Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maryam Ussi Yahya (2 total)

MHE. MARYAM USSI YAHYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali la nyongeza. Pamoja na kwamba kuna uvamizi wa ardhi, lakini bado tuna migogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Je, Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kuanzisha mfumo maalum kama vile ilivyo Samia Legal Aid, sasa uanzishwe mfumo maalum wa kusikiliza changamoto ya migogoro ya ardhi ili kuweza kutatulika kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Mariam kwa swali zuri na nia yake njema ya kuwafanya wananchi wetu waishi bila migogoro kwenye maeneo yao wanayoishi na kufanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwapongeze sana Mamlaka ya Serikari za Mitaa hususan Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya mpaka Wakurugenzi waliopo katika halmashauri zetu, wamejiwekea utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi, na kila wiki wamepanga siku moja au siku mbili mahususi kusikiliza na kupokea kero za ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu nitoe rai yangu kwa Watanzania wote kwanza, nimesema Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu tunao Maasifa wa Ardhi waliomo kwenye maeneo hayo ambao nao ni sehemu ya timu ambayo Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa wanatumia katika kusikiliza changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Wizara ya Ardhi imejitanabahisha kabisa, tutaweza kutatua changamoto hizi kwa mfumo niliyoeleza, huu wa kusema vijiji vyote vipimwe. Licha ya hivyo, tuna utaratibu wa kuwa na kliniki maalum ya kusikiliza zile kero ambazo zimeshindikana katika ngazi ya wilaya au ngazi ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wenyewe ni mashahidi, tumetoka juzi tu hapa kufanya kliniki ya wiki moja Tanzania nzima, hii ambayo tuliita jina kubwa kabisa, Samia Ardhi Kliniki, tuliweza kusikiliza wananchi wengi na tuliweza kutatua changamoto nyingi na tukawapatia wengine hati za umiliki wa maeneo ambayo wameomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wabunge wakiwa sehemu ya wananchi ambao wanawatumikia, tuungane na Serikali hususan Wizara yetu ya Ardhi kuweza kuwasikiliza wananchi katika mikutano yetu tunayokwenda kuongea nao na kutatua matatizo. Kwa kuwa matatizo mengine ni ya kiutawala, lakini yale mengine sisi kama Wizara ya Ardhi, tuko tayari kusaidiana kwenye mikutano au ziara ambazo tutaziweka.
MHE. MARYAM USSI YAHYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninamshukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Millya kwa majibu yake mahiri. Nina swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwamba Tanzania imeshalipa kwa asilimia mia moja, lakini je, ana taarifa yoyote kwamba Wabunge wa Afrika Mashariki hawajalipwa ndani ya miezi sita, na kama anayo, je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Wabunge hawa wanapata stahiki zao kwa muda mwafaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (MHE. JAMES K. MILLYA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba kipekee nimpongeze Mheshimiwa Mariam Ussi kwa namna ambavyo mara nyingi anafuatilia masuala yake na masuala haya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mambo ya Nje kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali hili ni zuri, lakini kwa kuwa mwanadiplomasia namba moja, pale Arusha Machi, 2026 mwaka huu katika Mkutano wa 25 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania kwa diplomasia ya kipekee iliyojengwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imepata Katibu Mkuu kwa mara nyingine ya pili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara, tunalichukua hili kama changamoto ya wanachama 6,000 ambao waliwahi kutumika kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunaenda kufuatilia kwa umahiri. Kwa kuwa usukani huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upo mikononi mwa Tanzania, mnamfahamu Mheshimiwa Rais ni mtu mnyenyekevu; mnaifahamu Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marais wote ambao wanaunda Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni watu mahiri wanaojali masilahi ya wanachama wote na nchi zote za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Naibu Waziri ninayehusika na sehemu hii ya Mambo ya Nje, nipo tayari kufuatilia na nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba iwapo atahitaji mimi na yeye kukaa ili kubainisha, kwa sababu pia miongoni mwa watu waaminifu huwezi kukosa wawili watatu ambao wanaweza wakapotosha, lakini nipo tayari kukutana naye na kuweza kubaini kwa umakini na kwa uangalifu ili niweze kufuatilia kwa hatua stahiki. Ninaomba kuwasilisha. (Makofi)