Answers to supplementary Questions by Hon. Kaspar Kaspar Mmuya (12 total)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nimweleze kwamba kuna changamoto kubwa katika eneo la Bwakila Chini, kwa maana ya Kijiji cha Ngwade, Serikali imepima maeneo kwa ajili ya kuwamilikisha wananchi na wananchi wamelipa fedha zote, lakini hadi sasa hawajapatiwa hati zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Kijiji cha Msonge pia wananchi walijiunga katika kikundi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo, wakawa na makubaliano na Serikali ya kujenga zahanati katika eneo husika, wananchi hawa waliahidiwa kupimiwa viwanja na Wizara ya Ardhi na kumilikishwa na tayari wamefanya wajibu wao kwa kujenga jengo lile, lakini hadi sasa Serikali haijatimiza wajibu wake wa kuwapimia na kuwapatia hati ili waendeleze shughuli za kilimo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari sasa kuambatana nami jimboni kuwasikiliza wananchi na kujionea changamoto hizi ili aweze kuzitolea majibu? Ninafahamu Mheshimiwa Naibu Waziri kwa muda mchache aliohudumu katika ofisi yake ni bingwa wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza Morogoro Kusini kwa kweli wamechagua Mbunge ambaye anafuatilia changamoto mbalimbali za wananchi wake. Wakati ni mgeni kabisa katika nafasi hii alishawahi kunipigia na tuliwahi kuzungumza juu ya changamoto mbalimbali na hatma yake na leo hii ameleta jambo hili na anazidi kuwatetea kujua haki ambazo wanastahili katika maeneo hayo, hongera sana Mbunge na hongereni wananchi wa Morogoro Kusini kwa kupata mwakilishi mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji alivyovitaja na alivyozungumza kuhusu haki yao ya kupatiwa hati, huo ni wajibu wa Wizara kwa sababu tayari mpango ulishapangwa na upimaji umeshafanyika, ni suala la kutoa hati tu. Nikuahidi, nitaambatana na wewe katika ziara ambayo tutakubaliana, tutaenda maeneo husika na siku hiyo nikuhakikishie kama kutakuwa na hati ambazo wanastahili kupewa watu hao katika vijiji hivyo tutazitoa na wewe ukiwemo na wananchi wako wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na sheria, sera, kanuni na taratibu ambazo amezieleza hapo Mheshimiwa Naibu Waziri, maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo bado yanavamiwa, na bado yanabadilishwa matumizi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni hatua gani ambazo Serikali inachukua kwa yale maeneo yote ambayo yamevamiwa na yale ambayo yamebadilishwa matumizi mpaka tunavyozungumza sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa baadhi ya maeneo ya wazi hasa maeneo yanayoenda kwenye masoko yaliyo karibu na shughuli za watu yamevamiwa na yamejengwa holela kiasi cha kuzuia hata magari ya zimamoto kwenda kuzima moto inapotokea dharura, na maeneo mengine ya michezo yamevamiwa na shughuli za michezo haziendelei katika maeneo hayo. Je, Serikali kwa nini pamoja na sheria nzuri ambazo amezitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, wameshindwa kuzisimamia ili Bunge liweze kuchukua hatua na kuweza kusaidia jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru sana kwa kuwa ameonyesha kuelewa matumizi ya maeneo haya yaliyotengwa ambayo tunaweza kusema kwa ujumla yake ni maeneo ya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninaomba niseme maeneo yote ambayo kisheria yametengwa kwa matumizi maalum, au maeneo ya wazi, yatabaki hivyo kwa kutumia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote aliyeweza kumilikishwa maeneo hayo ya wazi bila kufuata utaratibu uliowekwa, utaratibu na sheria zinazungumza, haijalishi kuwa una hati sasa hivi, lakini Wizara ya Ardhi kupitia Kamishna wa Ardhi ana uwezo wa kufuta hati hiyo endapo itathibitika kuwa utaratibu wa kumiliki eneo hilo haukufuatwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwaagiza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Wakurugenzi ambao ndio wenye dhamana ya kusimamia maeneo hayo kote nchini kuhakikisha maeneo hayo yanalindwa, na malalamiko yote yanayotolewa mtu kumilikishwa eneo la wazi, kuhakikisha yanashughulikiwa kwa kuangalia taratibu kama zilifuatwa. Ikithibitika kama hazikufuatwa, basi Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa ana dhamana ya kufuta hati ya umiliki wa eneo hilo ili libaki wazi kama ilivyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Husna. Kwanza Serikali haijashindwa. Licha ya jibu langu la msingi nililolitoa kwenye swali la msingi kuhusu uwepo wa sheria, sera, kanuni na miongozo, lakini pia licha ya uwepo wa mfumo wa usimamizi na utekelezaji wa sheria hizi, uwepo wa Wizara na watumishi katika ngazi ya Wizara na pia ugatuaji uliofanyika wa uwepo wa watumishi mpaka ngazi ya halmashauri, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imenuia kusimamia suala hili kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilijulishe Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imenuia kwamba ardhi yote ya Tanzania yenye kilometa za mraba 948,740 yote itapimwa. Ardhi hii ina vijiji 12,333. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo, na Mheshimiwa Waziri wetu anasimamia. Hivi ninavyoongea, mpaka sasa hivi tumepima vijiji 4,873 Tanzania nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tu, amewezesha kupima vijiji 2,697 sawa na 55% ya vijiji 4,873 vilivyopimwa tokea uhuru. Hii ni dhamira ya dhati ya kufanya vijiji vyote vilivyobakia 7,460 viwe vimepimwa ndani ya awamu hii ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti huo ndio mkakati wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Upimaji wa vijiji hivi maana yake itaainisha maeneo haya ya wazi, yatajulikana na tutashirikisha mifumo yote ikiwemo mamlaka za upangaji ili kubainisha maeneo hayo na yalindwe kama nilivyoeleza kwenye rai niliyoitoa kwenye jibu letu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MARYAM USSI YAHYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali la nyongeza. Pamoja na kwamba kuna uvamizi wa ardhi, lakini bado tuna migogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Je, Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kuanzisha mfumo maalum kama vile ilivyo Samia Legal Aid, sasa uanzishwe mfumo maalum wa kusikiliza changamoto ya migogoro ya ardhi ili kuweza kutatulika kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Mariam kwa swali zuri na nia yake njema ya kuwafanya wananchi wetu waishi bila migogoro kwenye maeneo yao wanayoishi na kufanya shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwapongeze sana Mamlaka ya Serikari za Mitaa hususan Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya mpaka Wakurugenzi waliopo katika halmashauri zetu, wamejiwekea utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi, na kila wiki wamepanga siku moja au siku mbili mahususi kusikiliza na kupokea kero za ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu nitoe rai yangu kwa Watanzania wote kwanza, nimesema Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu tunao Maasifa wa Ardhi waliomo kwenye maeneo hayo ambao nao ni sehemu ya timu ambayo Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa wanatumia katika kusikiliza changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Wizara ya Ardhi imejitanabahisha kabisa, tutaweza kutatua changamoto hizi kwa mfumo niliyoeleza, huu wa kusema vijiji vyote vipimwe. Licha ya hivyo, tuna utaratibu wa kuwa na kliniki maalum ya kusikiliza zile kero ambazo zimeshindikana katika ngazi ya wilaya au ngazi ya mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wenyewe ni mashahidi, tumetoka juzi tu hapa kufanya kliniki ya wiki moja Tanzania nzima, hii ambayo tuliita jina kubwa kabisa, Samia Ardhi Kliniki, tuliweza kusikiliza wananchi wengi na tuliweza kutatua changamoto nyingi na tukawapatia wengine hati za umiliki wa maeneo ambayo wameomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wabunge wakiwa sehemu ya wananchi ambao wanawatumikia, tuungane na Serikali hususan Wizara yetu ya Ardhi kuweza kuwasikiliza wananchi katika mikutano yetu tunayokwenda kuongea nao na kutatua matatizo. Kwa kuwa matatizo mengine ni ya kiutawala, lakini yale mengine sisi kama Wizara ya Ardhi, tuko tayari kusaidiana kwenye mikutano au ziara ambazo tutaziweka.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Wapo baadhi ya wawekezaji wamehodhi maeneo makubwa ya ardhi na wameshindwa kuyaendeleza kwa 100%, na wengine kubadilisha matumizi. Nini kauli ya Serikali katika kufanya tathmini na kurejesha maeneo hayo ili kupangiwa matumizi mengine Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mfumo ndani ya Serikali wa kuwezesha wawekezaji hawa wapatiwe ardhi, na ardhi yao ilindwe ili waweze kufanya shughuli ambazo wameombea. Tunashirikiana vizuri na hawa TISEZA na mamlaka nyingine kwa ajili ya kuwapatia ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na ninatoa tu angalizo kuwa maeneo haya yalitolewa kisheria na wanatakiwa wayatumie kulingana na walivyoomba. Ila Wizara ya Ardhi ina utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa kutekeleza matumizi ya ardhi waliyoomba kutokana na hati ambayo tumepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi pale tunapogundua mwekezaji ameshindwa kutimiza masharti ya upatikanaji wa ardhi hiyo na kuyaendeleza, huwa tunampata taarifa na kufuata utaratibu wa kuyachukua na kuweza kuwakabidhi watu wengine ambao wana mahitaji ya ardhi. Hivyo, Mheshimiwa Sara, kama ana mwekezaji ambaye ameshindwa, hivyo, tuwasiliane na Wizara ya ardhi ili tuweze kufuata utaratibu tuweza kuyachukua maeneo hayo.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Tunalo suala la double allocation, na hili limeleta migogoro mingi kwa wananchi. Serikali imejipangaje ku-solve tatizo la double allocation?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yamepatikana pasipo kufuata utaratibu wa kisheria, mamlaka zinaturuhusu kusikiliza changamoto hiyo na kumfutia yule ambaye amepata ardhi hiyo bila kufuata utaratibu, na yule ambaye amethibitika kuwa ni mali yake anapewa. Kwa hiyo, tunamfutia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama kuna makosa yametendeka, huwa tunaongea kwa utaratibu wa kiutawala na kufanya umilikishaji wa maeneo mengine, lakini la msingi ni kufuta umiliki wa yule ambaye amepata pasipo utaratibu.
MHE. SAIDI SALIM HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza madogo kama ifuatavyo: _
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali kupitia Waziri iko tayari kuja Jimbo la Ole kuona jitihada ambazo tunazifanya kwenye suala hili la mikoko?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa Jimbo la Ole tumeanzisha vikundi kwa ajili ya kuvikuza na kuitunza mikoko, je, Serikali iko tayari kuviwezesha vikundi hivyo vya akina mama? Ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Saidi kwa jitihada zake za kusimamia mazingira, na kama ulivyofahamu, mazingira ni kipaumbele na ni moja kati ya nguzo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Vision 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, na ninakuahidi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, nitaambatana naye baada ya kukubaliana ni lini ambapo yeye atakuwa na nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimhakikishie, pwani ambayo ina kilomita zaidi ya 1,424 hivi, inaendelezwa kwa kutumia mpango huu wa kupanda mikoko, na tunatumia sana vikundi kwa ajili ya kupanda mikoko. Hili nimhakikishie, tunaendelea na tutaendelea pamoja na vikundi ambavyo ataviainisha katika Jimbo lako la Ole.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Saidi kwa jitihada zake za kusimamia mazingira, na kama ulivyofahamu, mazingira ni kipaumbele na ni moja kati ya nguzo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Vision 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, na ninakuahidi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, nitaambatana naye baada ya kukubaliana ni lini ambapo yeye atakuwa na nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimhakikishie, pwani ambayo ina kilomita zaidi ya 1,424 hivi, inaendelezwa kwa kutumia mpango huu wa kupanda mikoko, na tunatumia sana vikundi kwa ajili ya kupanda mikoko. Hili nimhakikishie, tunaendelea na tutaendelea pamoja na vikundi ambavyo ataviainisha katika Jimbo lako la Ole.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, naomba nimwulize Waziri maswali ya nyongeza mawili. Swali la kwanza, kwa sababu ya uharaka wa ujenzi wa kituo hiki, na kwa sababu sasa hivi wale zimamoto wanapata shida sana sehemu ya kuishi, je, ni lini sasa hiyo hati itakamilika, kwa sababu tulipita kwenye mfumo wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan uliokuwa unaitwa Samia Ardhi na ulikuwa kwake Mheshimiwa Waziri, nadhani na katika sehemu nyingi alipita, lini sasa tutapata hiyo hatimiliki kwa ajili ya kuanza ujenzi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya kupata hiyo hati kuambatana na mimi kwenda kutukabidhi hilo eneo ili kuleta motisha katika jamii na watu wa Katoro? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumpongeza sana Injinia Kija, kwanza kwa ukaribu wake na wananchi wake, anayeweza kufuatilia changamoto za wananchi wake. Ninakiri kuwa jambo hili analifahamu kwa kina na ndiyo maana analifuatilia kujua lini hati itatoka?
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali lake limekuja kwa wakati muafaka, hati hii nikitoka hapa leo nitaenda kuifuatilia na ndani ya wiki ijayo nitampatia jibu ambalo nina uhakika atapata lini hati yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Injinia Kija ni kwamba Wizara ipo tayari na mimi nipo tayari kuongozana naye katika muda ambao atapanga ili twende kwenye eneo hilo, huku nikifahamu jimbo lake ni kubwa na lina ukuaji mkubwa wa kiuchumi. Ninafahamu hata Kata tu ya Katoro pale jinsi ilivyo na watu wengi zaidi ya 92,000 inahitaji huduma za zimamoto za haraka. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na gari ipo, tukijenge kituo hiki, tunawaletea na gari kabisa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Kakonko ilianzishwa tarehe 8 Machi, 2013 na hadi leo hatuna Ofisi ya Zimamoto wala gari la Zimamoto. Je, ni lini Serikali italeta gari la Zimamoto na kujenga ofisi kwa kuwa tayari eneo lilishatengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mbunge kutoka Kakonko kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, nimhakikishie tu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mapinduzi makubwa sana kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani, hususan Jeshi hili la Zimamoto.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie mpaka sasa hivi kwa mkopo ambao ameupata zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100 ameweza kununua magari zaidi ya 237 ambayo yamesambazwa katika mikoa na wilaya zake.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza sasa, kuna Wilaya sita tu ambazo hazijapata magari haya na siyo kama hawajapata kwa sababu hawastahili, hapana, ni kwa sababu madereva wanaotakiwa kuendesha magari hayo bado hawajapatikana katika Wilaya hizo.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie, kwa jitihada ambazo Serikali inazifanya, hao madereva, hao Askari sasa hivi wapo vyuoni na watafundishwa na watapatikana na tutampelekea gari pamoja na madereva kwa ajili ya vituo hivyo sita. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NASSORO RASHID NASSORO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri aliyonipa, lakini katika eneo hilo la Makangale ambalo sasa hivi linaendelea kukua kiutalii na wageni wanaingia na kutoka, na wengine bila kuripoti katika Ofisi za Uhamiaji. Juzi tu kuna mgeni tulimkamata ana wiki mbili hajaripoti katika Ofisi za Uhamiaji na tukaweza kumpeleka katika Ofisi za Uhamiaji. Je, Waziri ana mpango gani kwa sasa hivi kuweza kuidhibiti hiyo hali au kuiondoa kabisa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kumshukuru Mheshimiwa Nassoro Rashid Nassoro, kwanza kwa uzalendo wa kujua na kuifanyia kazi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan kwa kuwa mlinzi wa eneo ambalo unatoka.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba nikuhakikishie kuwa eneo hilo ni la kimkakati, ni kati ya shehia ambazo zipo kwenye eneo ambalo watalii wengi sana wanakuja. Nikuhakikishie kwamba nitaongeza idadi ya askari ambao watakuja kushirikiana na viongozi wote wa shehia ili kuweza kufanya doria na kuimarisha vipenyo vyote ambavyo kuna uwezekano wa hao wanaokuja kuingia na kutoka bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Spika, pia tutaendelea kuwachukulia hatua wote ambao watapatikana kadri ya vile ambavyo itathibitika kuwa wameingia na kutoka bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Sikonge ni miongoni mwa wilaya za zamani, lakini mpaka hivi sasa hatuna Ofisi ya Uhamiaji. Hivi sasa watendaji wa Ofisi hii ya Uhamiaji wapo katika kijumba kidogo sana na wanafanya kazi katika mazingira magumu kweli. Je, ni lini sasa Serikali itaona haja ya kwenda kujenga kituo cha Uhamiaji katika Wilaya ya Sikonge? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma kwa Askari wa Idara hii ya Uhamiaji, hususankwenye upatikanaji wa Ofisi za Mkoa na Wilaya.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie, bajeti ya 2026/2027 moja kati ya vipaumbele vyake ni kuweka bajeti kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizi. Sasa katika Wilaya ya Sikonge ninaomba tuipe kipaumbele kwa ajili ya upatikanaji wa ofisi hiyo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. NAOMY D. MAIPOPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pia ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa muda mfupi walivyopewa dhamana ya kusimamia Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninampongeza Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma Ndugu Gwakisa Tumaini kwa namna ambavyo anapambana kutatua migogoro kwenye mkoa wetu, lakini hasa kwenye Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada ambazo Serikali imeendelea kuzifanya hasa Wizara hii ya Ardhi, wamefanya kliniki kwenye Wilaya za Kigoma, lakini bado kuna changamoto, ambayo inawagusa wanawake wajane na wazee. Ni ukweli usiopingika kwamba…
MWENYEKITI: Naomba uulize swali.
MHE. NAOMY D. MWAIPOPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa waathirika wakubwa wa migogoro ya ardhi ni wanawake wajane na wazee, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuna sheria mahususi itakayowalinda na kuwatetea wanawake hawa kwenye migogoro hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na migogoro kwa baadhi ya ardhi inasababishwa na watumishi ambao siyo waadilifu kwenye Wizara hii ya Ardhi, je, Serikali ina mpango gani kuwachukulia hatua na pia kuwarudisha kwenye maeneo yao husika ili kutatua migogoro?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakushukuru, na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, tunapokea pongezi ambazo amezitoa na ninamhakikishia nitazifikisha pongezi hizi kwa watumishi wote wa Wizara ya Ardhi kwa sababu ndio wao wanaoleta matokeo hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wajane na wazee, ni ukweli alichokisema kuwa walio wengi ndio wanamiliki ardhi kulingana na historia za kimila ambazo wanakuwa na ardhi hiyo. Ndiyo maana Waziri wetu wa ardhi alitoa maelekezo tukaanzisha kliniki maalum ambayo tuliita ‘Samia Ardhi Kliniki’ kwa ajili ya wanawake pamoja na makundi hayo maalum ya wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumepokea ushauri wake na tutaendelea kuona jinsi gani ya kuwafikia kwa rahisi pamoja na kwenda kufanya kliniki hizi katika ngazi ya kata au vijiji pale ambapo tutaona wingi wa changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Watumishi ambao wanakiuka taratibu za kiutumishi aidha za kinidhamu, mara nyingi tumekuwa tunachukua hatua. Ninaendelea kuwaimiza Makamisha Wasaidizi wote wa Mikoa wahakikishe wanasikiliza changamoto hizi za kiutumishi kutoka kwa wananchi wanaolalamika na kuchukua hatua mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo wanaona kuna hitaji la kupeleka Wizarani, Katibu Mkuu wetu Eng. Anthony Sanga yeye ni mahiri katika usimamizi hasa eneo hili la kinidhamu. Ninaamini hakuna Mtumishi ambaye tutamhamisha tu eti kwa sababu amechafua eneo moja, hapana. Utaratibu wa kinidhamu utafuatwa na atapata adhabu kulingana na kosa ambalo amelifanya ikithibitika. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lini Serikali itatatua changamoto ya mgogoro wa ardhi uliokuwepo Kijiji cha Kanamalenga kati ya Mwekezaji na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kanamalenga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Neema kwa kuwa karibu na Wizara hii katika kusaidia kusikiliza kero za wananchi mpaka akatambua uwepo wa mgogoro huu kati ya vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Neema, baada ya hapa niko tayari pamoja naye kukaa na kupanga tuweze kutembelea eneo hilo na kuwasikiliza wananchi na kuweza kutatua changamoto hiyo.