Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hemed Sumry Haidary (1 total)

MHE. HAIDARY H. SUMRY aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kupunguza riba za mikopo ya biashara katika mabenki ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa mikopo yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Haidary Hemed Sumry, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kulikumbusha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali haliingilii moja kwa moja upangaji wa viwango vya riba za mikopo katika benki za biashara zinazofanya shughuli zake hapa nchini. Aidha, viwango vya riba katika benki hizo huamuliwa kwa kuzingatia misingi ya soko, ikiwemo viwango vya mfumuko wa bei, vihatarishi vya mikopo kutolipwa, gharama za uendeshaji wa benki husika pamoja na kiwango cha faida kinacholenga kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria na za kiusimamizi na kuwezesha benki za biashara kutoa mikopo kwa riba nafuu zaidi, ikiwemo kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei, ambao ni moja ya kiashiria muhimu kinachotumika katika kukokotoa na kuamua riba inayotozwa kwenye mikopo na benki hizi za kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanikisha azma hiyo, Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kufanya mabadiliko katika viwango vya riba vya Benki Kuu (Central Bank Rate) kuendana na mwelekeo wa kiuchumi, ili kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki ndani ya wigo, huku ikiendelea kuhakikisha uwepo wa kiwango cha kutosha cha ukwasi kwenye uchumi, ili kuchagiza upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha mfumo wa ulinganishi wa bei unaojulikana kama Price Comparator System. Mfumo huu unaongeza uwazi kuhusu viwango vya riba na gharama zinazotozwa na taasisi mbalimbali za kifedha, hivyo, kuwasaidia wakopaji kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma za mikopo wanazozihitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu vilevile unachochea ushindani miongoni mwa benki za kibiashara, jambo linaloweza kuchangia kupungua kwa gharama za mikopo kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza benki na taasisi za fedha kutumia kanzidata ya taarifa za wakopaji (Credit Reference Bureau), ambayo hutoa taarifa za kihistoria za ukopaji na ulipaji wa madeni ya wakopaji. Mfumo huu hupunguza wasiwasi wa benki kuhusu vihatarishi vya mikopo kutokulipwa, hivyo kusaidia kupunguza gharama za tathmini ya mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)