MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa ruksa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Jimbo la Bumbwini, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewekeza nguvu kubwa sana katika uchumi wa nchi na maeneo mengine; je, haioni sasa kuna haja ya kujengwa kituo kikubwa cha polisi katika jimbo hilo kutokana na uchumi wa nchi ulivyokuwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mwinyi Jamal swali lake la nyongeza kuhusiana na jimbo lake la Bumbwini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba Bumbwini kwa sasa ni eneo la kimkakati hasa kwa uchumi wa Zanzibar, kwani Bumbwini inaenda kuelekea kujengwa uwekezaji wa bandari kubwa mpya; Bandari ambayo itakuwa na maeneo karibu matano. Katika bandari ile kwa bahati nzuri wakati nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa mkoa ule, niliwahi kupata fursa ya ushiriki kidogo wa maandalizi ya bandari hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango ulioandaliwa wa eneo lile la Bumbwini kumeandaliwa kujengwa miundombinu yenyewe ya bandari, miundombinu ya barabara za kisasa lakini pia kujengwa mji mdogo. Katika mpango uliowekwa wa mji mdogo ndani yake kuna ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi ambacho kitaweza kusaidia kuimarisha eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa heshima hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Ninaomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, je, ni sababu zipi zinafanya kujengwa kwa kituo cha Polisi? Ni wingi wa watu, idadi ya uhalifu, kilometa, nyumba au ni nini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nimemwelewa vizuri alichotaka hasa ni elimu ya kufahamu kwamba tunapokwenda kufanya maamuzi ya kujenga vituo vya Polisi, ni vigezo gani vinavyotusababisha kufanya maamuzi hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivyo ndivyo, nataka kumwambia tu Mheshimiwa Mwinyi Jamal Ramadhan kwamba kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kuna kitu kinaitwa security audit kwa maana ya ukaguzi wa kiusalama. Eneo ambalo linaonekana lina matishio zaidi ya kiusalama, ndilo eneo ambalo tunalipendekeza kuweza kuliwekea miundombinu ya kiulinzi vikiwemo vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wingi wa watu au idadi ya watu ni moja ya sababu, kasi ya ukuaji wa uchumi inaweza ikawa moja ya sababu, uhamiaji unaweza ukawa pia ni sehemu ya sababu.
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa heshima hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa bandari hii ni bandari tegemezi kwa wafanyabiashara wetu kutoka visiwani na bara na inaleta tija sana kwa uchumi wa nchi yetu, swali langu lipo hapa, ni mara ngapi tangu nchi yetu imepata uhuru bandari hii imefanyiwa utanuzi ama ujenzi wa kuongezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza, katika jitihada za Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukuza uchumi wetu wa nchi na kuweka mkazo katika eneo hili, hatuoni sasa suluhisho la kuongeza uchumi wa nchi yetu ni kwa kutengeneza Bandari ya Bagamoyo? Sambamba na hilo, tujue, je, Bandari ya Bagamoyo kwa sasa imefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Jamal Ramadhan kwa uzalendo wake mkubwa wa kufuatilia miundombinu ya kimkakati katika Taifa letu hususan roho ya nchi ambayo ni bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia uhuru kwa kweli takwimu specific nitashindwa kuzisema hapa lakini ni mara ngapi Serikali imefanya maboresho? Ni mara nyingi katika kuhakikisha na kuona kwamba bandari hii inaongezewa uwezo. Pamoja na mambo ambayo yamefanyika huko nyuma, bado inaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumeboresha gati namba sifuri mpaka namba saba ambapo imeongeza uwezo wa bandari yetu kuhudumia. Pia tumeongeza kina cha bandari yetu ili iweze pengine kuwa na urefu zaidi kwenda chini pamoja na kuongeza upana wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuna miradi mingine inayoendelea bandarini, kama vile kuunganisha reli kwenye bandari yetu, kuhakikisha kwamba tunajenga Gati Namba 12 mpaka 15, kama nilivyozungumza kuhakikisha kwamba, tunawezesha Kituo chetu cha Kurasini kinakuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tayari kuna mradi mkubwa ambao uko 32%, mradi wa kujenga matenki 15 yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo wa mafuta 378. Maboresho yote hayo yana lengo moja tu la kuhakikisha kwamba, bandari yetu inazidi kuimarisha uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, swali lake la pili la nyongeza ametaka kufahamu kuhusiana na ujenzi wa bandari yetu ya Bagamoyo ya Mbegani. Ni kweli kabisa ukiangalia uwezo wa mahitaji yetu sasa ya mzigo kutokana na diplomasia nzuri ya Rais wetu, na jinsi anavyosimamia Uchumi, unaona kabisa Bandari ya Dar es Salaam hata ungeifanyia maboresho kiasi gani inazidi kuzidiwa. Hivyo basi, Serikali imefanya maamuzi ya kuboresha au kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Mbegani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza, tumeshamaliza usanifu. Tayari tumeanza taratibu kwa ajili ya kuanza ujenzi, ili tuanze na kilomita moja, kwa ajili ya kupata kilomita 1.3, kupata gati ambayo itawezesha sasa meli kubwa ambazo kwa sasa haziwezi kutua kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambayo itakuwa inaweza kufika pale. Kwa kweli, bandari ile ikianza kufanya kazi itakuwa ndiyo bandari kubwa kuliko zote kwa ukanda wetu wa Afrika.