Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jamal Ramadhan Mwinyi (2 total)

MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN aliuliza:-

Je, kwa nini Bandari ya Dar es Salaam inashindwa kupokea meli nyingi kwa wakati mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upokeaji wa meli katika gati za bandari zote duniani hutegemea mambo kadhaa yakiwemo urefu wa gati kwa meli husika, ukubwa wa yadi ya kuhudumia shehena, kina cha lango la kuingilia meli, vifaa vya kuhudumia shehena, mifumo ya kuhudumia meli na shehena iliyo fungamanishi, aina na ubora wa barabara na reli zinazoingia na kutoka Bandarini, kasi ya ongezeko la shehena na mahitaji ya meli, pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inazo gati 13 zenye uwezo kuhudumia meli za aina ya Post Panamax ambazo ni kubwa katika ukanda unaohudumiwa na Bandari za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Hata hivyo, idadi hii ya gati bado ni ndogo ukilinganisha na kasi ya ongezeko la meli na shehena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kutokana na ongezeko la meli na shehena kwa ujumla, Bandari ya Dar es Salaam inaendelea na mipango kuongeza idadi ya gati, vifaa na mifumo stahiki ili kukabiliana na hali hiyo. Kwa kuanzia, ujenzi wa gati la meta 500 katika Bandari ya Dar es Salaam umeanza sambamba na maandalizi ya ujenzi wa gati nyingine nne (gati namba 12-15) ambapo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na TPA imeanza mazungumzo ya awali na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata mkopo nafuu kugharamia ujenzi wa gati hizo.
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN aliuliza: -

Je, ni wanyama gani wana vibali vya kuwindwa kwa matumizi ya kijamii kwa kuwa nchi yetu ina wanyama wengi katika mapori ya vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwinyi Jamal Ramadhan, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwindaji kwa matumizi ya kijamii kwa maana ya uwindaji wa kujikimu wa wenyeji, ni moja ya matumizi endelevu ya uvunaji wanyamapori kwa lengo la kutoa fursa kwa wananchi wazawa na wakazi kujipatia kitoweo. Ili kuwezesha wananchi kutumia fursa hiyo, Serikali imetunga Kanuni za Uwindaji wa Kujikimu wa wenyeji za Mwaka 2022 katika Tangazo la Serikali Na. 635 la Mwaka 2022 ambazo zimeainisha taratibu za kufuata ili kuweza kufanya shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni hizo zimebainisha jumla ya aina 23 ya jamii za wanyamapori ambao wanaruhusiwa kuwindwa kupitia uwindaji wa wenyeji ambapo kati yao jamii ya mamalia zipo 18 wakiwemo nyati, pofu dume ama mbunju, pongo, digidigi, nyumbu na jamii za ndege aina tano wakiwemo bata, kanga na firigogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatambua umuhimu wa wananchi kunufaika na rasilimali za wanyamapori, kwani wao ndio walinzi namba moja wa misitu na wanyamapori wetu. Hivyo, Serikali inawaomba wananchi kuzingatia sheria na kanuni zilizopo katika kuwawinda wanyamapori kwa matumizi ya kijamii.