MHE. MARYAM USSI YAHYA aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha uhai na uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikizingatiwa kuwa malipo ya michango ya nchi wanachama yamekuwa yakisuasua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (MHE. JAMES K. MILLYA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu tangu niteuliwe kuwa Naibu Waziri, ninaomba kipekee nimshukuru Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Chama chetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Heshima hii ni kubwa na isionekane ni aibu kusema tangu dunia iumbwe, na tangu uhuru wa nchi yetu utokee, ni mara ya kwanza tangu Jimbo hili lipate uteuzi wa namna hii, tunachukua kwa heshima na unyenyekevu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia, kwa namna ya kipekee, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Simanjiro, ambao wamenirejesha Bungeni, nami ninawashukuru ninasema ahsanteni sana. Ninaomba niseme kwamba heshima hii siyo ya bure, ninaiheshimu na mimi nitoe ahadi yangu kwamba nitaitumikia Serikali hii na Watanzania kwa ujumla na kusema nitatenda kazi zangu kwa uzalendo mkubwa na unyenyekevu wa kipekee, ahsanteni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na Waheshimiwa Wabunge ninawashukuru kwa namna ambavyo mmenipa ushirikiano tangu niteuliwe mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Ussi Yahya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeendelea kulinda na kutetea maslahi ya Taifa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuhakikisha kuwa, Jumuiya inaendelea kuimarika na kunufaika kupitia utekelezaji wa programu za maendeleo, ukuaji wa biashara, ongezeko la uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii kama vile afya, elimu, sekta za uchumi za viwanda, nishati, kilimo, mifugo, uvuvi, miundombinu, maji, utalii, upatikanaji wa ajira na kuchangia kuimarika kwa ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na manufaa yanayopatikana, changamoto kubwa inayoikabili Jumuiya kwa sasa ni michango ya baadhi ya Nchi Wanachama kutotolewa kwa wakati na ukamilifu hali inayoathiri utekelezaji wa shughuli na programu za Jumuiya.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea kuwa hai na inatekeleza kikamilifu majukumu yake. Mathalan, Tanzania ilikuwa sehemu ya maamuzi ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Machi, 2026 ambao uliidhinisha mfumo mpya wa uchangiaji ambapo 50% ya mchango utatolewa kwa usawa na kila Nchi Mwanachama na 50% utatokana na uwezo wa nchi wa kiuchumi (GDP). Mfumo huu umeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai, 2026.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Tanzania kama mwanachama hai na mwaminifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tayari imeshatoa mchango wake wa mwaka huu wa fedha 2026/2027 kwa 100%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)