Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hemed Sumry Haidary (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu na kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niendelee kumshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, jemedari ambaye anaongoza mapambano kuhakikisha kwamba nchi hii inaenda kwenye mabadiliko makubwa kwenye Wizara hii ya Kilimo. Ninawapongeza na kuwashukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Mpanda Mjini tuna maeneo ambayo yanapaswa kulimwa kwa kilimo cha umwagiliaji, maeneo mawili. Eneo la kwanza ni eneo la Mwamkulu. Ninaishukuru sana Serikali kuna mradi pale wa umwagiliaji unaendelea na tayari umeshafikia 70%. Tunaishukuru sana Serikali, lakini rai yangu katika eneo hili, tunaiomba Serikali ikamilishe huu mradi na kubwa zaidi iweze kujenga mabwawa, kwa sababu tunatamani kupata matokeo. Mradi huu ukikamilika kufika 100% ya ujenzi wa ile miundombinu ya umwagiliaji, kama hatuna bwawa tafsiri yake wakulima watabaki kwenye hatua ile ile ya kulima mara moja kwa mwaka ambayo siyo malengo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba sana Wizara ije na mpango wa kujenga mabwawa na wakulima na wananchi wa eneo lile wako tayari na wameupokea vizuri mradi. Tunaamini watazalisha karibu mara mbili au mara tatu ya kile wanachozalisha sasa. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, tupia jicho kwenye eneo hilo ili tuweze kupata matokeo ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuyapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la hii Skimu ya Umwagiliaji ya Kakese kumekuwa na ahadi za Serikali na juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya ziara kwenye jimbo langu. Maombi yangu na ya wananchi wa Jimbo la Mpanda Mjini ilikuwa ni kuomba hii skimu sasa ianze kujengwa. Majibu ya Naibu Waziri wa Kilimo ambaye tulikuwa naye kwenye ziara hiyo alisema kwamba Serikali wakati wowote itatangaza zabuni ya huu mradi ili sasa kazi ya ujenzi wa hii skimu ianze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kwenye hotuba yote ya Wizara ya Kilimo nimeona kwamba tuko kwenye upembuzi yakinifu kwa 25%, mambo hayo yalishafanyika tayari na kwa 100% mambo yote yameshakamilika, sasa kwa nini wanaturudisha kwenye upembuzi yakinifu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kupitia Wizara, wautangaze mradi huu wa Kakese ili nao uweze kuanza kujengwa. Ukianza kujengwa utaleta ukombozi na utaongeza mapato kwa Serikali, lakini pia utaongeza mapato kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ambayo bajeti yake kwa 50% wanategemea haya mabonde mawili ili kuweza kupata mapato ya ndani ya Halmashauri. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri azingatie huu mradi atusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi wa Kakese ambao bwawa lake litajengwa kwenye eneo la Dilif utahudumia mabonde mawili, utahudumia Jimbo langu la Mpanda Mjini na Jimbo la pili la Mheshimiwa Lupembe kwenye eneo la Nsimbo. Kwa hiyo, unaona ni muhimu kiasi gani bwawa na mradi huu uanze kujengwa ili kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongelea eneo la umwagiliaji, niende kwenye soko. Ahadi ya Ilani ya CCM ya mwaka 2025 - 2030 ni kujenga Soko kubwa la Kimataifa la Mazao kwenye Jimbo langu la Mpanda Mjini. Ninaiomba Serikali, hiyo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni, mambo mahsusi aliyoongelea ni pamoja na hili soko la mazao kwenye Jimbo langu la Mpanda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, tunafahamu ndiyo umeingia kwenye Wizara, inawezekana mambo hayajakaa sawasawa. Ninakuomba katika bajeti ijayo, sijaliona kwenye bajeti hii, ninakuomba katika bajeti ijayo, basi watutengee ili na sisi tuweze kupata soko. Tuna soko dogo pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna soko dogo pale ambalo linafanya vizuri, lakini watu wanapigwa na jua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Ninaunga mkono hoja na Mungu awabariki sana Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uhai. Niendelee kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye eneo hili la sekta ya maji kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nisipomshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji na Mheshimiwa Naibu wake na wataalamu wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwenye eneo hili la kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mpanda uko miongoni mwa miji ambayo ina miradi ya miji 28. Mradi huu ukikamilika utakwenda kupunguza kabisa changamoto ya maji tuliyonayo kwa sababu Mji wa Mpanda kwa sasa unapata lita milioni sita, lakini mradi huu ukikamilika, utatuongezea upatikanaji wa maji kutoka lita milioni sita mpaka lita milioni 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kabisa mradi huu utaenda kuwa mkombozi kwa wananchi wa Jimbo la Mpanda mjini. Ombi langu kwa Wizara ni kwamba itusaidie kusukuma huu mradi kwa sababu mradi huu ulikuwa ukamilike Oktoba, 2025 lakini kuna ahadi ya Wizara kwamba mradi huu utakamilika mwezi wa Saba mwaka 2025, lakini kinachoendelea kule site kinatutia mashaka kwamba mradi huu utaenda kukamilika huu mwezi wa Saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, kaka yangu, twende atusaidie ku-push hawa wakandarasi ili mwezi wa Saba kweli maji yatiririke Mpanda na changamoto ya maji iondoke kwenye Mji wetu wa Mpanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili, tuna kata za pembezoni ambazo zilikuwa zinahudumiwa na RUWASA, lakini kwa kuwa mji wetu ni Manispaa, miji yote ile ya pembezoni imerudishwa kuhudumiwa na Mamlaka ya Maji Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mfano kwenye Kata ya Mwamkulu, Kata ya Kakese, Kata ya Misunkumilo na Kata ya Magamba; kwenye kata hizi za pembezoni kuna miradi ambayo ilikuwa inafanywa na RUWASA, lakini sasa hivi imekuwa kama imesimama kwa sababu ukienda Mamlaka ya Maji hamna bajeti yake. Ukienda RUWASA, wameshaikabidhi Mamlaka ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Aweso aende akaiamshe hii miradi. Wananchi wa Kakese na Mwamkulu wanasubiria hii miradi ikamilike ili waweze kupata maji kama yeye alivyosema, maji hayana mbadala, na ni ukweli usiyopingika kwamba maji hayana mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hii miradi iende ikakamilike ili iweze kuwahudumia wananchi wangu wa Jimbo la Mpanda Mjini. Ninaamini huko waliko wananisikia, ninaongea Mheshimiwa Mbunge wao hapa, message imefika na ninaomba kama kuna uwezekano, kama ni Waziri au Naibu Waziri, basi waende wakatembelee kwenye hizi kata ili wakaone adha ambazo wananchi wanazipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninamshukuru Mheshimiwa Waziri. Kipindi cha kampeni, yeye na Mheshimiwa Mgombea wa Urais walikuja kwenye jimbo langu, na mimi kama mgombea kipindi kile nilimwomba sana aende akaitembelee Kata ya Magamba, lakini akaniambia ndugu yangu Sumry, mimi sasa hivi siyo Waziri, hapa nimemsindikiza tu Mheshimiwa Rais kuja kuhakikisha kwamba tunapata kura za kutosha, lakini ninakuahidi baada ya Mheshimiwa Rais kuchaguliwa, na Mungu akijalia nikawa Waziri wa Maji, nitahakikisha hiyo Kata ya Magamba tunakwenda kupeleka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye jimbo langu, hii Kata ya Magamba na ilikuwa commitment yangu kwa wananchi kwamba nitapambana usiku na mchana, nitashawishi kuhakikisha kwamba wanapelekewa maji. Ziko dalili, nimeongea na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mpanda ameniambia ziko dalili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili peke yake hazitoshi. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti hii awapelekee maji wananchi wa Kata ya Magamba na watamwandika kwenye historia kwa sababu kata hii ni kata kubwa, lakini kuna kisima kimoja na wananchi wote wanaenda kuteka hapo maji kwenye kisima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akienda kukitembelea hiki kisima anaweza akakuta ndoo zaidi ya 2,000 zinasubiria huduma ya maji. Kwa hiyo, ninaomba sana chondechonde Mheshimiwa Aweso anisaidie, aniokoe kwenye hili eneo, wananchi wa Kata ya Magamba nao waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri amekuja kwenye Mkoa wa Katavi mimi nikiwa Meya na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Katavi tukamsukuma kuhakikisha kwamba...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia kwa kuunga mkono hoja.

MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongelea mradi ule wa gridi ya Taifa, nafikiri Mheshimiwa Waziri amenielewa, tumeona na tunaomba a-push ili mradi huu uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mpanda Mjini kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mbunge wao, niendelee tu kuahidi kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya kwenye Jimbo letu la Mpanda Mjini. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jimbo letu la Mpanda Mjini limepiga maendeleo makubwa sana. Ninaomba tumpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri ambao anashirikiana nao katika Ofisi yake. Ni ukweli usiopingika kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 16, Machi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa kwenye jimbo langu la Mpanda Mjini. Kwa namna ya pekee ninamshukuru sana sana sana kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye jimbo hili. Ametatua kero za wananchi wengi, lakini amesikiliza changamoto za wananchi wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, mimi kama Mbunge wa jimbo nilipata fursa ya kufikisha hoja zangu kwa maana ya changamoto za Jimbo la Mpanda Mjini, na Mheshimiwa Waziri Mkuu alizichukua na ninaamini katika bajeti ijayo zitafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, ninapenda kuwashukuru viongozi wangu wa Mkoa wa Katavi, kwa maana ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Mwanamvua Hoza Mrindoko kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwenye Mkoa wetu wa Katavi. Pia, na dada yangu Jamila Yusuf Kimaro, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, naye kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye wilaya yangu ya Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeeleza wazi mambo mengi ambayo yalitekelezwa katika kipindi kilichopita ambacho tunaenda kuishia mwezi Juni, lakini matazamio na matarajio ya bajeti ijayo. Sasa mimi nitajikita kwenye maendeleo kwa sababu Mkoa wa Katavi ni mkoa mpya na mambo mengi yalikuwa hayajafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na eneo la nishati kwa maana ya umeme. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kwenye mkoa wetu kwa kuhakikisha Mkoa wa Katavi, unaunganishwa na gridi ya Taifa. Kwa kweli watu wa Mpanda sasa hivi nao wamekuwa kama watu wa mikoa mingine, lakini kubwa zaidi imepunguza mzigo kwa TANESCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu na mkoa wetu wa Katavi tulikuwa tunatumia generators ambazo zilikuwa zinaendeshwa kwa gharama kubwa, lakini kwa namna Serikali ilivyofikisha gridi ya Taifa, tunaamini sasa gharama za TANESCO zimeondoka na tunaamini sasa TANESCO inaanza kupata faida kwenye eneo letu la Mkoa wa Katavi, na pia kwenye jimbo langu la Mpanda Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo la TANESCO, niendelee kuwaomba watu wa TANESCO, Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie na watu wa Wizara ya Nishati watusaidie kupeleka kwenye maeneo ambayo yanahitajika ujazilizi wa umeme. Pale kwenye eneo langu la Mpanda Mjini kuna kata ambazo bado zina changamoto, ni kata ambazo ziko mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mpanda unakua kwa kasi. Kwa mujibu wa Sensa, Mkoa wa Katavi unakua kwa karibia asilimia saba kila mwaka. Kwa hiyo, utaona ni namna gani Mkoa wa Katavi unavyokua kwa kasi na Mpanda Mjini ndiyo kitovu cha maendeleo ya mkoa wetu. Kwa hiyo, tunapoongelea kukua kwa asilimia saba, tafsiri yake ni kwamba asilimia saba hiyo itatafsirika kwenye jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba sana kwenye Kata za Shanwe ambapo umeme umefika lakini kuna maeneo mapya ambayo yanajengwa bado umeme haujafika na ningeomba ufike. Vilevile, kwenye kata ya Kazima nako umeme umefika lakini bado kuna maeneo mapya ambayo yamejengwa na umeme bado haujafika. Kata ya Nsemulwa, Kata ya Misunkumilo, Kata ya Magamba, Kata ya Kakese, na kata ya Mwamkulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo bado tumefikishiwa umeme, lakini kwa kuwa kuna makazi mapya yanajengwa, kwa hiyo, kuna uhitaji mkubwa wa maeneo yale mapya. Kwa hiyo, ningeomba sana Wizara ya Nishati katika bajeti ijayo waangalie namna ya kutuongezea bajeti ili umeme uweze kufika kwa wananchi, nao wafurahi na watabasamu kama Mheshimiwa Rais alivyotuahidi tabasamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hilo hilo ningeomba kuiomba Serikali itusaidie kujenga ile njia ya umeme ambayo sasa hivi kuna kazi inaendelea kufanyika pale Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya Sumbawanga, lakini mradi huu unatakiwa uje Mkoa wa Katavi ufike pia mpaka Kigoma ili sasa tuondokane na changamoto kabisa kwa sababu tutakuwa na maeneo mawili ambayo tunategemea ya umeme hata ikipata changamoto, njia hii tutakuwa tunatumia njia nyingine ili kuendelea kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka eneo hilo, niende sasa kwenye eneo la TARURA. Ninakiri wazi kwamba TARURA inafanya kazi nzuri, na kwenye jimbo langu imefanya kazi nzuri, madaraja mengi yamejengwa na tunafurahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi na Mheshimiwa Lupembe tunapakana majimbo yetu, na juzi tu hapa tumepata mkandarasi anakwenda kujenga daraja la karibia shilingi bilioni tatu ambalo linapakana na Kata ya Itenka - jimbo la Mheshimiwa Lupembe na Kata ya Mwamkulu ambayo ni jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa fedha hizi alizotuletea, lakini bado tuna changamoto kwenye eneo hilo la jimbo langu na Mheshimiwa Lupembe, kuna daraja lingine ambalo linaunganisha Kata ya Kakese kwenye jimbo langu na Kata ya Itenka kwenye jimbo lake Mheshimiwa Lupembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili lilijengwa, lakini bahati mbaya lilisombwa na maji. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali irudishe huduma pale kwa sababu tunaamini daraja hili likijengwa litawasaidia sana wananchi wa majimbo yetu haya mawili kuweza kufanya biashara na kuongeza uchumi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la TARURA niendelee kuiomba sana TAMISEMI watusaidie kwa kweli kutuangalia kibajeti. Sisi Mkoa wa Katavi kwa neema ya mvua, basi sisi tunaweza tukawa ni namba moja kwenye nchi hii. Tumepata neema ya mvua kubwa na mazao yamelimwa sana na tunaamini wananchi wetu watavuna mazao kwa wingi katika msimu huu, lakini mvua hizi zimebadilika kuwa changamoto kwenye miundombinu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaombe ndugu zetu wa TARURA waweze kutuongezea fedha ili tuweze kwenda kukarabati hizi barabara ambazo zimeharibika katika kipindi hiki cha mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuwashukuru, wanafanya kazi nzuri na kwa kweli Mungu awabariki sana na Mungu ambariki Mheshimiwa Waziri, Mungu aendelee kumbariki Mheshimiwa Rais, hata Mtendaji Mkuu wa TARURA anafanya kazi nzuri. Sisi Waheshimiwa Wabunge tukimpigia simu amekuwa ni msikivu, anatusikiliza na anatatua changamoto zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hilo hilo la barabara, Mji wa Mpanda ndiyo kitovu cha Mkoa wa Katavi kama nilivyosema awali. Tunazo barabara za lami karibia kilometa 20 zimejengwa kwenye jimbo langu, lakini hazina taa za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana ndugu zangu viongozi wangu wa Wizara hii ya TAMISEMI watusaidie angalau kila mwaka tupate bajeti kidogo ambayo itaendelea kuzipunguza hizi barabara, at least katika miaka mitano ijayo basi tuwe tumemaliza hizi barabara kuziweka taa za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, tunapoweka taa za barabarani kwenye maeneo ya miji yetu, tunasaidia wananchi wetu, wafanyabiashara wadogo wadogo, wachoma mahindi, wachoma ndizi na wafanyabiashara wadogo wadogo wananufaika na haya maeneo hasa wakati wa jioni wanaweza kufanya biashara zao. Kwa hiyo, niendelee kuomba sana sana sana kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la TARURA pia tuna fedha za mfuko wa jimbo...

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, nashukuru sana.