Supplementary Questions from Hon. Mwamengo Ulimboka Baraka (6 total)
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi hii. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Kasumulu kilichopo border ya Kasumulu ndani ya Jimbo la Kyela kwa kuwa kiliathirika na vurugu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Kyela na nimpongeza vilevile kwa kuona umuhimu, na ninadhani kwa sababu ya ufafanuzi wangu wa hoja ya msingi ya kwa nini tunajenga vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye swali la msingi tulilojibu la Jeshi la Polisi kwa mara ya kwanza Bungeni, tulikuja na mpango wa dharura wa maeneo ambayo yana uhitaji wa kujenga vituo vya Polisi na tuliainisha wastani wa maeneo 698 nchi nzima. Hayo ndiyo maeneo ya dharura kujenga vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo 698 ambazo ni karibu kata zaidi ya 600 zilikuwa hazina kabisa vituo vya Polisi na kata 77 zilikuwa zimeanza ujenzi kwa maboma, lakini hawajakamilisha. Nataka kumwambia tu Mheshimiwa kwamba tunaona umuhimu wa kujenga kituo cha Polisi eneo hilo, lakini lini? Mpango ule tumeugawa katika awamu tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza tutakuwa na vituo 196, awamu ya pili tutakuwa na vituo 212 na awamu ya tatu tutakuwa na vituo 211. Kwa hiyo, kukamilika kwa Mpango huu, basi na eneo lake litakuwa tayari limeingia kwenye ujenzi.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza, na ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki cha Barabara cha kutoka Ibanda kwenda Itungi Port kwa sasa kimeharibika sana na hasa section ya kutoka Kyela Mjini mpaka Itungi Port na Wananchi wa Kajunjumele wanapata shida sana. Je, Waziri atakuwa tayari kufika Kyela kutembelea hicho kipande ili kuweza kujionea hali iliyopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, niishukuru Serikali kwa jinsi ilivyotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Border Post pale Kasumulu kwenye mpaka wetu na Malawi. Ninaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia. Je, Serikali itakuwa tayari kutoa fedha za kujenga barabara inayounganisha ile Border Post ya Kasumulu ili kuonesha nia njema ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya kile kituo cha border ya pamoja ikiwemo barabara za kuingia stendi na taa za kufanana na kile kituo kilichojengwa, kile cha border ya Kasumulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ikishakuwa na mkandarasi, mara nyingi mkandarasi ndiye anahusika, kwa hiyo, nina uhakika kwa kuwa alisimamishwa, kutakuwa kuna mahitaji makubwa yanahitajika ya kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba tu kutumia Bunge hili Tukufu kumwelekeza Meneja wa Mkoa wa Mbeya ambapo nilisikia wanamsifia sana, na kweli ni mchapakazi mzuri, aweze kuwasiliana na TANROADS Makao Makuu, kwa kuwa mkandarasi hayupo, basi aweze kupata fedha ya dharura ya kuitengeneza barabara hiyo iweze walau kupitika na kuondoa hiyo adha kwa sababu mkandarasi hayupo kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kufanya matengenezo ama ujenzi wa barabara ya kwenda stendi na kuweka taa kwenye ile eneo la OSBP ili kupata sura nzuri ya nchi; ninajua hiyo ndiyo sehemu ambayo wananchi wetu wanapokwenda Malawi, ndiyo njia ya kutokea, na pia wananchi wa kutoka Malawi ndipo wanapoingilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwelekeze Meneja wa Mkoa wa Mbeya aweze kuangalia hizi barabara, afanye tathmini na kuleta mahitaji. Nina uhakika atashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuona nini wangetamani kifanyike katika ile OSBP ambayo ndiyo mpaka wa kwenda Malawi, waangalie namna ya kuboresha halafu walete tathmini tuweze kutafuta fedha, na kufanya watu wanapoingia katika nchi yetu kuwe na sura ambayo wanasema sasa wanatoka Malawi, wanaingia Tanzania.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa Miradi ya Angana Group, Miradi ya Mbambo Group ndani ya Jimbo la Kyala ambayo imekwama kwa muda mrefu wakandarasi hawajalipwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamtoa hofu Mheshimiwa Mbunge, tunao mpango, tumepanga vipaumbele na miradi ambayo ipo katika utekelezaji tunayo. Tunayo maelekezo ya kuhakikisha kwamba, tunakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutaongeza nguvu ya kupeleka fedha ili wakandarasi warudi, ambao wamekuwa wanasuasua, waweze kuongeza speed ya utekelezaji wa miradi hiyo, ili iweze kukamilika na wananchi waweze kupata huduma ya majisafi na salama.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, eneo lile la Barabara hiyo ya Ipyana – Kasumulu kwa kipindi hiki cha mvua imeathirika sana na maeneo makubwa ambayo yanakwamisha magari kupita ni eneo hilo, hasa kipande cha eneo la Igoma, je, Serikali itakuwa tayari kupeleka fedha za dharura, ili kuendelea kuikarabati hiyo barabara wakati tunasubiri huo mradi mkubwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa, Serikali tayari imesema kuwa, imeanza kipande, section ile ya upande wa Ileje, je, awamu ya pili itakuwa tayari sasa kuanza kipande cha Ipyana – Kasumulu – Ngana, ili wananchi waone Serikali inajali, kama ilivyoandikwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi? Ninashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, hii ni barabara ya changarawe, ambayo katika kipindi cha mvua na hasa ule Ukanda wa Kyela ambao una mvua nyingi, huwa barabara nyingi zinakuwa zimeharibika. Huu ni mwezi wa Tano, kwa hiyo, ninamwelekeza Meneja wa Mkoa wa Mbeya afike eneo la barabara kuangalia kama sasa tunaweza tukaanza utengenezaji wa kawaida, na kama sivyo, basi aweze kuhakikisha kwamba, mkandarasi ambaye atatengeneza barabara hiyo katika matengenezo ya kawaida, anatengeneza na kurekebisha yale maeneo ambayo sasa yanafanya hiyo barabara isipitike kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Mbeya, kwa maana ya Wilaya ya Ileje na Wilaya ya Kyela. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ombi la kuanza upande mwingine Serikali itasikiliza, lakini ninafahamu Mheshimiwa Mbunge pia ni mtaalamu wa barabara. Kuna vigezo kadhaa ambavyo vinaangaliwa, hasa kulingana na ushauri wa mhandisi mshauri, barabara ianze wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara zinaanza katikati, nyingine zinaanza mwisho. Kwa hiyo, tutaangalia, kama kutakuwa na vigezo hivyo vya kuanza upande huo wa Ipyana, haitashindikana kufanya hivyo, ahsante. (Makofi)
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kuniona. Ninaomba niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kyela kuna vitongoji ambavyo vina watu wengi na havijapata umeme mpaka leo. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika vitongoji hivyo ikiwemo vya Kata ya Ngonga, Ngana na baadhi ya maeneo ya Lusungo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Baraka, Mbunge wa Kyela kwa kufuatilia kwa karibu kuhakikisha suala la kupeleka umeme kwenye vitongoji vyake 52 vilivyobaki unakamilika kwa wakati. Mheshimiwa Baraka ni kwa sababu ya umakini wako na wewe ni mmoja kati ya Majimbo ambayo kwa kweli vitongoji ambavyo vimebaki ni vichache sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, pamoja na vitongoji ambavyo tayari tumeshakupatia mwezi Februari mwaka huu, tumekuongezea vitongoji vingine 20 ambavyo sisi pamoja na wewe tuliketi na kukubaliana na vile ambavyo vimebaki tutaendelea kutafuta fedha na kuhakikisha kwamba vinapatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kwa niaba ya Mbunge wa Mbeya Mjini. Eneo la bypass ile ya pale Mbeya Mjini ni muhimu kwa bandari yetu na kwa maendeleo ya nchi yetu kwa sababu, inaongeza ubebaji wa mizigo. Ni lini sasa barabara ile itakamilika kwa kile kipande cha bypass?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa Iringa alitoa tamko la kuwa, mikataba mipya haitaanzishwa, badala yake ataendeleza ile ambayo iko tayari, ambayo hatua za manunuzi zimekamilika; Barabara ya Ibanda – Kajunjumele hatua ya manunuzi imekamilika. Ni lini sasa mkataba ule utasainiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Bypass ya Mbeya ni sehemu ya hiyo barabara kuu ya kutoka Igawa – Mbeya – Songwe hadi Tunduma na ndiyo inayofanya ziwe hizo kilometa 218. Kwa hiyo, itajengwa wakati huo baada ya huyo mbia kuwa amekamilisha tathmini na Serikali kukubaliananaye; kwa hiyo, ni sehemu ya hiyo barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, hata fidia ya hicho kipande ambacho ni barabara tayari tumewalipa wananchi, ikiwa inasubiri tu kukamilika. Hata hivyo, tumemwelekeza Meneja wa Mkoa pale anapopata hela kidogo aendelee kuifungua, ili wale watakaohitaji kuitumia waitumie, lakini tukiwa tunasubiri kuijenga kwa njia nne. Kwa hiyo, mpango huo upo na unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Barabara ya Ibanda – Kajunjumele, tulikuwa tumepata mkandarasi, lakini akasimama, tunavyoongea hivi tumempata mkandarasi mwingine, tunachosubiri ni kupata siku ya kusaini na, kama tulivyosema, ni moja ya barabara ambazo tumeanza kupokea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, itakuwa ni moja ya barabara ambazo tutasaini muda si mrefu, hasa baada ya kupata fedha kwa sababu, ni barabara ambayo kimsingi ilitakiwa iwe inaendelea, lakini tukashindwana na mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni barabara ambayo inapewa kipaumbele kikubwa sana katika kipindi hiki cha utekelezaji, hasa wa mwaka huu wa fedha. Tuna hakika tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami.