Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mariam Anzuruni Mungula (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii adhimu kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa kuwa leo ndiyo nimesimama kuchangia kwa mara ya kwanza, ninaomba kuanza kwa shukrani nyingi sana kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa uzima na uhai wa kunifikisha siku ya leo nikiwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kumshukuru kwa dhati Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na vikao vyake vyote anavyoviongoza vya Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua na hatimaye nikachaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na shukrani hizo ninaomba kumpongeza sana Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa kazi kubwa anayoendelea nayo ya kuendeleza taifa letu. Hata leo tumeona amezindua minara zaidi ya 750 ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa sana kutuletea maendeleo ya mawasiliano katika wilaya zetu na nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine za mwisho, lakini siyo kwa umuhimu na shukrani ninaomba ziwaendee Wabunge wenzangu wote humu ndani, kwanza shukrani kwa kunichagua kuwa mmoja wa wawakilishi wa nchi yetu katika Bunge la Afrika, vilevile niwapongeze na ninyi kwa kuteuliwa kuingia humu ndani ninafahamu haikuwa kazi rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwenda moja kwa moja kwenye mchango wangu kwa hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri, bora kabisa inayoenda sambamba na dira yetu ya maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwa upande wa ardhi na makazi. Waziri Mkuu kwenye hotuba yake amesema kwamba Serikali itaendelea kutekeleza au kujenga nyumba za bei nafuu, tunapongeza sana. Kwanza ninaomba kuipongeza sana Serikali kwa ujenzi wa nyumba hizi za bei nafuu ambao unaendelea nchi nzima katika halmashauri tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza vilevile Serikali kwa jitihada zake za kutaka kuendelea kuwapa Watanzania makazi bora. Niliona kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa, ulisema tuna upungufu wa nyumba takribani milioni 3.8 mpaka tutakapofikia mwaka 2050. Huu ni upungufu mkubwa sana na Dira ya Maendeleo ya Taifa iliainisha suluhisho mbalimbali za kukabiliana na changamoto hii ya upungufu au uhaba wa nyumba za bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kihistoria suala la ujenzi wa nyumba za bei nafuu nchini kwetu lilikuwa linasimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (National Housing), ambalo tangu tulipopata uhuru muasisi wetu au waasisi wetu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume walianzisha initiatives tofauti za kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa wanapata makazi bora. Baba wa Taifa alipoanzisha ninadhani Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa ni moja ya mashirika yaliyoanzishwa mapema sana, vilevile kule Zanzibar Mheshimiwa Karume nae alijenga nyumba za makazi nyumba za bei nafuu pale Michenzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na utaratibu huo wa kuwa na nyumba za bei nafuu kupitia National Housing, kwa bahati nzuri kutokana na maendeleo Shirika la Nyumba la Taifa mwaka 2005 lilibadilika kutoka kuwa Shirika la kutoa huduma kwa jamii kwa maana ya hizo nyumba za bei nafuu, likaenda kuwa Shirika la kibiashara linalojiendesha kibiashara zaidi na liliwekewa sheria yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale ndiyo tukapata vacuum kwamba tumekuwa na pengo. Sasa hivi nchini kwetu tunavyoongea hakuna utaratibu maalum wa kuweka hizi nyumba za bei nafuu zaidi ya Serikali, ndiyo inafanya na hakuna utaratibu kwa maana ya kwamba hatuna sheria inayosimamia hili eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kushauri kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu waangalie uwezekano wa sisi kuanzisha Sera ya Nyumba. Tunayo Sera ya Ardhi, mpaka sasa hivi Tanzania tunayo Sera ya Ardhi, tunayo Sheria ya Ardhi, tunayo sheria mbalimbali ambazo zinafanya kazi katika eneo hili, lakini hatuna Sera Maalum ya Nyumba, wala hatuna sheria maalum inayosimamia makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu gani umuhimu wa kuwa na hii sera, tunakoelekea kwenye ujenzi au upungufu wa kuwa na nyumba milioni 3.8 bila ya kuwa na sera ya usimamizi, Serikali bila ya kuwa na sera muhimu au maalum ambayo itaweza kusimamia hii sekta tutashindwa, kwa sababu nyumba nyingi za bei nafuu au zinazojengwa, zinajengwa kwa kutumia private sector na private sector mara nyingi wako kwa ajili ya faida. Sasa hili ongezeko linaweza likazidi ikawa imetuwia ugumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba Serikali iangalie uwezekano, Bunge hili kwa sababu sisi ndiyo tuliopitisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ili dira yetu iweze kufanya kazi kiufasaha lazima tuitambulishie vitendea kazi, kwa hiyo kuwa na Sera ya Ardhi ni moja ya njia ambazo zitafanya Dira yetu ya Maendeleo ya Taifa ifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo suala la nyumba na Sera ya Ardhi nilikuwa ninaomba kuangalia vilevile, leo asubuhi alikuwa anachangia Mbunge nimemsahau amenitoka, aliongelea kuhusu nyumba za watumishi, upungufu wa nyumba za watumishi na Naibu Waziri wa Afya alitoa takwimu kwamba tuna upungufu wa nyumba za watumishi wa afya takribani 25,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba kuelekeza kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, sasa imefikia muda tuweze kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi. Kwa sababu tunapoelekea population yetu kama nchi inakua na hawa watumishi hususan watumishi wa afya na watumishi wa elimu ni jadi ya kazi yao wanahamahama sana, anaweza akatoka Dodoma akaenda kufanya kazi Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akifika kule anakuta hana makazi maalum ya kukaa, inamfanya kazi yake inakuwa ngumu sana. Hivyo, tutakapoweza kutenga maeneo rasmi au tuseme land bulks sasa hivi ambazo zitatumika kujenga nyumba za watumishi, hiyo itatusaidia sana hata kwa baadaye kuhakikisha kwamba watumishi wetu wanapata makazi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln kuna usemi mmoja maarufu unahusishwa nae unasema kwamba: ‘If I had six hours to chop down a tree, I would spend the first four hours sharpening the axe’. Kwamba ukinipa masaa sita ya kukata mti nitatumia manne ya kwanza kunoa lile shoka. Sasa hivi tuko katika kuelekea au tunaanza kutekeleza Dira yetu mpya ya Maendeleo ya Taifa, kwa hiyo ni muhimu sana tuipe hii dira uwezo wa kufanya kazi na kutekelezeka kiurahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na sheria au sera ya nyumba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaomba kumalizia kwamba, kuwa na sheria au sera ya nyumba itakuwa ni kiungo muhimu sana katika kutekeleza na kuifanya dira yetu ifanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami ya kuchangia katika Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora, Wizara yenye Jimbo langu la uchaguzi nikiwa kama Mwakilishi wa Wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunifikisha siku ya leo nikiwa mwenye afya njema na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba kumshukuru mtumishi wetu namba moja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza sana, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kuchapa kazi kwa bidii na kutupa moyo sisi watumishi wengine wote tunaomsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Dkt. Samia anafanya kazi, wazungu wanasema above and beyond her call of duty. Kwa hiyo, tunampongeza sana na tunazidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu afya bora, afya njema, hekima zaidi na utulivu ili aendelee kutuletea maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuipongeza sana Wizara ya Utumishi na Utawala Bora chini ya Waziri wetu Ridhiwan Kikwete na taasisi zake zote na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi njema wanayoifanya, wanayo kazi kubwa sana, lakini wanaendelea kutuwakilisha Watanzania vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ninaomba kuwapongeza watumishi wote wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka. Utumishi ni kazi ya kujitolea zaidi na kwa kweli watumishi wetu wote wanafanya kazi kwa bidii kwa kiasi kikubwa sana na Mwenyezi Mungu azidi kutubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza zaidi katika upande wa utumishi wa umma. Ninaomba kuanza kama nilivyosema, nikiwa kama mwakilishi wa watumishi mengine ninaweza nikaongea ambayo tayari Wabunge wameshayapitia, lakini nimetumwa na watumishi niyasemee. Kwa hiyo, ninaomba nitayarudia wanivumilie kidogo kwa ufupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la uajiri, ninawapongeza sana Wizara ya Utumishi kupitia Sekretarieti ya Ajira kwa kuendelea vile vile kututolea ajira mpya. Tunayo changamoto moja ndogo ambayo imenifikia wakati wa usaili wa waajiriwa wa wapya, pale tunakuta kwamba obviously, wale wanatoka maeneo tofauti, wanatoka sehemu mbalimbali mikoani pengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu anafika pale amesahau labda cheti cha kuzaliwa anarudishwa anaambiwa hataweza kushiriki kwenye ile interview (usaili), lakini huyu unamkuta ana kitambulisho cha NIDA. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba watumishi kuwe kuna angalau ile customer care iwe kuna hali ya utu fulani wa kuwaangalia hawa watumishi. Wengine wame-struggle miaka mingi hana kazi, halafu anaona hii labda ndiyo chance ya yeye kupata ajira, lakini mambo yanaenda ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru pia Serikali kwa kuendelea kupandisha mishahara na stahiki za watumishi. Vilevile ninaomba kwenye hili suala la mikataba ya hali bora, ukweli ni kwamba hii mikataba ya hali bora inatakiwa kuboreshwa kila baada ya miaka mitatu, lakini unakuta taasisi nyingine hazijaiboresha hii mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi nyingine nyingi hususani za binafsi bado hazijaingia hii mikataba ya hali bora. Hii mikataba ya hali bora kwa kiasi kikubwa inachangia kuleta utofauti wa mishahara na watumishi kuamua kwamba labda nitoke niende nikafanye kazi sehemu fulani, kwa ajili ya kwenda kufuata tu yale maslahi mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba Wizara iangalie uwezekano wa kuhakikisha kwamba taasisi zote zinaingia hii mikataba ya hali bora na inakuwa up to date. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa vilevile tuna suala la mabaraza ya wafanyakazi. Kwenye haya mabaraza ya wafanyakazi ndiyo sehemu ambayo mfanyakazi anakwenda kutoa nyongo yake, tunaweza tukasema, kama ana lolote anaweza kwenda kuongelea hapa kwenye Baraza la Wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inalifahamu kwamba kuna baadhi ya taasisi nyingi huwa hazifanyi haya mabaraza ya wafanyakazi na yako pale kisheria. Kwa hiyo tunaomba Wizara ihakikishe kwamba taasisi zinatekeleza hili jukumu au Maafisa Masuuli wanafanya haya mabaraza ya wafanyakazi. Katika hili ninaomba Waziri wakati akija kuhitimisha atuambie ni taasisi zipi au ngapi ambazo hazifanyi haya mabaraza ya wafanyakazi na Wizara inawachukulia hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba vilevile kwenye hili suala la watumishi wanaojitolea ninaipongeza Wizara imeshachukua hatua.

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Wizara kwa kuchukua hatua kwa watumishi wanaojitolea lakini hizi hatua walizozichukua wao kwa kuweka mwongozo na kutenga bajeti zisambae katika Serikali nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaomba kuliongelea hili. kuna watumishi ambao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha. (Makofi)

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)