Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwanahamis Athumani Munkunda (2 total)

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Chuo cha Madini Mkoa wa Shinyanga ili kujenga uwezo kwa Vijana na Wanawake katika sekta hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanahamisi Athumani Munkunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Mkoa wa Shinyanga katika sekta ya madini, pamoja na uhitaji wa kuwajengea uwezo wananchi wake, wakiwemo vijana na wanawake katika shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini mbalimbali hususan madini ya almasi na dhahabu yanayopatikana mkoani humo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, Serikali inaendelea kutumia vyuo vyake mbalimbali kufundisha taaluma za madini na endapo itaonekana kuna umuhimu wa kimkakati wa kuanzisha Chuo cha Madini mkoani humo, hatua stahiki zitachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inatoa elimu kwenye tasnia ya madini kupitia vyuo vilivyomo Dar es Salaam, Dodoma, Tabora na Arusha. Itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya vitendo kupitia Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kupitia vituo vya mfano vilivyopo hapa nchini na vile vitakavyojengwa, ikiwemo Kituo cha Mfano cha Mwakitolyo ambacho kinachotarajiwa kujengwa Mkoani Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitoe wito kwa wananchi hasusan vijana wajitokeze kunufaika na huduma za mafunzo zinazotolewa na vyuo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Chuo cha Madini Dodoma (MRI) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo Arusha, ahsante sana.
MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kituo cha Umahiri eneo la Mwakitolyo kutokana na ushiriki mkubwa wa wachimbaji wa madini wanawake na vijana?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanahamisi Athumani Munkunda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Mwakitolyo ni moja ya maeneo ambayo Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inapanga kujenga vituo vya mfano vya uchenjuaji madini ya dhahabu kwa kutumia teknolojia ya Carbon-in-Pulp (CIP) kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Ujenzi wa vituo hivi ambavyo vingine viko Mikoa ya Geita, Mbeya na Mara ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwaendeleza na kuwakuza wachimbaji wadogo nchini kupitia Shirika la STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi wa kujenga Kituo cha Mwakitolyo ameshapatikana, na taratibu za kimkataba zikikamilika, ujenzi utaanza. Hatua ilivyofikiwa hadi sasa ni kukamilika kwa usanifu wa kituo, na kituo hicho kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kuchakata kiasi cha tani 120 kwa siku.