. Ninaombeni sana tufanye hivyo eneo hilo na ninaomba kwa kuwahakikisheni hayo, Waziri wangu huyu ameeleza na tumewaeleza kwenye hotuba hii tunataka mikoa yote iwe na mfumo huu wa e-Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tufanye hivyo, sasa hivi tuna mikoa mitano, lakini tuna halmashauri 41. Ninaombeni sana twende tukafanye kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mmezungumza huku chini kuna watumishi ambao wana changamoto katika kutoa huduma bora. Katibu Mkuu wetu yuko mahiri sana, Kamishna yuko mahiri sana, Makamishna wote wa Mikoa mmewasifia wako mahiri sana. Hatuna watumishi wengine isipokuwa hawa ndio tuliokuwa nao. Tusiwabeze, tuwatie moyo. Kazi kubwa wanayofanya, matokeo tunayopata ni wao ndio wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kazi yetu tutawasimamia watumishi hawa na kuchukua hatua. Ninyi wenyewe mmeona kuna watu ambao wamefukuzwa, kuna watu ambao wameshushwa mishahara, kuna watu ambao wameshushwa vyeo na kuna wengine wapo kwenye uchunguzi ili shughuli zingine za kisheria ziendelee. Ninawahakikishia tutaenda kuboresha utendaji huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili mmezungumza sana kuhusu mfumo wa kiutendaji. Mnapendekeza wengine watumishi wetu wa ardhi waende kwenye halmashauri, wengine waende Wizarani. Maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yako wazi kabisa. Tunaenda kuanzisha commission ambayo Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa. Ile commission, kwa kifupi tu ona kama TARURA ilivyo, ona kama TANROADS, ona kama DUWASA, ona kama DAWASA ndio mfumo huu ambao utakuwa unaenda kusimamia sekta hii ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hakutakuwa na huo mkanganyo na hiyo itakuwa kuanzia juu mpaka chini. Ninawahakikishia kwa mfumo huu, taratibu zote zinaelekea kumalizika. Mheshimiwa Rais ninadhani baraza lake anaweza kupitisha kwa haraka na mambo mengine tukayaleta katika mabadiliko ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo moja uniruhusu kwa dakika tano. Kuna Mheshimiwa Paschal Inyasi Chinyele alisema hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Dakika mbili Mheshimiwa.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge wa Dodoma ndugu yangu Mheshimiwa Paschal alisema hapa anataka kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Kabla sijasema lolote, ninaomba tu ujiandae kuona, mwachie shilingi yake na wewe uunge mkono hoja bajeti hii tupitishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tu nimkumbushe kuna mambo mazuri sana yamefanyika Dodoma toka jiji hili mwaka 1973 ilivyotangazwa mkoa huu kuwa makao makuu ya nchi hii kuna mambo mengi yamefanywa pamoja na kuandaa master plan ambayo ipo na ambayo tunaitekeleza sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya sisi kama sekta ya ardhi ni kuandaa detailed plan ya kila maeneo ya kimkakati. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo, maeneo yote ya kimkakati ni lazima yapangwe. Leo hii utakuwa shuhuda, tumeshirikiana na wewe katika kupanga maeneo ya Kitelela.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Kitelela unayoiona ile pale ni kwa sababu ya maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaomba tu nikuhakikishie, maeneo yote ambayo umeyasema jana nasema tu machache Matumbulu, Chigongwe, Mpunguzi, Mbabala, Zuzu na maeneo mengine yote ya kimkakati, tayari tumeshakubaliana na Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo hapa tunaenda kuandaa mpango wa kina wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama yameendelezwa tutaweka jinsi gani ya kurasimisha, lakini tutashirikiana na sekta zote katika upangaji ili Jiji na wao wahusike, Wizara ya Maji, Ujenzi, barabara na umeme ili tunavyopanga tuwe kitu kimoja. Leo hatutaki maendeleo yakienda mtu mwingine aturudishe nyuma kwa ajili ya kwenda kufanya ubomoaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo nikasema nieleze ili ndugu yangu asichukue shilingi ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)