Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Suleiman Mohamed Rashid (4 total)

MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi na stahiki za Walimu wanaosahihisha Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua na kuniamini katika nafasi hii ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera. Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita ni mitihani muhimu ambayo usahihishaji wake hufanyika kwa baadhi ya walimu kukusanywa katika vituo maalum kwa ajili ya jukumu hilo unaozingatia muda maalum, usalama, usiri, mazingira wezeshi na ubora wa kazi.

Mheshimiwa Spika, stahiki za Walimu wanaosahihisha Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita hulipwa kwa kuzingatia miongozo ya usahihishaji wa Mitihani kwa kipindi husika. Ili kuleta ufanisi wa kazi hiyo, miongozo hiyo imeendelea kuboreshwa mara kwa mara. Serikali itaendelea kuboresha maslahi na stahiki za walimu katika usahihishaji wa mitihani ya Taifa ili kuimarisha na kuongeza ufanisi wa kazi hiyo.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje katika utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipanga kikamilifu katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 sambamba na mitaala iliyoboreshwa kwa kufanya yafuatayo:-

(i) Kuongeza miundombinu kwenye shule zilizopo;

(ii) Kuendelea na ujenzi wa shule mpya zikiwemo shule za mkondo wa Amali;

(iii) Kutoa mafunzo kazini kwa walimu ili kuendana na mahitaji ya mtaala mpya;

(iv) Kuimarisha uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari; na

(v) Kutoa ajira mpya za walimu ambapo katika mwaka 2024/2025 kibali cha ajira mpya 12,678 kilitolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali imezindua rasmi Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na Mpango wa Pamoja kati ya Waajiri, Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo Vikuu ili kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa. Aidha, Serikali inafanya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura 353 ili kuendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza: -

Je, lini Serikali itakipatia gari Kituo cha Polisi Mwera ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshakipatia Kituo cha Polisi Mwera kilichopo Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi magari mawili mapya namba PT 5672 Toyota Land Cruiser Pickup na PT 5954 Toyota Double Cabin Pickup ili kutoa huduma za polisi katika eneo la Mwera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza: -

Je, kero ngapi za Muungano zimetatuliwa mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imefanikiwa kutatua na kupatia ufumbuzi jumla ya hoja 15 kati ya hoja 18 za Muungano zilizokuwa zikijadiliwa na pande zote mbili za Muungano. Hivyo, kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano zilizokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.